Friday, March 02, 2012

SIMULIZI YA KOSA LANGU SEHEMU YA ...7...

 AUTHOR ADELA DALLY KAVISHE


Wakati Joyce akiwa anashangaa kumuona Maliki akiwa na mwanamke tena huku wakiwa wamekumbatiana na kupeana mabusu motomoto bila ya kujali Maliki alimgeukia Joyce na kusema "Hivi wewe una mamlaka gani ya kuniuliza huyu ni nani?" Joyce alimjibu kwa uchungu "kweli Maliki unanijibu kama hunijui hivi nimekukosea nini mimi unanifanyia yote haya umeona haitoshi kuwa na wanawake nje umeamua kuwaleta kabisa na hapa ndani"

 Kwa dharau yule mwanamke aliyekuwa na Maliki alicheka na kumwangalia Maliki "Mpenzi nimechoka bwana huyu nani mbona anaongea sana" alisema yule mwanamke Joyce kusikia hivyo alishikwa na hasira na kumsogelea yule mwanamke kwa nia ya kumpiga "Wewe unauliza mimi ni nani? mwendawazimu mkubwa usiye kuwa na haya kuchukua mabwana za watu" alisema Joyce huku akiwa amemkamata yule mwanamke ambaye alionekana ana umbo kubwa kuliko la Joyce wakati akiwa anafanya hivyo Maliki alimvuta na kumsukuma maskini Joyce alianguka chini huku akiwa analia kwa uchungu .

Maliki alimsogelea na kusema "Unataka kujifanya wewe ni kichaa nitakufukuza pakashume mkubwa nimekuokota huko barabarani unataka kujifanya unajua zaidi maskini mkubwa wewe" aliongea maneno hayo Maliki bila hata ya huruma Joyce alibaki analia na Maliki akamchukua yule mwanamke wake wakaelekea chumbani kulala na kumuacha Joyce akiwa anaendelea kulia mdogo wake Joyce alikuwa amelala lakini alishtuka baada ya kusikia malumbano yakiwa yanaendelea alitoka na kuelekea sebuleni ambapo alimkuta dada  yake analia alimsogelea kwa masikitiko huku akiwa anafikicha macho kutokana na usingizi.

"kuna nini dada mbona hivi mimi nimechoka kila siku unalia bora tuondoke " alisema James huku akiwa anamuangalia dada yake ambaye alinyanyuka na kumshika mdogo wake huku akisema " Hapana mdogo wangu usijali mimi niko sawa" James kwa hasira akamwambia " huwezi kunidanganya dada nimesikia kila kitu shemeji Maliki anakunyanyasa sana bora tuondoke kama ni shule hata mimi nitaacha ili tutafute pesa tuondoke dada" aliongea James huku machozi yakiwa yanamtoka".


 Joyce alinyamaza kimya akamshika mdogo wake na kuelekea chumbani ambapo siku hiyo Joyce alilala na mdogo wake hadi asubuhi  aliamka na  kumkuta yule mwanamke na Maliki wameondoka ilikuwa ni siku mbaya sana kwa Joyce aliyekuwa na mawazo na masikitiko zilipita kama siku mbili akiwa anaendelea kuishi maisha ya shida Joyce alijigundua kuwa ni mjamzito kwa mara nyingine kitu ambacho kilimuumiza sana kichwa kwa mawazo kuwa  atafanya nini, ilimbidia amueleze Maliki hali halisi ambapo kama kawaida Maliki alimtaka aitoe hiyo mimba.

Joyce aliyekuwa hana la kufanya ilimbidi amsikilize kile alichokuwa anataka basi aliitoa tena ile mimba na kurudi nyumbani huku akiwa anaishi kwa mateso bila kujua nini hatima ya maisha yake kila kukicha kwa Maliki vituko vilikuwa haviishi siku moja Joyce akiwa amelala chumbani aliwaza moyoni mwake na kusema "hivi nini hatima ya maisha yangu si nitakufa mimi napigwa sana,nikipata mimba natoa ,,Eee Mungu naomba unisaidie, sitaki James ateseke angalau yeye angesoma, lakini nitaweza kweli kuendelea kuishi katika hali hii si nitakufa nimuache mdogo wangu akiteseka" aliwaza Joyce huku akiwa analia kwa uchungu.

 Maisha yaliendelea hadi siku moja mida ya jioni ambapo siku hiyo Maliki alikuja na mwanamke mwingine na kumtaka Joyce na mdogo wake waondoke ilikuwa ni saa moja za jioni Joyce alilia na kumuomba sana Maliki asiwafukuze lakini hakuswasikiliza kwani yule mwanamke aliyekuja naye alikuwa hataki kina Joyce waendelee kuishi pale hivyo hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kuondoka huku wakifukuzwa kwa maneno ya kashfa waliondoka bila ya kujua wapi wanaenda walitembea huku na kule ili kutafuta sehemu ya kujipumzisha kwa usiku huo.

walirudi katika maisha ya mitaani ambapo yalikuwa ni maisha ya shida sana kwasababu walikuwa hawana chochote siku moja kutokana na kuishi maisha ya tabu  James alianza kuumwa homa lakini dada yake alikuwa hana hata hela ya kununua dawa ilimbidi aombe watu ili wamsaidie ambapo walimsaidia kununua dawa lakini siku zilivyozidi kwenda hali ya James ilikuwa mbaya kutokana na hivyo Joyce ilimbidi aanze kujiuza ili apate pesa za kumpeleka mdogo wake hospitalini, alijiingiza katika biashara ya ukahaba ili aweze kupata pesa za mahitaji mbalimbali, wakati mwingine iliwabidi walale njaa kutokana na hali halisi ya maisha.

 Pesa alizokuwa anapata Joyce zilikuwa hazitoshi kuwasaidia na huku  hali ya James haikuwa nzuri hatimaye alifariki dunia. ni siku ambayo Joyce alilia kwa uchungu bila ya kujua nani atamsaidia alisaidiwa na watu mbalimbali wa mtaani katika mazishi ya mdogo wake  na baadaye alibaki pekee bila kujua ataenda kwa nani ili aweze kumsaidia. Je nini hatima ya maisha ya Joyce usikose sehemu ya nane................

2 comments:

Anonymous said...

kweli simulizi ni nzuri sana na inasikitisha sana yaani hadi machozi yamenitoka jamani joyce

lulu ibrahim said...

dahhhhhhhhhh maisha ya joice kuumia kila kukicha ahsante dda kwa histria nzuri

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...