Jumatatu, Aprili 29, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI ........SURA YA ....8.......


ILIPOISHIA:
Kilikuwa ni chumba kizuri sana, ilinibidi nianze kufundishwa kutumia kila kitu kwasababu nilikuwa sijui chochote, lakini Mama Bilionea alinionyesha upendo wa hali ya juu kwani hata kazi niliyokuwa natakiwa kuifanya sikuiona muda mwingi nilikuwa nikiangalia video, niliishi kama mtoto wake wa kumzaa na alikuwa akinipa pesa nyingi sana.JE NINI KINAENDELEA ....USIKOSE SURA YA ....8...

INAPOENDELEA
Baada ya mwezi mmoja nikiwa naendelea kuishi na Mama Bilionea. Maisha yangu yalibadilika kwani nilikuwa sina matatizo yoyote. Ijapokuwa tatizo kubwa lilokuwa moyoni mwangu  ni kuhusu Mama yangu kwenda kutibiwa India, na Baba yangu aachiwe huru  kutoka gerezani.Siku moja nilikuwa nimejipumzisha sebuleni huku nikiwa nazungumza na nafsi yangu "Maisha yangu yana msalaba mzito sana, hapa nilipo naishi maisha ya kifahari lakini sijui nini hatima ya Mama yangu na hata Baba yangu. Kama ikiwezekana Mama Bilionea angenikopesha kiasi cha pesa ili nimpeleke Mama India akatibiwe. Halafu mimi nitamfanyia kazi zake bila  ya kunilipa chochote sijui atakubali?" Nilikuwa nikiwaza nakujiuliza maswali mengi sana bila ya kupata majibu.

Mama Bilionea alifika muda huo akiwa anatokea katika shughuli zake za kila siku. "Haujambo Kandida, habari za hapa nyumbani" Ilikuwa ni sauti ya Mama Bilionea ambayo nilihisi kuisikia kwa mbali lakini kutokana na mawazo niliyokuwa nayo nilikuwa kimya kana kwamba sikumsikia akinisalimia "Wewe mtoto, unawaza nini? Mbona nakusalimia umekaa kimya?" Mama Bilionea alizungumza kwa sauti kali kidogo "Shikamoo Mama, samahani nilikuwa sijakusikia, nilipitiwa kidogo Mama" Nilinyanyuka huku nikiwa naongea kwa sauti iliyo na kigugumizi".

 Mama Bilionea alinisihi niketi "Una matatizo gani, si nilishakuambia kama kuna tatizo lolote usisite kuniambia".Baada ya Mama Bilionea kuniambia nimueleze matatizo niliyonayo, niliamua kumueleza kila kitu kwamba nahitaji anisaidie kiasi cha pesa kwaajili ya matibabu ya Mama na siku zote nitaendelea kufanya kazi katika nyumba yake bila malipo. "Kandida mwanangu usijali kuhusu hali ya Mama yako mimi nitakusaidia" nilijihisi kupata faraja moyoni mwangu "Asante sana Mama Mungu atakuzidishia.


Mama Bilionea alinyanyuka na kuelekea chumbani kwake alipoingia chumbani aliniita na kunitaka nimfuate , Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika chumba cha Mama Bilionea tangu nilipoingia katika ile nyumba ya kifahari. ndani ya kile chumba kulikwa kumepambwa na vioo vya dhahabu kila kona.Na kila sehemu ya chumba kuanzia mapazia hadi shuka la kitandani vyote vilikuwa vya rangi nyekundu. "Mama chumba chako ni kikubwa na kizuri sana".

 Nilizungumza huku nikiwa napepesa macho huku na kule nikishangaa uzuri wa kile chumba. "Karibu uketi Kandida" Nilijisogeza na kuketi katika sofa lilokuwepo pembezoni kidogo na kitanda, "Kuna jambo ningependa ulifahamu Kandida, wewe ni msichana mdogo na mrembo sana, Nataka nikusaidie ili na wewe uweze kuwa tajiri kama mimi" alizungumza Mama Bilionea huku akinitazama kwa umakini "Kweli Mama inawezekana na mimi nikawa tajiri kama wewe, mbona nitafurahi sana kwani nitaweza kuisaidia familia yangu".

Mama Bilionea alinyanyuka na kuchukua kitambaa chekundu kisha akanipa nikishike mkononi "Kandida hicho kitambaa ulichokishika kinaweza kukusaidia wewe kuwa tajiri  maisha yako yote" Nilishangaa kwani kile kilikuwa ni kitambaa tu kinawezaje kunifanya mimi kuwa tajiri Mama Bilionea aliendelea kuzungumza "Usishangae Kandida katika haya maisha inabidi uwe mjanja na mwenye kufahamu mambo mengi, kwani yawezekana kila mtu akawa tajiri, kwani wewe hupendi kuwa na pesa nyingi na nyumba ya kifahari kama hii ya kwangu?" Aliniuliza Mama Bilionea "Napenda kuwa tajiri Mama kwani nimeishi maisha ya shida sana nisaidie na mimi niweze kufanikiwa" Nilizungumza huku nikionyesha uso wenye furaha "Sasa usijali unaweza kuwa tajiri ila inabidi ukubaliane na jambo moja, unatakiwa kupoteza kitu cha muhimu sana kwako ili uweze kufanikiwa kama mimi.Alisema Mama Bilionea.

Nilinyamaza kimya kidogo "Kitu gani hicho Mama, kwani kwa shida nilizonazo nipo tayari kufanya lolote ili nifanikiwe" Mama Bilionea alicheka kidogo "Nimefurahi kusikia hivyo mwanangu sasa leo tuishie hapo lakini hicho kitambaa nenda nacho utalala nacho kitandani kila siku usikiache hata siku moja, umeniskia Kandida usikitupe hicho kitambaa" Huku nikiwa nimekishikilia kile kitambaa mkononi nilinyanyuka na kusema "Sawa asante sana nitakitunza vizuri" Sikujua nini maana ya kile kitambaa niliondoka na kuelekea chumbani kwangu nakukiweka kile kitambaa kwenye kabati langu la nguo nikiwa pale chumbani nilikuwa nikiwaza "Hivi kweli Mama Bilionea anaweza kunisaidia mimi nikawa tajiri kama yeye, na hiki kitambaa sijui kina maanisha nini? Na tena ameniambia hiki kitambaa ndiyo kitanifanya niwe tajiri. NINI KITAENDELEA USIKOSE .....SURAYA...9


Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

mungu wangu htamwambia hamuue mama ake.

Unknown alisema ...

Yaani nimeipenda sana

emuthree alisema ...

Ahsante sana Mungu,...tupo pamoja mpendwa, ahsante kwa kisa hiki

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom