Jumapili, Aprili 07, 2013

SIMULIZI YA .....BADO MIMI.... SURA YA ....4.......


ILIPOISHIA
Nilipofika nyumbani niliwakuta wadogo zangu wakiwa wamekaa nje, Renata ambaye alikuwa darasa la tatu na Tumaini alikuwa darasa la kwanza. Waliponiona walinikimbilia huku wanalia “Dada Kandida,, Dada Kandida Baba , baba, baba”Alikuwa akilia Renata huku akinivuta katika gauni langu nilishindwa kuelewa Baba amepatwa na kitu gani? “Renata Baba yuko wapi? Mnalia nini? Baba amefanyaje” Nilimuuliza mdogo wangu wa kike “Baba amechukuliwa na watu, wamempiga Baba”

INAPOENDELEA

Baba amechukuliwa na watu, wamempiga Baba” Alinijibu kwa sauti yenye  kigugumizi, Nilihisi kuchanganyikiwa kwani sikuamini kile alichokuwa anakisema mdogo wangu. Nilikimbia na kuelekea kwa Mama Keku kabla hata sijafika Mama Keku aliniita “Kandida nipo huku njoo” alikuwa ameketi jikoni kwake akiandaa chakula. Nilisogea huku nikiwa na shauku la  kutaka kujua Baba yangu ameenda wapi?"
 Karibu uketi mwanangu, aliongea Mama Keku huku mimi nikiwa namuangalia "Mama Keku Baba yangu amepatwa na kitu gani?" Mama Keku alijaribu kuniliwaza na baadaye akaamua kunieleza hali halisi ya kile kilichotokea.

 “Kandida wewe ni msichana mkubwa, fikiria Mama yako na wadogo zako wanakutegemea wewe. Baba yako amepelekwa Polisi” akiwa anaendelea kuongea yale maneno nilihisi kama yananichanganya kichwa changu kabisa. “Ati unasema Baba yangu amepelekwa Polisi, amefanya nini? Baba yangu eeh Mungu balaa gani hili jamani mbona tunateseka hivi” Nijikuta nimekaa chini huku nikilia kwa sauti  Mama Keku alijitahidi sana kunibembeleza lakini sikutaka kumsikia.Niliamua kuchukua maamuzi ya haraka na kwenda hadi kituo cha polisi.

“Wewe binti una matatizo gani? Unalia nini?” Ilikuwa ni sauti ya Askari ambaye nilimkuta pale kwenye mapokezi ya kituo cha polisi “Namtaka Baba yangu jamani, namtaka Baba yangu” Yule askari akaniuliza “Binti sasa unavyolia sikuelewi unamtaka Baba yako yuko wapi? ametekwa? au amefanyaje” Nilikuwa nalia kwa uchungu “Baba yangu amekamatwa na Polisi, na Mama yangu amelazwa hospitalini sisi tutabaki na nani? Namtaka Baba yangu” Kulikuwa na askari mwingine kwa pembeni ambaye alikuwa ni mwanamke alinichukua na kuanza kunibembeleza huku akinisihi ninyamaze na kumuelezea taratibu. 


Baadaye walinuliza jina la Baba “Anaitwa Kitali Shirima” Askari mmoja akacheka “Hahahaha huyo mzee aliyeletwa hapa kwa kosa la kuiba pesa kutoka katika kiwanda cha plastiki” Nilimuangalia Yule askari na kumwambia “Baba yangu siyo mwizi jamani hawezi kufanya hivyo” Nilihisi kama sielewi kabisa kile nilichoambiwa eti Baba yangu mwizi? Hapana haikuniingia akilini.  Niliomba niende kumuona "Subiri hapo Baba yako akaitwe atakuambia ameiba nini?"

Baba aliitwa, kwa namna alivyokuwa anaonekana alikuwa amechoka na huku akionekana kuwa na majeraha mikononi na kwenye paji la uso wake. Machozi yalinitoka huku nikimuangalia kwa uso uliokosa amani. Baba alinisihi nirudi nyumbani na nisimwambie Mama chochote kuhusu hali yake. “Mwanangu wewe nenda nyumbani mimi nitakuwa salama, nitatoka siku yoyote usijali. Nenda ukawaangalie vizuri wadogo zako pamoja na Mama yako usimwambie chochote kuhusu mimi." Muda wa mazungumzo uliisha na Baba alirudishwa katika chumba cha Mahabusu.


Niliondoka na kuelekea nyumbani nafsi yangu ilikuwa inaumia sana “Chanzo ni umasikini , Baba yupo gerezani kwasababu ameiba pesa kwaajili ya matibabu ya Mama, lakini kwanini aliiba jamani,kwani ametenda kosa na sasa hakuna mtu wa kutusaidia, sasa sijui hata nifanyeje nani atanisaidia mimi” Niliongea na nafsi yangu huku nikiwa nimepoteza matumaini. Nilipofika nyumbani Mama Keku alinipa matumaini kuwa nisikate tamaa Mungu atatusaidia Mama atapona na Baba atatoka gerezani. Niliingia jikoni na kundaa chakula kwaajili ya wadogo zangu na baadaye nilirudi hospitalini kumwangalia Mama.

Tayari Mama alikuwa amefanyiwa upasuaji, na kwa muda nilioenda alikuwa amepumzika  nilibaki pale hospitalini mpaka asubuhi. Ambapo baadaye Mama alizinduka na kwa wakati huo alikuwa akihisi maumivu kutokana na kidonda cha upasuaji na nyuzi alizoshonwa ndiyo zilikuwa zinampa maumivu makali. Daktari alinisihi nisiwe na waswasi hali ya Mama itatengamaa. 

Baada ya wiki mbili tokea Mama afanyiwe upasuaji hali yake ilianza kutengamaa hivyo aliruhusiwa kurudi nyumbani, kwa wakati wote huo Mama alipokuwa akiniuliza kuhusu Baba nilimwambia Baba amesafiri.Lakini aliporudi nyumbani ilimchukua siku chache akafahamu ukweli kuwa Baba alikuwa amekamatwa na Polisi “Masikini mume wangu chanzo ni mimi,Mungu tusaidie” Mama alihuzunika sana baada ya kufahamu kilichomtokea Baba ambapo kwa wakati huo Baba alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. 


Maisha yaliendela hali ya Mama ilikuwa ni njema aliweza kuandaa chakula na kumpelekea Baba gerezani mara kwa mara. Kwa upande wangu nilikuwa nimekaa nyumbani kwa kipindi kirefu bila kwenda shule.Kutokana na hali ya pale nyumbani Mama aliniambia  hawezi kunilipia ada ya shule kwahiyo ilinibidi nibaki nyumbani , ijapokuwa nilitamani sana kusoma lakini kutokana na hali halisi ya maisha ya pale nyumbani sikuwa na namna nyingine yoyote.Nini kitaendelea usikose sura ya ......5..........

Maoni 2 :

Unknown alisema ...

Dah inasikitisha sana

emuthree alisema ...

Kisa muruwa tupo pamoja mpendwa

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom