Jumatatu, Mei 13, 2013

SIMULIZI ....BADO MIMI ....SURA YA .........12..........

 ILIPOISHIA
Baadaye nilipitiwa na usingi, nikiwa nimelala niliota ndoto ya ajabu sana. Nilikuwa namuona Baba yangu akiniita "Mwanangu Kandida njoo, niokoe, njoo niokoe,,usiniache huku shimoni, toka huko ulipo njoo nateseka sana" Ilikuwa ni sauti ya Baba nikiisikia nikiwa ndotoni" Wakati nikiwa najaribu kumsogelea Baba niliona kitambaa chekundu kikimwaga damu. Wakati wote huo ilikuwa ni ndoto nilishtuka sana na kuita kwa nguvu "Baba, Babaaaaaa" Mama Bilionea alishtuka na kuja chumbani kwangu kwani sauti yangu ilikuwa kali sana.............NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA .....12,,.........

INAPOENDELEA
 Nilikuwa natetemeka kama mtu aliyekuwa anahisi baridi kali, huku jasho likinibubujika kwa wingi mithili ya maji yakitiririka usoni. Mama Bilionea aligonga mlango wa chumbani kwangu "Kuna nini wewe Kandida, mbona unapiga kelele usiku  wa manane?" Nilinyanyuka haraka kitandani nakuelekea kufungua mlango "Mama nilikuwa naota ndoto mbaya sana, hapa nilipo naogopa hata kulala peke yangu." Mama Bilionea aliingia chumbani na kuketi kitandani kwangu "Inamaana ndoto ndiyo inakufanya upige kelele kiasi hicho?Ni ndoto gani hiyo?"

 Aliuliza Mama Bilionea huku akiwa ananitizama "Nimeota Baba yangu ananiita nimsaidie lakini ......"Mama Bilionea alikuwa amenikazia macho kabla sijamaliza kuzungumza akasema "Unajua wewe mtoto una mambo ya ajabu sana, ule mkufu niliokupa uuvae  uko wapi? na mbona haujauvaa?" Nilishangaa kumuona Mama Bilionea akiwa mkali kidogo huku akinisisitiza nivae mkufu wa dhahabu alionipa. "Mkufu nimeuweka kwenye kabati kwani sikuona kama ni vyema nikilala huku nikiwa nimeuvaa".

Mama Bilionea alifungua kabati na kunitaka nivae ule mkufu niliuchukua na kuuvaa "Sikiliza nikuambie Kandida huo mkufu ni zawadi nzuri sana kwani utakusaidia usiote tena ndoto za ajabu. Hakikisha unauvaa wakati wote, tizama mimi nimevaa mkufu huu unafanana na wako unanisaidia sana,  ukinisikiliza utaishi vizuri sana lakini tatizo watoto wa siku hizi mkiambiwa mfanye jambo fulani haufanyi ila unafanya vile unavyotaka wewe. Hakikisha huo mkufu unauvaa na usiutoe hata siku moja nadhani tumeelewana." Alinisisitiza Mama Bilionea huku nikiwa namsikiliza kwa umakini "Sawa Mama nimekuelewa, naomba unisamehe kwani sikujua kama huu mkufu natakiwa niuvae hata wakati wakulala, na tena kama utanisaidia nisiote ndoto za ajabu, nakuahidi siwezi kuuvua kamwe." Mama Bilionea alinisihi nilale kwani ilikuwa ni saa nane za usiku. 

Baada ya kuvaa ule mkufu nilijisikia tofauti kwani sikuwa na hofu yoyote nilipanda kitandani na kulala mpaka asubuhi kulipambazuka. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kwangu kwani ni siku ambayo Mama Bilionea angenipeleka katika Duka langu ambalo nilikuwa na hamu sana ya kwenda kuliona.Nilifanya kazi ndogo ndogo za pale nyumbani na baadaye Mama Bilionea alinipeleka dukani kwangu maeneo ya Mwenge karibu na kituo cha daladala. 

Lilikuwa ni duka kubwa sana kuliko nilivyotarajia kwani kwa wakati wote nilifikiri lingekuwa duka dogo. Duka lilikuwa na vipodozi vya aina mbalimbali pamoja na wafanyakazi wanne. Mama Bilionea alinitambulisha "Vijana leo nimemleta bosi wenu ili mfahamiane" Mmoja kati ya wale vijana alinitizama na kusema "Karibu sana bosi tumefurahi kukufahamu mimi naitwa John". Alijitambulisha yule kijana "Asante sana John usijali tutashirikiana pamoja, nawategemea sana katika kuimarisha hii biashara."


Nilikuwa siamini kama yale yalikuwa maisha yangu mapya muda wote nilikuwa nawaza "Hivi ni mimi Kandida, au naota jamani, leo hii na mimi naitwa bosi ninamiliki duka kubwa kiasi hiki?" Nilijiuliza maswali mengi sana huku nikiendelea kumshukuru sana Mama Bilionea kwa kuyabadilisha maisha yangu. Kuanzia siku hiyo sasa maisha yangu yalibadilika niliishi maisha ya kifahari, asubuhi nilikuwa nikipelekwa kazini na dereva  na kurudi jioni. Mama yangu alimshukuru sana Mama Bilionea na kwa kipindi hicho tayari Mama Bilionea alianza kunijengea nyumba maeneo ya Mmbagala ilikuwa ni nyumba nzuri na ya kisasa. 

Siku moja nikiwa natoka kazini kuelekea nyumbani Mikocheni. Nilipofika maeneo ya pale mtaani nilimwambia dereva anipitishe dukani kwa mzee Temba nikanunue vocha. "Mzee Temba habari za masiku, naomba unisaiddie vocha ya mtandao wa voda shilingi elfu tano."Mzee Temba huku akiwa anaipokea ile pesa yangu akanitizama na kusema "Hee! Ni wewe umebadilika sana binti, inaonekana maisha yako yamekuwa mazuri sana.  Hivi bado unaishi na Mama Bilionea? "Aliniuliza Mzee Temba" Hahahahahahaha nilicheka kidogo "Asante Mzee Temba. Bado naishi  kwa Mama Bilionea" Mzee Temba aliniangalia kwa umakini huku akitikisa kichwa akasema "Binti usilolijua ni sawasawa  na usiku wa kiza kinene, kuwa makini sana na huyo Mama siyo mtu mwema kama unavyofikiria" Nilishangaa ni kwanini Mzee Temba amekuwa  akimfikiria vibaya Mama Bilionea, lakini sikutaka kuendelea kuzungumza naye kwani pale dukani kulikuwa na wateja wengi. Nilirudi kwenye gari na kuelekea nyumbani. 

Nilipofika nyumbani moja kwa moja nilielekea chumbani kwangu kupumzika pia nilikuwa nikiwaza sana maneno ya mzee Temba "Usilo lijua ni sawasawa na usiku wa kiza kinene, mmmh huyu Mzee Temba anamaanisha nini? Inamaana kuna mambo ambayo siyajui kuhusu Mama Bilionea? Na wale vijana sikuile waliniita msukule sijui walikuwa wanamaanisha nini? Lakini huu utakuwa ni wivu tu na chuki binafsi. Mama Bilionea ananipenda sana haiwezekani akawa na tabia za uchawi." Nilikuwa nawaza na kujiuliza maswali mengi sana.Maisha yangu yalikuwa mazuri lakini muda wote nilikuwa nawaza kumpeleka Mama yangu India kwaajili ya upasuaji kwani wakati wote huo alikuwa akitumia dawa.

Baada ya miezi mitatu kupita tangu nianze kufanya kazi yangu ya dukani. Maisha yangu yalikuwa mazuri sana sikuwa na wasiwasi wowote, siku moja nikiwa dukani alikuja dada mmoja anataka kununua  mkufu. "Habari yako dada, natafuta mkufu mzuri wa dhahabu" Nikiwa najiamini niliamua kuushika mkufu niliokuwa nimeuvaa ambao nilipewa zawadi na Mama Bilionea "Karibu sana, hapa kuna kila aina ya mkufu hata ukitaka kama huu niliouvaa utaupata."

 Yule dada alinitizama na kusema "Mbona sioni kama umevaa mkufu wowote" Nilishangaa kwasababu mimi nilikuwa najiona nimevaa mkufu kijana wangu wa pale dukani naye alinitizama na kutabasamu "Dada haujavaa mkufu, na huwa haupendi kuvaa mkufu" Sikutaka kuamini kwani nilihisi mkufu niliouvaa ni wa maajabu kwani wote walikuwa hawauoni mimi pekee ndiye nilikuwa najiona nimevaa mkufu "Mmmmh siamini hiki ninachokisikia hapa nilipo nimevaa mkufu inakuwaje hawauon, ni mauzauza gani haya" Nilijikuta nikipatwa na mawazo ghafla huku nikiwa nimenyamaza kimya nikitafakari bila kupata majibu. ..........NINI KITAENDELEA USIKOSE ........SURA YA ...13.......

Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

mungu wangu naomba aseme samahn nimesahau nilijua nimevaa asije kuonekna mweu bure.

Bila jina alisema ...

Hadithi ni nzuri na kila nikiimaliza inakuwa patamu .Nakupa pongezi dada kwa kutupa vitu vitamu na Mungu akubariki maisha na blog yako uiwe ya aina hii

NAAMINI KAMA WATANZANIA WANGEFUNGUA MA BLOGS YA KUELIMISHANA KUPOTEZA MAWAZO KAMA HII TUNGEFIKA MBALI

ADELA KAVISHE alisema ...

Asanteni sana wadau kwa kuendelea kuwa pamoja nami

ADELA KAVISHE alisema ...

Asanteni sana wadau kwa kuendelea kuwa pamoja nami

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom