Jumatatu, Mei 20, 2013

SIMULIZI.......BADO MIMI....SURA YA ....14.......

  ILIPOISHIA
Nilihisi kama nataka kuchanganyikiwa kwa maneno aliyokuwa anazungumza Mzee Temba "Inamaana Mama Bilionea ndiye aliyemuuwa Baba yangu? Mungu wangu akili sasa ndiyo inanifunguka, na yule mchungaji namkumbuka kule hospitalini alisema tumefungwa macho na nguvu za giza. Pia  naikumbuka ile ndoto niliyoota Baba ananiita nimuokoe kabla Mama Bilionea hajanivisha ule mkufu. Huyu Mama ni mchawi eeh Mungu nisaidie nitafanya nini mimi, Mzee Temba naomba unisaidie. .......JE NINI KITATOKEA ...USIKOSE SURA YA 14.......
  
INAPOENDELEA
"Sijui nini hatima ya maisha yangu" Nilikuwa katika wakati mgumu sana huku nikimtizama Mzee Temba "Sikiliza nikuambie binti yangu, jambo la kufanya wewe rudi nyumbani kwa Mama Bilionea na uishi bila ya kuogopa chochote. Na wakati huo ukiwa unapanga ni namna gani unaweza kuondoka. Kwani kwa sasa hata ukisema unaenda nyumbani kwenu Mmbagala, anaweza kuja kukufuata kwani si anapafahamu?" Alikuwa akinishauri Mzee Temba huku mimi nikiwa nimekodoa macho mithili ya mjusi aliyebanwa kwenye mlango, "Lakini mimi naogopa sana, sizani kwama naweza kurudi ndani ya ile nyumba.Ukweli mimi siwezi Mzee Temba".

Aliendelea kunishauri nirudi ila nifanye juu chini yule Mama asigundue chochote kama mimi nimekwisha fahamu tabia yake. Baadaye ilinibidi nimsikilize Mzee Temba alichonishauri na kunyanyuka kuelekea nyumbani huku nikiwa na mawazo sana "Eeeh Mungu naaomba unisimamie, hapa nilipo sijui nini kitatokea katika maisha yangu. Huyu Mama si ataniuwa mimi." Nikiwa natembea taratibu ghafla nilisikia mlio wa honi ya gari "piiiii,piiiiii,piiiiii".

 Kutokana na mawazo niliyokuwa nayo nilikuwa nikisikia mlio wa honi kwa mbali, "Wewe Kandida una matatizo gani? Kama ningelikuwa katika mwendo wa kasi si ningekugonga na gari" Aliongea kwa sauti ya ukali Mama Bilionea aliyekuwa anaendesha lile gari. Niligeuka na kubaki nikimtizama bila ya kuzungumza chochote "Ehee umetoka wapi? Na mbona haujachana nywele na nguo inaonekana haijanyooshwa, hivi una kichaa? Embu panda ndani ya gari twende" Aliongea huku akinitizama kuanzia chini mpaka juu.

Kwa sauti ya upole na iliyojaa wasiwasi mwingi huku nikijikaza nisionekane kama nina tatizo lolote nikasema "Samahani Mama nilikuja dukani mara moja kununua dawa kichwa kinaniuma" Huku nikiwa napanda ndani ya gari la kifahari la Mama Bilionea "Sasa kama unaumwa si unasema mwanangu, pole sana ila siku nyingine kuwa makini unapotembea barabarani kwani unaweza kugongwa na gari, pikipiki na hata baiskeli." Nilikuwa kimya huku moyoni nikiwaza "Yaani huyu Mama ni muuaji mkubwa, anajifanya mpole tena mwenye huruma kumbe nia yake ni kuimaliza familia yangu! Tena naomba Mungu asikumbuke kama sijauvaa ule mkufu".

 Hatimaye tulifika nyumbani, huku Mama Bilionea akielekea chumbani kwake. Na mimi nikiwa natembea kwa kuogopa nilifungua mlango wa chumba changu.  Huku macho yangu moja kwa moja nikiyaelekeza juu ya kitanda, ambapo kulikuwa na kile kitambaa chekundu na ule mkufu.

Niliingia kwa ujasiri wa ajabu huku moyoni nikisali "Mungu nisaidie, ni wewe pekee nakutegemea sina mtu mwingine nisaidie Mungu wangu" Nilivuta lile shuka pale kitandani na kulifunga pamoja na vile vitu bila hata ya kuvishika, na kuviweka ndani ya kabati. kisha nikalifunga kabati na ufunguo. Baada ya hapo nilichukua shuka lingine na kutandika pale kitandani. Nilikuwa na hofu nyingi sana kwani siku hiyo sikuwa na amani hata kidogo. Baadaye nilienda sebuleni na kula  chakula cha usiku pamoja na Mama Bilionea. Nilikuwa  nikijikaza sana asielewe chochote. Haraka baada ya kumaliza chakula nilimuaga  Mama Bilionea kuwa nakwenda kupumzika.



Nikiwa nimelala usiku wa manane niliota ndoto ya ajabu. Nilikuwa nawaona watu wengi wakishangilia na kupiga vigelegele kwa sauti. Wakiimba nyimbo ambazo nilikuwa sizielewi nikiwa ndotoni nilijisogeza hadi wale watu walipokuwa wanaimba. "Mama, Mamaaa, muacheni Mama yangu jamani " Nilikuwa nikilia kwa uchungu, baada ya kuuona mwili wa Mama yangu, ukiwa katikati ya wale watu ambao walionekana kushika visu na mapanga. Na kichwani walikuwa wamefunga vitambaa vya rangi nyekundu. Nilishtuka usingizini huku jasho likinitoka "Mungu wangu ni ndoto gani hii!Inatisha sana Eeeh Mungu msaidie Mama yangu" Nilinyanyuka kitandani huku nikiwa nasali kwani nilijua ile ndoto itakuwa inamaanisha kuna kitu kibaya kinamtokea Mama yangu. 

Wakati nikiwa naendelea kusali nilizisikia zile sauti za wale watu waliokuwa wanaimba kwa mbali, na sasa nilikuwa nimeketi kitandani. Niliogopa sana, nakupata wasiwasi mwingi niliwaza kutoroka usiku huo huo. "Mungu wangu nisaidie, nifanyeje mimi jamani "Wakati huu machozi yalinitoka kwani ilikuwa siyo ndoto tena kwani zile sauti nilikuwa nikizisikia. Akili ikanituma nikimbilie kwenye chumba cha mfanyakazi wa pale nyumbani aliyeitwa Esta Nilifungua mlango huku nikiwa nanyata taratibu nilipofika karibu na chumbani kwa Mama Bilionea nilisikia sauti ikisema "Mama Kandida, Mama Kandida ndiye tunayemuhitaji" Nilihisi kuishiwa nguvu "Mungu wangu Mama Bilionea anataka kumtoa kafara Mama yangu?".

Niliwaza kutoroka usiku uleule wa manane muda huu nilikimbia kuelekea mlango wa kutoka nje. Lakini cha ajabu kabla hata sijafika mlangoni nilikutana na Mama Bilionea. "Unaenda wapi usiku huu wa manane?" Niliogopa sana huku nikishindwa hata kumjibu lolote nilikuwa nataka kuendelea kukimbia Mama Bilionea akaniambia "Huwezi kwenda popote Kandida hapa ni nyumbani kwako, na wewe ndiye mwanangu niliyekuchagua utakayerithi mali zote hizi. Sijui kwanini unaikimbia nyumba yako?"

 Aliongea Mama Bilionea huku akiwa amenikazia macho na mavazi aliyokuwa amevaa ni ya rangi nyekundu na alikuwa amefunga kile kitambaa chekundu. Niliogopa sana nikajipa matumaini na kupata ujasiri wa kuongea "Mama Bilionea naomba niende nyumbani Mama yangu ni mgonjwa" hahahahahahahaha, heheheheheh. Alicheka kwa sauti kali Mama Bilionea na kusema "Unataka kwenda nyumbani usiku wa manane?"

Wewe Kandida mbona umeanza kuwa mtoto ambaye ni muongo?usiwe na tabia mbaya mwanangu si unajua Mama yako nakupenda sana, huwezi kwenda nyumbani usiku huu". Alinijibu Mama Bilionea. Huku nikiwa natafuta njia ya kutoroka nilisikia kitu kikinisukuma kwa kishindo kikali sana. Ghafla nilianguka chini na hata nilipoamka mazingira niliyoyaona yalikuwa tofauti kabisa.Mama Bilionea sikumuona tena ila kulikuwa na watu wengi sana katika hilo eneo. .......JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA..........15.....

Maoni 7 :

Bila jina alisema ...

Mmmh! Jamani so sad! Adela napenda simulizi zako sana. Keep it up my dear.

Bila jina alisema ...

nataman kila siku uwe unaiweka jmn uwiiii inanoga kila cku ya mungu.

ADELA KAVISHE alisema ...

asanteni sana wadau wangu mambo ndiyo kwanza yanazidi kunoga tuendelee kuwa pamoja

Bila jina alisema ...

Yaani hiki kitabu ukikitoa tu naomba unijuze kwakweli simulizi zako zinaelimisha sana

emuthree alisema ...

Kazi nzuri mpendwa, una kipaji kweli kweli, ....hongea na ubarikiwe sana. Tupo pamoja.

Bila jina alisema ...

Adela dear simulizi yako ni nzuri natamani iwe kwa siku mara mbili. Fans wako tunakupenda

ADELA KAVISHE alisema ...

Asanteni sana wadau wangu tuendelee kuwa pamoja

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom