Jumamosi, Juni 01, 2013

SIMULIZI ....KOSA LANGU NI LIPI..?....SURA YA .....3........




 ILIPOISHIA
Wakati huo Mama Joyce alikuwa  hajitambui walimuhamishia Hospitali ya Muhimbili Dar es salaam  kuendelea na matibabu.  Huko nyumbani mazishi yalifanyika, vilio na simanzi vilitawala, watoto walilia sana kwa uchungu na hata kupoteza fahamu huku wakiwa hawajui nini hatima ya Mama yao mzazi. Hapo ndipo maisha ya Joyce na mdogo wake  yalianza kubadilika. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA...3..

INAPOENDELEA
Baada ya kumuhifadhi Marehemu kwenye makazi yake ya milele.Watu walitawanyika pale nyumbani na kuwaacha akina Joyce wakiwa na simanzi na wakati huo waliishi kwa kumtegemea Mzee Ngonyani na mke wake. Maisha yaliendelea huku baadhi ya watu ambao walikuwa ni majirani na marafiki wa karibu,  walitoa michango yao kwa ajili ya matibabu ya Mama Joyce ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Yule rafiki yake na marehemu Mzee Ndesanjo alirudi Dar es salaam baada ya mazishi ya mke wake. Akiwa anatokea  Morogoro alikuwa hajui hili wala lile, na  nini kimempata rafiki yake kipenzi. Kwani hata marafiki zake walimficha kwasababu naye pia alikuwa katika matatizo ya kufiwa na mke wake. Aliporudi Dar es salaam alienda  nyumbani kwa marehemu ili kumjulia hali, alipofika alimkuta Mama Ngonyani akiwa pamoja na Joyce wakiwa wanajiandaa kwenda Hospitali kumuona mgonjwa.

 Joyce alikuwa akimfahamu rafiki wa Baba yake ambaye alikuwa akifahamika kwa jina la Mzee Simba. Alipomuona akaanza kumfuata huku akilia kwa uchungu “Baba mdogo Baba mdogo, ulikuwa wapi Baba yangu amefariki na Mama anaumwa sana” Mzee Simba alimuangalia Joyce  kisha akasema  kwa mshtuko  "Eti nini! Mzee Ndesanjo amefariki haiwezekani jamani nini kilitokea, siamini mimi haya maneno” alizungumza huku akiwa amemshika mkono Joyce aliyekuwa analia kwa uchungu.

 Mama Ngonyani akamsimulia kila kitu kuhusu ajali waliyoipata marehemu Mzee Ndesanjo na mkewe wakati wakielekea msibani Morogoro, Mzee Simba  aliinama kwa uchungu na machozi yalimbubujika katika paji la uso wake. Alisikitika sana kumpoteza rafiki yake, "Siamini kilichotokea sasa kwanini walinificha jambo hili jamani  eeh Mungu ilaze roho ya marehemu mahali pema peponi".  Alisema Mzee Simba.Baadaye waliondoka pamoja hadi hospitalini kwenda kumjulia hali  Mama Joyce.



Walipofika walimkuta amepata fahamu  lakini alikuwa haongei chochote muda wote  alikuwa kimya na alimshangaa kila aliyekuwa anamuona Joyce aliyekuwa karibu na Mama yake alimuita “Mama, Mama mimi mwanao Joyce ongea basi Mama hata kidogo” alimuita bila mafanikio Mama yake alibaki akimshangaa bila kusema chochote, hali ile iliwatatiza sana Mzee Simba na Mama Ngonyani iliwabidi waende  haraka kumuona Daktari ili waweze kufahamu  Mama Joyce ana matatizo gani.


 Daktari akawaeleza kuwa "Mgonjwa amepoteza kumbukumbu zote kwani katika hali aliyonayo hawezi kumkumbuka hata mtoto wake, na pia kuna uwezekano hata kama akirudi katika hali yake ya kawaida  basi atakuwa hana akili vizuri." Mama Ngonyani kusikia hivyo alishtuka na kusema “Mungu wangu sasa itakuwaje ndiyo tumekwisha mpoteza Mama Joyce, ina maana Daktari hakuna njia yoyote ya kumrudisha katika hali yake ya kawaida, tusaidie jamani”. Aliongea mama Ngonyani huku machozi yakiwa yanambubujika Daktari alimjibu akisema “Uwezekano hakuna mama, kilichobaki ni Kumuomba Mungu amsaidie pia tunaweza kumruhusu kesho ili muweze kumuangalia kwa ukaribu  akiwa nyumbani”.

 Walibaki wanahuzunika na kutafakari, Joyce alilia sana huku akiwaza nini hatima ya Mama yake. Baadaye ilibidi waondoke na kesho yake walirudi kwaajili ya kumchukua Mama Joyce ambaye alikuwa haelewi chochote. Maisha yalianza kubadilika kwa upande wa Joyce aliyekuwa na Malengo ya kusoma na baadaye kuja kuwa Mwanasheria. Hali ya maisha  ilizidi kuwa ngumu. Kwani Mama Joyce alikuwa akihitaji huduma wakati wote ilifikia kipindi familia ya Mzee Ngonyani ikaanza kuwatenga na hata waliokuwa  marafiki waliwaacha wakitaabika wenyewe. "Mwanzoni kabla Baba hajafariki majirani walikuwa wanatupenda lakini leo hii tunabaki tukitaabika peke yetu, tizama Mama yangu ni mgonjwa sana" Alikuwa akiwaza Joyce.

 Kutokana na hali kuwa mbaya  Joyce aliamua  kuacha masomo akiwa darasa la sita ili aweze kumsaidia mama yake pale nyumbani. Mzee Ngonyani na Mkewe waliamua kuhama katika ile nyumba.  Na tokea walipohama hawakuwahi kurudi hata siku moja kwenda kumjulia  hali  Mama Joyce. Maisha yalizidi  kuwa magumu, Joyce na mdogo wake ilibidi wakati mwingine waende mitaani na kuomba msaada angalau wapate pesa ya kununua chakula pale nyumbani.


Siku moja Mama Joyce aliamka asubuhi kichwa kilikuwa kinamuuma sana hivyo alitakiwa apelekwe hospitalini.  Joyce alikuwa hana chochote kwani alikuwa akitegemea biashara ya kuuza maandazi na pesa ilikuwa ni ndogo alihangaika sana bila kupata msaada wowote. Hatimaye kutokana na hali ya maisha na Joyce bado alikuwa ni msichana mdogo alishindwa namna ya kumsaidia Mama yake. Masikini  Mama Joyce alifariki Dunia kutokana na kuumwa sana bila kupata matibabu. 

Aliwaacha  Joyce na James ambao sasa walikuwa ni yatima. Maisha yalikuwa magumu  hawakujua nini cha kufanya kwani hata nyumba waliyokuwa wakiishi walifukuzwa kutokana na kushindwa kulipa kodi. Baada ya kufukuzwa walijikuta  wakirandaranda mitaani kutafuta kipato."Dada njaa inaniuma" James alikuwa akimwambia Dada yake aliyekuwa amejiinamia huku akiwaza siku hiyo walikuwa hawajapata pesa kabisa kwani kila walipokuwa wanaomba hakuna aliyewapa pesa  Joyce alimtizama mdogo wake na kusema "Usijali James nitakunulia chakula, ngoja niende nikaombe kwenye magari yanayopita barabara ya upande wa pili".

 Alinyanyuka huku akiwa ameweka mikono yake kichwani alijaribu kumuomba kaka mmoja "Samahani kaka naomba unisaidie hela nikamnunulie mdogo wangu chakula" Yule kaka alimtizama Joyce kuanzia chini hadi juu na kusema "Unawazimu wewe msichana, mimi nikusaidie hela umeambiwa mimi benki halafu mabinti wa sikuhizi mnajifanya ombaomba kumbe makahaba tu wa mitaani kwenda zako." Yule kaka alimtukana Joyce ambaye alinyamaza kimya na kuondoka taratibu aliendelea kuomba hatimaye alifanikiwa kupata shilingi elfu moja na mia tano ambapo alienda moja kwa moja kumnunulia chakula mdogo wake. Maisha ya Joyce na James yamebadilika na sasa wamekuwa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu huku wakikutana na changamoto nyingi sana wakiwa mitaani. JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE SURA YA...4.....
 

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Duh maskin.ila mungu ni mwema hamtupi mja wake

Bila jina alisema ...

Ooh! Jamani nna imani maisha yatakuja kubadilika hapo badae inshallah.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom