Ijumaa, Agosti 23, 2013

SIMULIZI FUPI "BORA KUKAA KIMYA"


MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

Mara nyingi nilikuwa nikimshauri sana Sara, kuachana na mpenzi wake kutokana na mpenzi wake huyo kuwa na tabia mbaya. Ambapo wakati mwingine alikuwa akimpiga sana. Siku hiyo nilikuwa nyumbani nimepumzika ghafla nilisikia mlangoni kuna mtu anabisaha hodi kwa nguvu. "Suzi, Suzi, naomba ufungue mlango John ananiuwa" Ilikuwa ni sauti ya Sara nilinyanyuka haraka na kufungua mlango Sara alionekana kuumia  maeneo ya usoni nilishtuka sana kumuona katika hali ile "Hee! Umepatwa na nini Sara, mbona hivyo kulikoni?" Nilimuuuliza huku nikimkaribisha ndani.

 Aliingia na kuketi lakini bado alikuwa analia kwa uchungu huku akisema "Yaani mimi kweli John ni wakunifanyia hivi,  wakati nimemfumania na mwanamke mwingine? Halafu ananipiga" Nilisogea na kuketi karibu huku niki mliwaza "Pole sana Sara, lakini kwanini anakupiga, kwa kosa lipi ulilomfanyia, huyu mwanaume ana kichaa heee! na wewe rafiki yangu mwanaume kama huyo hakufai ni bora uachane naye kabisa. Embu tizama  umemfumania halafu anakupiga,  usiwe mjinga kiasi hicho Sara wanaume wapo wengi, kama yeye anakuona wa nini, basi ajue kuna wengine wanafikiria watakupata lini. Mwanaume gani mshamba huyo usipoangalia ipo siku atakuvunja mguu".

 Niliongea maneno mengi huku nikimtizama Sara aliyekuwa anaendelea kulia akasema "Inaniuma sana, kwa jinsi ninavyompenda John, lakini sasa siwezi kuendelea kuwa naye bora tuachane kabisa". Na mimi nilikuwa namshauri asikubali kuendelea kuwa na uhusiano na John kutokana na ukatili anaomfanyia.

Tuliendelea kuzungumza huku nikimliwaza Sara, ilifika majira ya saa mbili usiku nikiwa naandaa chakula,  huku Sara akiwa ameketi sebuleni mara mlango ulifunguliwa kwa nguvu, na aliyekuwa amekuja muda huo alikuwa ni John, nilisogea na kuongea kwa sauti ya jazba "Umefuata nini hapa kwangu, naomba utoke nje, mwanaume muuaji wewe.Toka nje John sitaki kukukona hapa kwangu" Sara alikuwa ameketi huku akiwa amejiinamia bila ya kuzungumza chochote.

John alinitizama na kusema "Nimekuja kumchukua mpenzi wangu" Alisema John kwa kujiamini, nilicheka kwa dharau na kusema " Unanichekesha kweli wewe, eti nimekuja kumchukua mpenzi wangu, kama unampenda kweli kwanini unamsaliti na tena kama haitoshi unampiga" John hakunijibu chochote alimsogeleaa Sara na kumshika mkono "Darling (mpenzi) nakuomba twende nyumbani tukazungumze, nakupenda sana Sara" 

Niliwatizama ilikuona Sara atasemaje lakini hakuongea chochote na baadaye aliinuka na kuondoka na John bila hata ya kula chakula nilichokuwa nimeandaa, nilibaki nashangaa na kuzungumza na nafsi yangu "Makubwa haya, inamaana huyu Sara na kuumizwa kote huko bado anaondoka na John ama kweli mapenzi ni kipofu".

Zilipita takribani kama wiki mbili tokea Sara aje nyumbani kwangu. Siku hiyo nilikuwa katika mizunguko yangu ya hapa na pale maeneo ya kariakoo. Nikawa nimeingia katika duka moja la nguo,  nilimkuta John mchumba wake na Sara nilimsalimia lakini hakuitikia alinyamaza kimya, na mimi sikumjali, mara ghafla katika chumba kidogo cha kujaribishia nguo alitoka mwanamke  huku akiwa anazungumza na John " Mpenzi nimependeza, asante sana asali wa moyo wangu hii nguo ni nzuri nimeipenda" Yule mwanamke alikuwa akijishebedua huku akimshikashika John mikononi. Wakati wote huo nilikuwa nashangaa nikiwa siamini nianachokiona, lakini ilinibidi nikae kimya.

 Bila ya aibu wala wasiwasi John alimnunulia nguo nyingi yule dada na waliondoka na mimi nilinunua nguo niliyoipenda na kuondoka.

Nikiwa nyumbani kwangu niliwaza  na kumuonea huruma sana Sara ambaye alikuwa anampenda John kwa moyo wake wote, Nilifikiria na kuamua ni bora nimweleze Sara kile nilichokiona "Yaani hawa wanaume sijui wako vipi jamani, Sara ni mwanamke mrembo sana kuliko hata yule mwanamke ambaye John alikuwa naye pale dukani, hili jambo siwezi kukaa nalo moyoni ngoja nimpigie simu rafiki yangu nimweleze". Basi nikachukua simu yangu na kumpigia Sara nikamsimulia kila kitu nilichokiona Sara alisikitika na kusema "Jamani kweli John ananifanyia hivi, mimi nimemkosea nini huyu mwanaume au kwasababu nampenda, asante sana Suzi kwa kunipa taarifa huyu mwanaume ni bora niachane naye" Na mimi kwa msisitizo nikamshauri "Ni bora kabisa uachane naye, mbona wanaume wapo wengi huyo wanini mwanaume ambaye kila mwanamke atakayepita mbele yake anamtamani, rafiki yangu huyo mwanaume hakupendi" Tuliendelea kuongea na baadaye kila mtu aliendelea na kazi zake.

Baada ya miezi miwili tokea nizungumze na Sara sikuhiyo alikuja rafiki yangu anaitwa Maria  nilifurahi sana kwani tulikuwa hatujaonana muda mrefu. Maria alikuja na kuniletea kadi ya mchango wa harusi "Rafiki nimepita hapa kwako mara moja kukuletea kadi ya mchango wa harusi ya Sara na John wameamua kufunga pingu za maisha" Nilishtuka na kusema "Eti unasema Sara na John kwani si walikuwa wameachana?" Niliuliza kwa umakini "Mmmh wewe Suzi  acha hizo, ila mimi nimepata fununu kuwa wewe ndiyo ulikuwa unawachonganisha,  na tena ulikuwa unamtaka John kimapenzi ndiyo maana ulikuwa unataka watengane." Alisema Maria huku akinitizama, mimi nilikuwa nimepigwa na butwaa na kusema "Jamani mimi, nilikuwa nawachonganisha? Nani anazusha maneno hayo ya uongo, hata siku moja sijawahi kuwaza kumtaka kimapenzi huyo John, ama kweli binadamu wabaya, leo hii Sara ananiona mimi nilikuwa namchonganisha?" Nilibaki nashangaa na Maria  aliondoka na kuniacha peke yangu. Siku hiyo nilijisikia vibaya sana lakini pia nikawa nimejifunza jambo. Tokea siku hiyo nilikuwa sipendi kabisa kutoa ushauri katika suala la mapenzi baina ya wawili wapendanao. Nimeamua BORA KUKAA KIMYA. Kwani unaweza kutoa ushauri ukiwa na lengo zuri lakini ukaonekana mbaya. NI BORA KUKAA KIMYA.

Maoni 7 :

Bila jina alisema ...

Mmh! Hili nalo neno.! Nimejifunza somo!

Bila jina alisema ...

Word

Bila jina alisema ...

Duuuuh we Adela kiboko napenda sana simulizi zako ubarikiw

Unknown alisema ...

Hii nimeipenda mno hata mie sishauri mtu mambo ya mapenzi

dj cany alisema ...

kweli..

ROOSEVELT BENARD alisema ...

Very true. Nobody advises lovers about their relationship. It is usually better to let them settle their issues alone unless you are a marriage chancellor.

ROOSEVELT BENARD alisema ...

Very true. You have to let lovers solve relationship issues by themselves to avoid blames and accusations. Ni bora kunyamaza.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom