Alhamisi, Septemba 26, 2013

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA, ENDELEA KUPATA UHONDO

 
 KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI-ADELA  DALLY KAVISHE 

ILIPOISHIA
“Sawa mimi nashukuru kama mmejipanga hivyo. Mungu akubariki sana
mimi sina kipingamizi tena alimradi mmependana na kufuata taratibu za
kufunga ndoa ili mpate baraka za Mungu. Pia ninaomba mkishaanza
maisha muwe mnakuja huku kutusalimia mara kwa mara.” Mama Julieth
alishauri huku akimkazia macho Julieth na baadaye John. “Hilo halina tatizo kabisa mama hapa ni nyumbani tutakuja bila shaka kwani nyumbani ni nyumbani, hata hivyo kwa sasa akishawaona wazazi wangu tu atarudi ili kukamilisha mambo ya ndoa kama ulivyoshauri.” Alijibu John.
INAPOENDELEA
Mikakati ya kuondoka ikaanza, mama Julieth akahamishwa kutoka
nyumba waliyokuwa wanakaa na kuhamia katika nyumba kubwa ambayo
ilikuwa na kila kitu ndani. Kisha alitafutwa msichana kwa ajili ya kazi za
ndani. Halafu nje ya nyumba alimfungulia duka dogo ambalo mama
Julieth alikuwa akiuza bidhaa ndogondogo kama sabuni, sukari, unga na
vinginevyo. Mwisho John alimnunulia mama Julieth simu kwa ajili ya
mawasiliano ili kukitokea tatizo lolote atoe taarifa mapema. Mama Julieth
alifurahi sana.

Siku ya kuondoka ilikaribia Julieth alionekana mwenye huzuni kwa ajili ya
kumwacha mama yake. Mama Julieth yeye alikuwa katika hali ya kawaida
akisisitiza kuwa Julieth akumbuke yote aliyomwambia.
Safari ya kwenda Mwanza ilianza hatimaye walifika salama na kwenda
moja kwa moja nyumbani kwa John, maeneo ya Igoma. Julieth alishangaa
sana kuona nyumba aliyokuwa akiishi John ilivyokuwa kubwa, nzuri na ya
kifahari iliyojaa vitu vya thamani.

“Mpenzi nyumba yako ni nzuri sana, yaani nyumba yote hii unakaa
mwenyewe?” Aliuliza Julieth.
“Hapa ni kwako mama, nilikuwa nakaa mwenyewe na vijana wa kazi lakini
sasa nina mke aitwaye Julieth naamini nyumba hii itakuwa nzuri zaidi hasa
ikiwa na watoto na mke mzuri kama wewe.” John alijibu kwa kiburi na
majivuno.


Julieth alitabasamu huku akizunguka huku na kule akishangaa uzuri wa
nyumba ile ya kifahari. John alipeleka mizigo chumbani na kumwelekeza
kila kitu kilichomo na matumizi yake.

John na Julieth waliishi maisha ya raha na furaha. John alimtembeza Julieth
sehemu mbalimbali ili kumwonyesha utofauti wa mazingira ya Mwanza
na Arusha. Katika kuishi kwake Arusha Julieth alikuwa hajawahi kufika
Mwanza, aliupenda sana mji wa Mwanza hususan samaki aina ya sato na
sangara wanaopatikana katika mji huo ambao huvuliwa katika Ziwa la
Viktoria. Kwa ujumla Julieth alifurahia sana maisha yake mapya.

Baada ya wiki moja kupita Julieth alitaka kuwafahamu wazazi wa John,
lengo kuu la safari yao ilikuwa kwanza kwenda kuwafahamu wakwe zake.
“Vipi mpenzi lini tutakwenda nikawafahamu wakwe?” Aliuliza Julieth.
“Usijali mpenzi wangu tutakwenda tu kwani una wasiwasi gani, si upo na
mimi kuna kazi tu zimenibana kwa sasa ila tutapanga mapema wiki ijayo.”
Alimjibu John.
“Sawa John hakuna tatizo nilikuwa nataka kujua ili nimjulishe mama
Arusha.” Alijibu Julieth.
Mazungumzo yaliendelea baadaye walichoka na kwenda kupumzika.
*****Baada ya mwezi mmoja****

Wazazi wa John walikuwa wakiishi Bukoba na siyo Mwanza kama John
alivyosema akiwa Arusha. Kila mara Julieth alipomwambia suala la kwenda
kuwafahamu wazazi wa John aliambiwa kuwa watakwenda asiwe na
wasiwasi. Baadaye kutokana na raha alizokuwa anazipata Julieth, alijisahau
kabisa kama hajafunga ndoa na John. Mama yake Julieth alipokuwa
akimpigia simu na kumuuliza vipi kuhusu ndoa alimjibu hakuna tatizo
mipango inaendelea vizuri. Kumbe ilikuwa ni uongo wao walikuwa
wakijirusha na kusahau mambo ya ndoa na taratibu nyingine za kimila.
********Baada ya miezi mitano**************

Baada ya mapenzi na raha kushamiri, Julieth alipata ujauzito ambao
hakugundua kama ana mimba. Aligundua baada ya kwenda hospitali
kupima afya yake kutokana na kutojisikia vizuri ikiwa ni pamoja na kusikia
kichefuchefu. Suala la mimba lilimfurahisha sana Julieth.
“Huu ndio wakati mwafaka wa kufunga ndoa, najua John atafurahi sana
nikimzalia mtoto. Akija leo nitamwambia tufanye haraka tufunge ndoa.”
Aliwaza Julieth.

Ilipofika jioni aliandaa chakula cha usiku mapema huku akiwa anamsubiri
mpenzi wake arudi ampe taarifa kuhusu mimba aliyonayo. John alirudi na
kumkuta Julieth anafuraha sana.

“Kulikoni leo mpenzi mbona unaonekana una furaha sana kuna nini?”
Aliuliza John.
“Mpenzi leo nimetoka hospitali kupima nina ujauzito wako na sasa
nadhani utakuwa muda mwafaka tufanye haraka tufunge ndoa.” Aliongea
Julieth huku akitabasamu na kujichekeshachekesha.
”Ni vizuri Julieth lakini kwanza ukisha jifungua ndio tutafunga ndoa.”
Alijibu John akionyesha kutofurahishwa na taarifa ya Julieth kuhusu
ujauzito.

“Jamani John ni muda mrefu tumekuwa pamoja kwa nini isiwe mapema
kabla sijajifungua?.” Alisisitiza Julieth huku akimsogelea na kuweka
mikono yake mabegani kwa John.
“Sikiliza Julieth nikwambie; ndoa ina mipango mingi sana kwa hiyo wewe
nisikilize mimi.” Alisema John huku akiwa anainuka na kuelekea
chumbani.

John alikuwa kama mtu ambaye hajafurahia habari alizopewa na Julieth,
basi Julieth alinyamaza kimya lakini aliendelea kufikiri na kutafakari hali
aliyoonyesha John baada ya kupewa taarifa ya ujauzito.
“Mbona John amebadilika ghafla kuna nini? Ngoja nimwache
nitamwambia kesho vizuri.” Aliwaza Julieth huku akimfuata John
chumbani.

Kesho yake asubuhi kama kawaida waliamka mapema sana, Julieth
aliandaa chai. Walipokuwa wanakunywa Julieth alimwambia John kuwa
angependa kwenda Arusha kuwaona mama na wadogo zake kwani ilikuwa
ni muda mrefu.
“John naomba niende Arusha nikamsalimie mama na wadogo zangu.”
Aliomba Julieth.

“Huko Arusha tutakwenda wote siku nitakayopanga mimi, tena nikipata
muda.” Alijibu John akiwa amenuna.
“Vipi John mbona umebadilika tangu jana naona haupo sawa tukiwa
tunazungumza unaonekana una hasira kuna tatizo gani?” Julieth alihoji.
“Tatizo ni wewe unaongea sana sipati hata muda wa kupumua, tena na hii
chai kunywa mwenyewe.” Akaondoka na kumwacha Julieth akiwa
ameduwaa.
“Huyu mwanamume amekuwaje mbona hivi jamani simuelewi.” Aliwaza
Julieth.
Basi Julieth akaondoa vyombo mezani na kuendelea na shughuli zake.
Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele tabia ya John ilizidi kubadilika.
Alianza kuchelewa kurudi nyumbani na akirudi anakuwa amelewa sana,
tabia hizo zilimuumiza sana Julieth kwani raha alizokuwa anazipata zote
aliziona chungu na kujikuta akiwa mtu wa mawazo na kulia siku zote,
wakati mwingine alikuwa akimpiga sana na alikuwa hataki kumsikiliza kwa
chochote.

Ilifikia kipindi alimfukuza chumbani kwake akawa analala chumba cha
wageni. John hakujali kama Julieth ni mjamzito alimpiga bila ya huruma,
kutokana na matatizo kuwa mengi Julieth aliamua kumpigia simu rafiki
yake wa kike aliyejulikana kwa jina la mama Janeth ili kuomba ushauri
kutokana na matatizo aliyonayo.

Akiwa anampigia simu alikuwa chumbani bila kujua kwamba John alikuwa
amejificha pembezoni mwa mlango wa kuingia chumbani akisikiliza kila
kitu alichokuwa anamwambia rafiki yake. Akiwa anaendelea kuongea na
simu John aliingia kwa hasira sana na kumnyan’ganya simu kisha kumpiga
makofi huku akizungumza maneno makali.

“We shetani ulikuwa unazungumza na nani?” Aliuliza John kwa hasira.
“John leo unaniita shetani? Halafu unanipiga?” Aliuliza Julieth huku
machozi yakimlengalenga.
“Ndio nani ulikuwa unamwambia mimi nakunyanyasa? We masikini
nakuuliza mwendawazimu mkubwa na nitakuua leo na simu naichukua,
hutakiwi kuwa na simu umekalia umbea tu. Nisikusikie unamwambia mtu
yeyote mimi nakutesa mwehu wewe hata ukiwaambia watanifanya nini?”
Wakati John akiwa anasema maneno yote hayo Julieth alikuwa akilia kwa
uchungu wa maumivu.

“Unanionea John nimekukosea nini mimi.” Alilalamika Julieth huku
akishikashika na kupapasa tumbo lake.
“Nyamaza sitaki kusikia sauti yako nasikia kichefuhefu kabisa toka hapa.”
Alisema John huku Julieth akiondoka akiwa analia. Ama kweli usilolijua
ni sawa na usiku wa kiza. Julieth hakujua kwa nini John amebadilika vile
ghafla na kwamba nini kifanyike ili kumrudisha katika hali yake ya kawaida
ilikuwa ni kitu kisichowezekana ilibidi awe mvumilivu na kujipa
matumaini.

Baada ya siku kadhaa kupita hakukuwa na mabadiliko yoyote ila matatizo
yalizidi kila siku ilikuwa ni ugomvi. Miezi kadhaa ilipita bila Julieth kuwa
na mawasiliano na wazazi wake kwani alikuwa hana simu, hivyo ilikuwa
vigumu kujua hata wazazi wake walikuwa wanaendeleaje. Kwa kweli
maisha yalikuwa magumu sana. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa
miezi saba lakini John alikuwa hajali.

Siku moja John alimwambia Julieth kwamba siku zake za kuondoka
zinahesabika. Ilikuwa ni yapata kama saa mbili usiku wakati Julieth
akiandaa chakula cha jioni. John alifika na kumwita Julieth.
“We mwehu si ulikuwa unataka uende nyumbani kwenu sasa muda wako
umefika unaweza ukaondoka muda wowote nakupa wiki mbili tu.”
Aliongea John kwa maneno ya kutukana.

“Lakini si ulisema tutakwenda wote? Hebu niangalie na hali hii kweli ndiyo
niende nyumbani mwenyewe. Afadhali nisubiri hadi nijifungue ndiyo
niende nyumbani. “Wewe una kichaa nini hivi hapa ni kwako? Tena
sikiliza kwa makini nataka uondoke uende popote unapopajua hata ukifa
shauri yako. Kwanza hata hiyo mimba si yangu. Kwa hadhi yangu siwezi
kuwa na mke kama wewe. Kwa taarifa yako mimi nina mke na mtoto na
siku si nyingi anarudi sitaki aje akutane na kinyago kama wewe humu
ndani.” John alitukana na kuongea kwa kebehi na dharau.

Akiwa amejiinamia Julieth alisikiliza yale maneno na kuhisi kama ni ndoto.
Kabla hajazungumza lolote John aliondoka na kumwacha akiwa na
mawazo sana na kushindwa kuelewa mwenziwe ana matatizo gani.
Baada ya wiki moja kupita tokea John alalame na kutukana wakati Julieth
akiwa amekaa sebuleni mara John aliingia na kupita pale sebuleni kama
hajamwona kisha aliingia ndani na kurudi na mabegi ya nguo na kumtupia
huku akimfukuza Julieth aondoke na kwenda kwao.

“Kuanzia muda huu ninavyoongea sitaki kukuona katika nyumba yangu tena. Kama kuna kitu nimesahau kukitoa ukakitoe sasa hivi sitaki kukuona
hapa mke wangu karibu atarudi.” Aliongea John kama mtu aliyepagawa.
“Jamani mimi nitakwenda wapi na hii mimba?  John uliniambia
unanipenda kweli leo unanifanyia hivi? Nakuomba kama nimekukosea
unisamehe unajua hali halisi ya maisha yangu nitafanyaje mimi kama
unanifukuza? Je, maisha yangu yatakuwaje? Aliuliza Julieth kwa uchungu
huku machozi yakimtoka kama mtoto mdogo.

“Mbona siku uliponitoa kwetu ulionyesha kunipenda sana, halafu
ukamwambia na mama….” Kabla Julieth hajamaliza kuongea machozi
yalimtiririka mashavuni kama vile kamwagiwa maji kichwani.
“Mimi nikupende wewe! Mjinga sana, nimekwambia ondoka kabla
sijakuua.John ”Alimfukuza Julieth na kutupa mabegi yake nje. Ilikuwa jioni
yapata saa kumi na moja, Julieth alilia sana huku akiwa hajui atakwenda
wapi. Aliondoka na kwenda nyumba ya jirani kidogo ambapo alikuwa
anakaa rafiki yake aliyeitwa mama Janeth na kumsimulia mkasa mzima.

“Pole sana rafiki yangu wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo, mimi
nitakusaidia ulale leo, halafu kesho uende tu nyumbani kwenu Arusha.
Nitakupa hela kidogo.” Mama Janeth alimwonea huruma na kumfariji.
“Asante sana mama Janeth kwani hapa nilipo sijui ningefanyaje.”
Alishukuru sana Julieth na kwenda kulala baada ya kuonyeshwa sehemu
ya kupumzika.. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE  MUENDELEZO WA SIMULIZI HII.

Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

Nzur sana.

Bila jina alisema ...

Kwanini umeamua kuirudia hii stori mamii wakati ulishaiweka hadi sura ya 11? unatupoteza jamani bora ungeendelea pale ilipoishia.

Bila jina alisema ...

Yaani wanaume ni mashetani

ADELA KAVISHE alisema ...

MDAU KUNA AMBAO WALIKUWA HAWAJAISOMA ILA NITAIWEKA HADI MWISHO WAKE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom