Jumatano, Machi 19, 2014

Alichokisema muigizaji Wastara "Magazeti yanasabisha mimi nikose mume"


STAA wa sinema za Kibongo, Wastara Juma ametoboa kuwa, kuna wanaume kibao walimchumbia kwa nyakati tofauti, lakini wakabadilisha uamuzi huo na hivyo kumfanya aendelee kubaki mpweke.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam, Wastara alisema, wanaume hao wanafikia uamuzi huo kutokana na magazeti na mitandao mbalimbali kuripoti mara kwa mara kuhusu uhusiano wake na Mtangazaji wa Channel Ten, Bond Binslum, habari ambazo anazikanusha.

IKOJE?
Wastara alisema, tangu kifo cha mume wake, Juma Kilowoko ‘Sajuki’, magazeti yamekuwa yakimwandama kwa habari za skendo badala ya kuangalia mambo ya msingi na hivyo kumkosesha mume mwema.
“Maisha yangu ni kama yanaendeshwa na magazeti, kila siku utakuta habari zangu kwenye magazeti tena siyo nzuri, sasa zinanisababishia matatizo.


Angalia sasa, kuna watu walijitokeza na kuonyesha nia ya kunioa, lakini wakija kuona habari kwenye magazeti wanabadilisha mawazo.
“Kwa kweli nawashukuru sana nyie (Global) huwa hamuandiki habari bila kuniuliza kwenye simu, lakini wapo wengine sijui wanatoa wapi maneno, wanayaweka kwenye gazeti hivyo hivyo. Yaani tangu nimepata misukosuko, sijatulia kabisa, kila siku ni mikasa baada ya visa,” alisema. 

KUHUSU BOND
“Watu wanaandika mimi nina uhusiano na Bond, tangu lini? Hata wakiniuliza nikikataa, bado wanaendelea kuandika kuwa Bond ni mpenzi wangu, si jambo la kweli. Sikia... kuna mwanaume mstaarabu sana, tena Muislam safi, alijitokeza nyumbani kistaarabu, akaniposa.
“Mambo yakaenda vizuri, lakini baadaye kidogo akaja kusoma kwenye magazeti eti mimi na Bond tunapika na kupakua, akabadilisha mawazo. Ilikuwa kazi ngumu kumuelewesha kuwa siyo kweli, hakuniamini kabisa.”

MAHARI YARUDISHWA
“Mwingine tulifikia mahali pazuri kabisa, hadi mahari alishatoa, baadaye akaona kwenye mitandao kuwa nimeonekana kwenye magazeti nikiwa na Bond, akahairisha kila kitu na akataka arudishiwe mahari yake - akapewa.

Hebu angalia ni mambo gani hayo?
“Huko ni kuharibiana. Naishi maisha ya huzuni kila siku, kwanini wasiandike mambo ya msingi ya kunisaidia badala ya kuzusha mambo kama wanavyofanya sasa?”

NDOA IPO LAKINI...
“Mimi ni mwanamke, nimekamilika. Siwezi kuishi peke yangu siku zote, kwa hiyo kuwa na mwanaume siyo kosa, ila sasa muda haujafika. Nikiwa na mtu wangu, kwa nini nisiwe mkweli? Habari za mimi kuwa na Bond zinazushwa tu, watu waachane na hayo mambo wafanye mengine ya muhimu.

“Kwa sasa niachwe nipumzike, najua ipo siku atatokea mwanaume wa ukweli, tutakamilisha taratibu zote, atanioa. Ikifika hatua hiyo, sitakuwa na sababu ya kuficha. Watu wanipe muda kwanza.”

MSIKIE HUYU
Risasi Mchanganyiko liliwasiliana na mmoja wa mashosti wa karibu na Wastara na kuzungumza naye kuhusiana na malalamiko ya Wastara ambapo alisema inawezekana shoga yake akawa na hoja lakini bado ishu hiyo ipo mikononi mwake.

Kwa sharti la kutotajwa gazetini, shosti huyo alisema: “Lakini rafiki yangu naye kayataka mwenyewe. Kama hatoki na huyo Bond, sasa mapicha aliyokuwa akiyaweka kwenye mitandao ya kijamii akiwa naye karibu ya nini? Maana chanzo cha yote ni hizo picha.

“Namshauri tu atulie, afanye mambo yake kimyakimya, kuweka picha kwenye mitandao ni hatari... yeye mwenyewe anaamua kuyaendesha maisha yake kupitia vyombo vya habari.
GPL

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom