Jumanne, Mei 13, 2014

HABARI ZILIZOCHUKUA UZITO MKUBWA KUTOKA KATIKA MAGAZETI YA LEO

GAZETI MWANANCHI

Lissu: Walipotelea wapi waasisi sita wa Muungano

Dodoma. Serikali imetakiwa kutoa maelezo bungeni, kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wanaodaiwa kuzikwa katika handaki moja Zanzibar.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza waasisi hao walifanya makosa gani.


Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama, Zanzibar.
Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu cha ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru’ kilichoandikwa na Harith Ghassany alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika kaburi moja.
************************************************************************************************Dar es Salaam. Wakati Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukitarajiwa kuanza ziara ya siku 10 katika mikoa ya Tanzania Bara kesho, viongozi wa umoja huo wamemvaa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa kauli yake kuwa Katiba haina umuhimu.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kwamba ameshangazwa na kauli ya Kinana kwa kuifananisha Tanzania na Uingereza ambayo haina Katiba.
“Kauli hii imenipa matatizo, naanza kutilia shaka kisomo cha hawa wenzetu...“Hawana Katiba ya kuandika lakini wana sheria zao ambazo wanaziheshimu, ndiyo maana huwezi kuwahoji kuhusu Malkia Elizabeth wakakuelewa.Mikutano ya Ukawa
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema awamu ya kwanza ya ziara hiyo itaanza kesho hadi Mei 26, mwaka huu.
Alisema ili kufanikisha ziara hiyo, Ukawa imejigawa katika timu tatu ambazo zitakuwa zinafanya mikutano na maandamano ya amani.
Kundi la kwanza litaongozwa na Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Mosena Nyambabe, la pili litakuwa na Dk Slaa na la tatu litakuwa chini ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba.
*************************************************************************************************Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitupa Katiba ya Yanga iliyopelekwa kwa shirikisho hilo kwa ajili ya kupitiwa kabla ya kusajiliwa na kutoa nafasi kwa klabu hiyo kufanya uchaguzi mkuu Juni.
Baada ya kuipokea katiba hiyo ya Yanga, TFF iligundua kwamba klabu hiyo ilipeleka Katiba ya mwaka 2010, ambayo haina marekebisho ya vipengele muhimu walivyokuwa wameagizwa kuviingiza katika katiba yao.
Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama wa TFF, Evodius Mtawala aliiambia  Mwananchi kuwa hadi sasa, licha ya Yanga kutangaza kuitisha mkutano wa wanachama wake Juni Mosi kwa ajili ya marekebisho ya katiba, bado uongozi wa klabu hiyo haujaijulisha rasmi (TFF) kwa maandishi.
***************************************************************************************************
GAZETI NIPASHE

Walimu waikimbia shule kwa imani za kishirikina

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nfunzi iliyoko katika kijiji cha Nyakasaa kisiwani Kome Wilaya ya Sengerema mkoani  Mwanza, Jaqueline Massawe, pamoja na walimu kadhaa, wameikimbia shule hiyo kutokana na imani za kishikirina.


Kutokana na imani hiyo, Idara ya Elimu wilayani Sengerema, imepanga kuwapeleka walimu ambao ni wazawa wa kisiwa hicho kuchukua nafasi ya walimu waliondoka kama njia ya kutatua tatizo hilo katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 500.



Walimu hao wanaofikia saba, walianza kuikimbia shule hiyo tangu Novemba, mwaka jana  baada ya baadhi ya walimu wenzao kudai kunyolewa nywele usiku zikiwamo sehemu zao  za siri.



Hali kadhalika, wengine walidai kucharazwa viboko wakiwa wamelala usiku, hali iliyoibua hofu miongoni mwao.



Shule hiyo inayomilikiwa na serikali, ina majengo bora ukilinganisha na shule zote 183 za msingi za wilayani Sengerema.

*********************************************************************************************************

Ulemavu wa mikono wamfanya atumie mguu kuandika shuleni

Mwanafunzi Julius Charles (12), anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko wilayani Singida, analazimika kutumia mguu wake wa kulia kuandika masomo yake kutokana na ulemavu wa kutokuwa na mikono.



Akizungumza na NIPASHE shuleni hapo mwishoni mwa wiki, mwanafunzi huyo alisema kuwa walimu wake au wanafunzi wenzake, humkamatisha kalamu kwenye mguu na kuanza kuandika kwa ufasaha sawa na wanafunzi wengine wenye mikono.



Katika mahojiano maalum yaliyofanyika darasani kwake na NIPASHE, Julius, mkazi wa kijiji cha Mgungari Wilaya ya Bunda mkoani Mara, alisema alianza darasa la kwanza mwaka 2006 akiwa hajui kuandika wala kusoma.



Hata hivyo, alisema kutokana na kupenda kusoma, alilazimika kujiunga na shule hiyo baada ya kupata taarifa zake kutoka kwa mama yake aliyempeleka shuleni hapo. Aidha, alisema katika matokeo ya mtihani darasani, alishika nafasi ya tatu darasani kati ya wanafunzi 62 wa darasa lake.
****************************************************************************************************************

Ugonjwa wa dengue wazidi kutikisa nchi

Ugonjwa  wa homa ya dengue umeendelea kuwa tishio nchini kutokana na idadi ya watu wanaoambukizwa kuongezeka.


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana ilitoa tamko ikisema kwamba idadi ya wagonjwa wa dengue imefikia watu 400 na vifo vya watu watatu na waliolazwa ni 13.



Aidha, wizara hiyo imesema Mei 9, mwaka huu idadi ya wagonjwa waliogundulika katika Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa ni 60 kati ya hao, Manispaa ya Kinondoni 42, Temeke 14 na Ilala wanne.



Tamko hilo lilitolewa jana na jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Charles Pallangyo, kwa waandishi wa habari.



“Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibitishwa kuwa na ungonjwa huu ni 400 na vifo vitatu, hivyo wizara inapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya mwenendo wa ugonjwa huu nchini,” alisema.



Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na kuwa dalili hizo huanza kujitokeza kati ya siku tatu na 14 tangu mtu alipo alipoambukizwa kirusi cha ugonjwa huo.



Aidha, aliwataka wananchi kusafisha mazingira yao ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vifuu  vya nazi, makopo ya maua na magurudumu ya magari. 

*************************************************************************************************************

Wambura achukua fomu Urais Simba

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) kwa  sasa TFF, Michael Wambura, jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Urais katika uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika Juni 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.


Wambura na Zacharia Hanspoppe ni baadhi ya wagombea walienguliwa katika mchakato wa uchaguzi wa 2010 kutokana na kutokidhi sifa na Wambura pia aliondolewa kwenye mchakato wa kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana.



Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu jana, Wambura, alisema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kuondoa umiliki wa wanachama wachache na vile vile anataka kuona Simba inakuwa klabu inayojitegemea.



Wambura alisema anataka kuona Simba inakuwa na vitega uchumi vyake vya kuiendesha klabu huku pia ikiwa na wachezaji wanaomilikiwa na klabu na si watu binafsi.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom