Jumatano, Mei 07, 2014

INASIKITISHA SANA MASIKINI ROZI "Wako wapi watoto wangu,, familia yangu"

Ama kweli ajali haichagui maskini wala tajiri.  Inasikitisha kwani ni mwanamke asiye na uwezo anayeishi kufanya biashara ya kuuza ndizi anazotembeza barabarani.  Hata hivyo, hivi sasa maisha yake yamezidi kuwa magumu kwa kuwa hajui familia yake ilipo.
Rose  Mathias (25) mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam aligongwa na gari na kuvunjika mguu wakati akivuka kuwafuata wateja upande wa pili wa barabara.

Rose, ambaye kwa sasa amelazwa Chumba Namba 2, Wodi ya Mwaisela ya Hospitali ya Taifa Muhimbili,  anasema alipatwa na masaibu hayo wakati akiuza ndizi ambazo humsaidia kupata fedha kwa ajili ya kulipa kodi ya nyumba na kuihudumia familia yake.
 “Mungu mkubwa ameninusuru na ajali mbaya. Sikudhani leo hii  ningeweza kuongea na wewe. Kwa kweli nilikosa matumaini ya kuendelea kuishi hapa duniani,” alisema.
“Ninachokumbuka ni kuwa siku hiyo niliamka salama na kuwaacha wanangu nyumbani kama kawaida. Kwao ni kawaida kwa kuwa ndio aina ya maisha yetu, lakini mpaka leo sijawaona wanangu wala hakuna ndugu aliyefika kunijulia hali,” anasema.
“Siku hiyo nilishtukia nikiwa chini baada ya kugongwa na gari. Sikujua kilichoendelea... nilikuja kupata fahamu nikiwa hapa hospitalini huku mguu wangu ukiwa umevunjika. Nimeumia pia sehemu mbalimbali za mwili. Kwa sasa sijiwezi. Nimepewa mtu wa kunisaidia na kunilisha chakula nikiwa kitandani,” anasema.
Anasema aliposhtuka alijikuta akiwa wodini tayari, lakini kinachomuumiza ni kutojua taarifa za familia yake na pia ndugu zake kutofika kumjulia hali.
“Sijajua wanangu wanavyoishi na wamekuwa wakila wapi. Suala la wanangu linaniumiza sana nikikumbuka nilivyohangaika nao kwa kipindi kirefu bila msaada wowote kutoka kwa mtu. Wakati fulani tumekua tukishinda nao njaa pale ndizi zinapokosa wateja. Najua kwa sasa hawanioni wamebakia kuomba chakula mitaani,” anasema.
“Nikikumbuka nilivyoangaika nao kutoka nyumbani kwetu Arusha baada ya baba yao kutoweka, nilifuatana nao kuja hapa Dar es Salaam kutafuta kazi baada ya dada yangu kuniita nije nifanye biashara huku. Lakini cha kusikitisha ni kwamba nilipomwambia nipo Kituo cha Mabasi Ubungo na watoto, alinikatia simu,” anasema.
“Niliamini alifanya hivyo kwasababu  nilikuwa na wanangu. Mama mmoja alinionea huruma na alinichukua baada ya kuona sina pa kwenda na nina watoto wadogo. Aliniomba nimsaidie kazi pale nyumbani kwake na kunilipa fedha. Nilikubali kwani hata ingekuwa namsaidia bila malipo, ningekubali kutokana na hali niliyokua nayo.”
Anasema suala la kuongozana na watoto lilikuwa kikwazo katika kazi yake kwani baada ya muda alitakiwa aondoke.
“Nilikaa kwa muda wa mwezi moja hali ikabadilika, nikawa naambiwa maneno ya kunifanya nitamani kuondoka. Walidiriki kunieleza kuwa watoto wangu wasumbufu na wanakula sana kuliko wa kwake. Nilitakiwa nitafute pa kwenda. Nilijifungia chumbani na kulia kwa muda mrefu kama mtoto kwa kuwa nilikuwa  sina  uwezo  wa  kujitegemea,” anasema.
“Nilitafuta kazi za ndani bila mafanikio. Niliomba  msaada kwa watu, lakini sikufanikiwa  ila  nilibahatisha kumpata msamaria  mwema  moja  alinisaidia  chumba kimoja  ili  niweze  kuishi  na  watoto wangu  wawili niliofuatana nao na alinipa  mtaji ili nianzishe biashara nami nikaamua  kutembeza ndizi mitaani,” anasema.
“Wakati fulani biashara inakuwa mbaya na  kushindwa jinsi  ya  kufanya  ila  kesho yake  ninaamka  asubuhi   na  kuendelea bila  kukata tamaa. Nikapangisha  chumba changu na nilikuwa  ninalipa Sh25,000 kwa  mwezi. Kodi iliisha  na  mwenye  nyumba alitaka  nimlipe  na kama sina nitafute  namna yaka  kufanya.
“Niliona nijitahidi kwa  biashara  hii ya kuuza ndizi na tayari nilishapata Sh40,000 na nilikuwa nikitafuta nyingine kwa  biashara  hii ninayoifanya ili nimlipe, lakini  kwa  bahati mbaya nikapatwa  na  janga  hili. Kwa sasa hata nikipona na kurudi nyumbani Mbagala, sitaendelea  kuishi hapa  jijini  bali  nawaombeni  Watanzania   mnisaidie fedha ili niweze kusafiri na familia yangu kurudi Arusha,” anasema Rose.
Anaongeza kwa kutoa shukrani kwa wauguzi na madaktari akisema:
“Ninawashukuru  madaktari  na  wauguzi  katika hospitali  hii kwa  tiba  wanazonipa. Hivi  sasa  naongea ingawa  siyo  sana, lakini  kumbukumbu   zinaanza  kurudi  kwani waliniambia kwamba nimepata  unafuu  kwa  kiasi kikubwa  tofauti  na  nilivyoletwa kwa kuwa nilikuwa  siongei wala sijitambui. CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom