Jumatano, Mei 28, 2014

Mtoto aliyeishi kwenye boksi,sasa anapatiwa matibabu zaidi Muhimbili

Mtoto aliyekuwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka mitatu mfululizo Morogoro,Nasra Rashid (4),akiwa kwenye Wodi B ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH)alikohamishiwa kwa matibabu zaidi. Picha na Beatrice Moses. 
Mtoto aliyekuwa amefichwa kwenye boksi mkoani Morogoro, Nasra Mvungi ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa uchunguzi zaidi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Morogoro, Dk Godfrey Mtei alisema Nasra alipelekwa Muhimbili juzi usiku baada ya hali yake kutoridhisha.
Alisema afya ya Nasra ilibadilika ghafla juzi asubuhi na kushindwa kupumua vizuri, jambo lililowalazimu madaktari kumpeleka Muhimbili kwa gari maalumu la wagonjwa akiwa chini ya uangalizi maalumu wa wauguzi na ofisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii mkoani Morogoro atakayekuwa anamhudumia hospitalini hapo. Dk Mtei alisema kama mtoto huyo atahitaji matibabu zaidi nje ya nchi, atapelekwa ili kuhakikisha kuwa anarejea katika hali ya kawaida.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu alisema ofisi yake itaendelea kufuatilia afya yake kwa karibu na ndiyo sababu mtoto huyo atahudumiwa na mama mlezi kutoka kituo cha kulelea wazee wasiojiweza ambaye alijitolea kumhudumia tangu alipofikishwa hospitalini hapo.
Akizungumza jana kwenye Hospitali ya Muhimbili, Ofisa Uhusiano wa MNH, Doris Ishenda alisema mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo juzi saa saba usiku... “Tayari ameanza kupatiwa huduma za awali ikiwa ni pamoja na kupimwa uzito, pia amechukuliwa damu na ninafikiri majibu ya baadhi ya vipimo hadi leo (jana) mchana yatakuwa tayari.”
Mkuu wa Jengo la Watoto, alimolazwa Nasra, Anna Kilufi alisema hali ya mtoto huyo imeanza kuimarika akionekana kuwa na mabadiliko makubwa.
“Shida yake kubwa ambayo tunaiona ni chakula tunatarajia kumhamishia kwenye wodi ya watoto waliokosa lishe ili tuendelee kumhudumia kwa chakula bora ili apate afya inayostahili,” alisema Kilufi.
Mama mlezi wa Nasra, Josephine Joel alisema kwamba mtoto huyo amechangamka na anashukuru kwamba ameshamzoea na anafarijika kuwa naye.
“Naomba Mungu anisaidie niendelee kumpenda kama mwanangu wa kumzaa, nisije kumnyanyapaa, ameshanizoea anazungumza nami vizuri hata kucheza nami kwa namna fulani,” alisema.CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom