Jumamosi, Mei 24, 2014

Taarifa hii inasikitisha sana tunaelekea wapi jamani "Mganga aua mtoto kikatili na kumzika"

Mganga Mujingwa John akiwa na matunguli yake.picha ya kulia akionyesha jinsi alivyomkaba na kumnyonga mtoto mdogo pia kukata viungo vyake kisha kuchimba shimo chini ya kitanda chake.


Mtoto wa darasa la kwanza, Fausta Geofrey (8), ameuawa kikatili kwa kunyongwa na kukakatwa viungo na mganga wa kienyeji na  mwili wake kuzikwa ndani ya nyumba.

Kwa mujibu wa Afisa mtendaji wa kijiji cha Bisole kata Muhutwe wilayani Muleba, Khamis Hassan, baada ya mauaji hayo, muuaji alimkata mtoto huyo mikono yake miwili kabla ya kumzika.

Hassan alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 21, asubuhi katika kijiji hicho wakati mtoto huyo akiwa na wenzake wakielekea shuleni. Inadaiwa kuwa mtoto huyo aliitwa na kukamatwa na mganga huyo Mujingwa John (20).

Alisema kuwa baada ya taarifa za mtoto huyo kutoonekana kuzagaa, wanakijiji walikusanyana na kuanza msako ambapo walikamata kundi la vijana wanaohofiwa  kuhusika na tukio hilo.

Alisema baada ya kukamata watu hao waliwaweka sehemu moja na kuwaita wanafunzi waliokuwa na marehemu ambapo walimtambua mganga huyo kuwa ndiye aliyemwita na kumkamata mtoto huyo.

Mtendaji huyo alisema kuwa baada ya mganga huyo kutambuliwa, wananchi na polisi waliofika eneo hilo waliondoka naye hadi katika nyumba anamoishi na kumtaka awaonyeshe alipo mtoto huyo.

Alisema baada ya kumbana aliwaonyesha sehemu alikomzika ambapo walichukua jembe na kufukua maiti ya mtoto huyo iliyokuwa imezikwa ndani ya nyumba.



Alisema baada ya mganga huyo kumuua mtoto huyo, alimkata mikono yake miwili na kisha kuchimba shimo ndani ya nyumba na kumzika ambapo shimo alitandaza nyasi na juu akaweka kitanda.

Alisema kuwa alipohojiwa ili kujua nani kamtuma kutekeleza unyama huo, mganga huyo alisema kuwa aliota mizimu yake ikimtuma kumuua mtoto ili amkate viungo vyake kwa ajili ya kuchanganya na dawa.

Alisema kuwa mikono hiyo alitaka kuibanika kwenye moto ili aichanganye na dawa ambayo angewapatia watu wanaohitaji kupata utajiri.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera, George Mayunga, alisema kuwa mganga huyo alikamatwa na polisi kwa kushirikiana na wananchi ambapo alikutwa akibanika viungo alivyomkata mtoto huyo.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kwa kujiamini, mganga huyo alisema amefikia hatua hiyo kutokana na hali ngumu ya umaskini inayomkabili.

Alisema baada ya kumkamata mtoto huyo alimkaba shingo na kumvuta hadi katika nyumba alimokuwa akiishi, akamnyonga hadi kufa na baada ya kufa alimkata ngozi ya mgongoni, mkono wa kushoto anaodai una bahati, sehemu za siri na masikio.

“Nilikamata mtoto na kumuua maana niliona nikikamata mtu mzima atanizidi nguvu,” alisema mganga huyo.
Alisema alipohakikisha amemuua alichimba shimo chini ya kitanda chake akamzika na kutandaza nyasi juu yake ili isigundulike kama eneo hilo kuna shimo.

Mganga huyo alisema viungo hivyo ambavyo hadi polisi wanafika alikuwa bado akivikausha angevichanganya na dawa ambayo angewapatia wateja wake ili iwasaidie kufanikisha mambo yao ikiwamo kupata bahati na utajiri.

Alisema yeye kabila lake ni Msukuma na kuwa ni mara yake ya kwanza kufanya tukio kama hilo ambapo alihamia kutoka mkoani Mwanza eneo la Nyanguge, wilaya ya Magu na kuhamia wilayani Muleba miaka miwili iliyopita.

Alisema alirithi uganga huo kutoka kwa babu yake mzaa mama na kuwa alianza kuwa mganga akiwa na umri wa miaka minane na hajawahi kwenda shule.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom