Jumanne, Juni 10, 2014

MAZOEZI NI TIBA NZURI SANA.Watafiti wamefanya uchunguzi "Mazoezi hutibu Saratani"

Mazoezi yanaweza kusaidia kupona baada ya kuugua saratani ya matiti lakini ni wanawake wachache sana wanashiriki katika mazoezi, utafiti unasema.
Watafiti wa Marekani, katika ripoti waliyochapisha katika jarida linaloandika mambo ya saratani, wanasema kuwa inajulikana wazi kwamba kufanya mazoezi ya aina moja au nyingine kunasaidia lakini imegunduliwa kuwa wanawake hawapendi kufanya mambo yanayowachosha.
Ni thuluthi moja pekee ya wanawake inayofanya mazoezi kufikia kiwango kinachopendekezwa.
Makundi ya kuwasaidia wanaougua saratani ya matiti nchini Uingereza yanasema wanawake nchini humo wanahitaji kusaidia wanawake kufanya mazoezi zaidi baada ya kutibiwa maradhi hayo.
Utafiti huo uliofanywa Marekani uliwashirikisha wanawake 1,735 wenye umri kati ya miaka 20 na 74 waliokuwa na saratani ya matiti kati ya mwaka 2008 na 2011 katika Carolina Kaskazini.

Marekani na Uingereza zinapendekezwa kuwa watu wazima wanapaswa kufanya mazoezi ya kadiri ya dakika 150 kwa juma moja au mazoezi makali zaidi ya dakika 75 kila wiki.
Lakini utafiti huu uligundua kuwa ni wanawake 35 pekee waliougua saratani ndio wanaofuata maagizo haya ya kufanya mazoezi baada ya kutibiwa saratani ya matiti.
Nchini Uingereza wahamasishaji wa saratani ya matiti wanasema wanawake wanapaswa kufanya mazoezi mengi zaidi nchini humo.
Caroline Dalton, kutoka kundi la Breakthrough Breast Cancer, alisema: " Mazoezi ya maungo baada ya mtu kuugua saratani ya matoto yanaimarisha uwezekano wa aliyeugua saratani kupona kabisa na kuna ushahidi pia kuwa yanasaidia kuhakikisha kuwa saratani ya matiti haimrudii aliyeugua tena.
"Kuendelea na mazoezi pia kunasaidia mgonjwa kustahimili, wakati wa matibabu na baadaye, kwa kuimarisha afya yake kwa ujumla na kuisha maisha bora."
Aliongeza: "Ingawa utafiti huu ulifanyiwa Marekani badala ya Uingereza, matokeo yanapendekeza kuwa wanawake ambao wamegunduliwa kuwa na saratani ya matiti wanapaswa kusaidiwa ili waendelee kufanya mazoezi."
"Hakuna mwelekezo kamili wakati huu kutueleza kikamilifu kiwango cha mazoezi kinachohitajika baada ya kugunduliwa kuwa una saratani ya matiti, lakini Breakthrough Cancer inapendekeza kuwa unapaswa kulenga kufanya mazoezi kwa masaa matatu u nusu kwa wiki moja, baada ya kushauriana na matabibu wako kukuelezea kiwango kinachokufaa."
Baroness Delyth Morgan, Afisa Mtendaji katika Breast Cancer Campaign, alisema: "Utafiti huu unapaswa kuwakumbusha wote kuwa ni muhimu kwa wanawake walio na saratani ya matiti kuwa kufanya mazoezi kunachangia pakubwa kama wataishi au kufariki baada ya kugunduliwa kuwa una saratani.
"Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa hata nyongeza ndogo ya mazoezi yanayofanywa baada ya kugunduliwa kuwa mtu ana saratani yanaongeza nafasi kwa mwanamke anayeugua kunusurika.
"Hii ndio sababu ni muhimu kwa wakawake kupewa mpango kamili wa kufuata ulioandikwa chini ambao utasaidia ushauri nasaha kuhusu maisha yao juu ya aina ya chakula na mazoezi." CHANZO BBC.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom