Jumatatu, Julai 21, 2014

KUELEKEA UCHAGUZI 2015 "Walimu wamtangaza Makamba urais 2015"



Walimu vijana wamezindua rasmi mtandao wao na kusema wanaunga mkono uamuzi wa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, wa kutangaza nia ya kugombea urais mwakani, ambayo wanaamini itatimiza ndoto ya vijana ya kujiongoza na kujitawala nchini.

Mtandao huo ujulikanao kama 'Mtandao wa Walimu Vijana Tanzania', ulizinduliwa baada ya viongozi wake kuchaguliwa katika mkutano uliofanyika mjini Dodoma jana.

Mratibu wa Mtandao huo, Frederick Mwakisambwe, akisoma maazimio katika mkutano huo, alisema wana wajibu wa kuvaa viatu vya mwalimu mwenzao, Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, siyo tu kushiriki kugombea uongozi, pia kuwaelewesha Watanzania aina ya kiongozi bora na makini atakayewafaa na kuwavusha salama kwenye changamoto za kizazi kipya.

Kwa maana hiyo, alisema wanataka taifa liongozwe na kiongozi mwenye kuendana na changamoto, mwenye fikra, mwenye kujua mahitaji, mwenye kuamini na kuaminiwa na mwenye kuzungumza lugha itakayoeleweka na kusikika na kizazi kipya.

“Tunataka sasa taifa liongozwe na damu mpya, damu changa, yenye maarifa, maono, uwezo na kasi kubwa ya kufikiria na kufanya maamuzi yenye kuleta maslahi kwa wengi na wengi hao ni sisi, ambao ni vijana,” alisema Mwakisambwe.

Aliongeza: “Tunafurahi kuona kijana mwenzetu January Makamba amejitokeza mbele na kutangaza nia ya kutaka kulitumikia taifa kwenye uchaguzi ujao. 

“Kwa kufanya kitendo hicho, tunasema siyo tu January ameonyesha ushujaa na uthubutu, bali pia ameonyesha ni jinsi gani vijana wana mapenzi ya dhati na taifa lao na wanaheshimu michango ya wazee wetu na hivyo tunawataka tuwasaidie pale walipoishia ili sisi vijana tuliongoze taifa lenye changamoto nyingi kwa fikra na maarifa mapya ya kizazi kipya cha vijana.”

Alisema Makamba ameonyesha namna gani watu waadilifu wanapaswa kuwa, dunia ya watu waaminifu, viongozi wenye kutaka kushika nafasi za juu kama urais, ambao hujitangaza mapema ili jamii imchambue na kumchuja kisha kujiridhisha kama anafaa au la.

Mwakisambwe alisema dunia ya watu waadilifu haisubiri kiongozi kuja kuomba akagombee urais, kwani urais ni utashi unaoambatana na uwezo na karama za Mungu, hivyo ni lazima ujipime mwenyewe kama unafaa.

“January (Makamba) amejipima na ametupa nafasi na sisi tumpime. Nasi walimu vijana tunamwambia asonge mbele, nyuma mwiko. Vijana tuliweza, tunaweza na tutaweza,” alisema Mwakisambwe.

Alisema dunia ya watu waadilifu haihitaji rais anayesubiri kuoteshwa na mizimu ya kwao kwamba, sasa nenda kagombee, wala dunia ya watu waadilifu haihitaji mgombea wa kufananisha urais na kuvuka daraja kwamba, mpaka alifikie ndiyo atangaze, bali waadilifu hutangaza nia na jamii huwachuja.

“Narudia, bila kuuma maneno, sisi Mtandao wa Walimu Vijana tunatangaza hadharani leo, kwamba tunaunga mkono nia ya kijana mwenzetu January Makamba na kwamba, tunamtaka asirudi nyuma kamwe,” alisema Mwakisambwe.

Alisema vijana ndiyo tunu ya taifa, ambao Watanzania wamewaamini na kuwaruhusu wawafundishe wadogo zao shuleni, leo zaidi ya asilimia ya walimu ni vijana na kuhoji: “Kwanini Watanzania hao hao wasituamini na kuturuhusu tuongoze Taifa kupitia January Makamba?”

“Kama Watanzania wametuamini vijana na kuturuhusu tulinde mipaka ya nchi hii, leo zaidi ya asilimia 80 ya wanajeshi ni vijana, kwanini Watanzania wasiamini na kutupatia amiri jeshi mkuu kijana?” alihoji Mwakisambwe.

Pia alisema kama Watanzania wamewaamini vijana na kuwakabidhi hospitali waokoe roho za wenzao, leo zaidi ya asilimia 90 ya madaktari na wauguzi ni vijana, hivyo, akasema Watanzania wana kila sababu ya kuwaamini na kuwapatia rais wa aina yao.

Vilevile, alisema askari polisi, waandishi wa habari, vibarua migodini na mashambani, wafanyakazi wa benki, mama lishe, ‘bodaboda’, madereva na makondakta, wafagiaji maofisini, wasafisha viatu, wahudumu wa baa na hoteli, wavuvi na waendesha mikokoteni na wasio na ajira wengi ni vijana.

Hivyo, akahoji: “Mbona huku hawaambiwi kuwa hawana uzoefu? Mbona huku hawaambiwi kuwa wabaguzi na kwamba, wanajipendelea? Kwanini tuulizwe uzoefu Ikulu tu?”

“Mbona asilimia kubwa ya walio na uzoefu ndiyo wenye kashfa za wizi na ufisadi mkubwa mkubwa unaoliangamiza taifa? Tunahitaji kiongozi wa kizazi hiki, huu siyo ubaguzi, huu ni ukweli, ukweli unatakiwa usemwe, siyo kuogopwa na kufichwa. Vijana ni wengi na sauti yao ni ya wengi, sauti ya wengi ni sauti ya Mungu na sauti ya vijana ni sauti ya Mungu,” alisema Mwakisambwe.

Aliongeza: “Tunamuunga mkono January Makamba kwa nia yake hiyo na kwamba, aendelee hivyo hivyo na sisi tutaendelea kuwaunganisha walimu vijana kote Tanzania kumpigania ili aje asikie kilio chetu cha samaki, ambacho machozi yake yamekuwa yanakwenda na maji kwa kipindi kirefu.”

 Alisema Makamba ni mzalendo, muadilifu na pia ana uwezo mkubwa wa kutambua na kuchambua mambo, hivyo hawana sababu ya kutokumuunga mkono.
Aliwaomba vijana wengine  zaidi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za  uongozi, ikiwamo uenyekiti wa serikali za mitaa na vijiji, udiwani na ubunge.

“Sisi Mtandao wa Walimu Vijana Tanzania, tunaahidi kuwafanyia kampeni January na vijana wenzake wote watakaojitokeza kwenye ngazi mbalimbali mpaka ndoto yetu ya vijana kujiongoza na kujitawala itakapotimia,” alisema Mwakisambwe.

Alisema wanataka kiongozi asiye na chembe wala nukta ya harufu za ufisadi, muadilifu ili wapumzike kusikia kelele za wizi wa mali za umma na kusema Makamba ni miongoni mwao.

Aliwataka walimu wa rika zote nchini kutoka mikoa yote kuunga mkono harakati zao hizi za kutaka taifa liongozwe na kiongozi anayeendana na kundi kubwa, mwenye sifa za kutosha, ya ujana ikiwa ni ya umuhimu wa kipekee.

Pia aliwakumbusha vijana wa kada na fani nyingine kwamba, wamekuwa wapigadebe vya kutosha, hivyo kwa sasa wanatakiwa wajipambe wenyewe, pia wamekuwa wasindikizaji vya kutosha sasa wajisindikize wenyewe.

“Tumekuwa wabebaji vya kutosha sasa tujibebe wenyewe, tumekuwa wasukumaji vya kutosha sasa tujisukume wenyewe na tumekuwa wawezeshaji vya kutosha sasa tujiwezeshe wenyewe. “Kumuunga mkono (Makamba) January kwetu sisi vijana ni kuunga mkono harakati za uundwaji wa taifa lenye fikra mpya,” alisema Mwakisambwe.

Mwenyekiti wa mtandao, Fredrick Philipo alisema kuwa uzinduzi wa mtandao huo umehudhuriwa na wajumbe 787, baadhi yao wakitoka mikoa ya Kigoma, Katavi, Lindi, Rukwa na Mtwara Phillipo ambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Viwanda iliyopo mjini Dodoma alisema kuwa mtandao huo una waasisi 100, na kwamba washiriki wote wa mkutano wamejigharimia safari kutoka kwenye mikoa 17 nchini ili kushuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa sekondari moja mjini Dodoma.

Alisema hadi sasa mtandao wao hauna ofisi, licha ya kwamba makao yao makuu kuwa Dodoma. 
Vilevile alisema mtandao  haujasajiliwa na kwamba malengo yake ni kuanzisha chama cha akiba na mikopo (Saccos) na kujihusisha na shughuli nyingine za uchumi ili kuwakwamua wanachama wake kiuchumi.

Alisema mtandao wao pia utakuwa unatoa mitazamo, na matamko kuhusiana na masuala  ya kitaifa hasa yanayogusa jamii na vijana.

MRATIBU WA MKUTANO
Katika hatua iliyowashangaza baadhi ya mashuhuda wa uzinduzi wa mtandao huo, ni kuwapo kwa mratibu wa mkutano ambaye ni Egla Mwamoto, mwanasiasa mwenye cheo cha ujumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) anayewakilisha mkoa wa Dodoma.

Alipoulizwa na NIPASHE kulikoni naye akawa miongoni mwa waratibu wa mtandao huo wa walimu vijana, Mwamoto alisema kuwa ushiriki wake wakati yeye si mwalimu, alisema kabla ya kuingia kwenye siasa, alikuwa mwalimu.

"Kitaaluma mimi ni mwalimu na niliwahi kufundisha," alisema bila ya kutaja shule aliyowahi kufundisha.

Inakadiriwa kuwa wajumbe hao, wametumia Sh. milioni 62.96 kwa siku kwa ajili ya posho za kujikimu nje ya kikao cha kazi kwa mujibu wa viwango vya serikali, achilia mbali ya nauli walizolipa kutoka kwenye mikoa yao, gharama za mawasiliano, usafiri wa ndani na matumizi mengine binafsi.

Julai 3, mwaka huu, akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), January Makamba, ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) alijitokeza hadharani na kutangaza nia yake hiyo, akiwa nchini Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano.

Makamba, ambaye ni mwandishi wa zamani wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete, alisema wakati huu ni wa kupisha fikra mpya kuongoza dola na kwamba, anaona wazee wakae kando. 

Siku moja baadaye, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walikaririwa wakisema kuwa Makamba yuko sahihi kutangaza nia.

Baadaye, baadhi ya makada wa CCM kwa nyakati tofauti, waliibuka na kuanza kumshambulia Makamba wakikosoa hoja ya msingi aliyoitumia kuamua kutangaza nia yake.

Rais Kikwete akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Soni Bumbuli, mkoani Tanga, wakati wa ziara yake ya siku tano, mkoani humo, mbali na kumsifu Makamba kwa kazi nzuri ya ubunge, ikiwa ni pamoja na kumsaidia sana kazi ya wizara aliyompa, alimkumbusha kwamba, kama Mungu akitaka, ndoto yake itatimia hata kama watu wote hawataki na isipotimia basi Mungu atakuwa hajaamua, hivyo asiweke nongwa.

Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, James Puya, akizungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE baada ya mkutano huo, alisema mtandao huo hautaiathiri CWT.

Alisema hiyo ni kwa sababu mtandao huo unatokana na walimu wenyewe na umelenga kuboresha maendeleo ya vijana katika nyanja mbalimbali, ikiwamo uchumi, ambao ni moja ya malengo ya CWT.

Pia alisema mtandao huo hauna itikadi za vyama na kwamba, hata kama itatokea kijana kutoka chama kingine cha siasa akatangaza nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi nchini naye pia watamuunga mkono.

Rais wa CWT, Gratian Mukoba, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana alisema  chama hicho hakifungamani na mtandao wowote wala pia hakijihusishi na siasa.

Alisema wanamtandao huo wana haki ya kuongea chochote kwa sababu siyo chama kwa sababu hakifungamani na CWT.
“Hata mimi hapa Mukoba nikiongea kitu kinachohusu siasa nitajitaja mimi mwenyewe na sitaihusisha CWT, kwa sababu kisheria CWT haifungamani na masuala ya siasa,” alisema Mukoba.

Naye Makamba alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana alisema: “Maazimio yenyewe sijayaona. Lakini kama ni hivyo unavyosema, basi nimepata nguvu na faraja kubwa. Imani huzaa imani. Imani waliyoionyesha kwangu walimu hawa nitailipa kwa imani.”
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom