Alhamisi, Julai 31, 2014

SIMULIZI YA MAISHA "USILIE NADIA SEHEMU YA NNE

SEHEMU YA NNE

Kama ni kulia hakika Nadia alikuwa Amelia haswa, na kama ni majuto hapakuwa na shaka alikuwa amejutia mengi sana ambayo aliyafanya kisha kutumbukia katika mdomo mbaya wa Desmund. Bado nilikuwa katika fumbo gumu sana la kuweza kujua nini kilijiri hadi binti huyu yakamsibu mazito kiasi kile. Alikuwa amekonda na hakuonekana kujali kuhusu hilo. Hakika alikuwa katika majuto makuu.

Sikutaka kusema neno lolote la ziada maana nilihofia kumtibua na kuanza kusimulia mkasa mwingine mpya ambao ungekiamsha kilio chake upya tena.

Lakini ni neno gani nilipaswa kusema na lipi sikupaswa kusema. Maana kama neno dogo la kiingereza nililosema lilimtibua Nadia na kujikuta akinieleza mambo mengine mengi. Ni neno gani lilikuwa sahihi kwa wakati ule. Nilifumba macho yangu na kumkabidhi Mungu wakati ule ili aniongoze vyema katika matamshi yangu.

 Ni kweli nilihitaji kuandika kitabu cha kusisimua kutoka katika simulizi ya kweli ya Nadia lakini bado sikupenda kumwona binti yule wa kiarabu akilia kilio cha uchungu, sikupenda Nadia alivyokuwa anajuta mbele yangu. Niliumia sana hakika. Lakini nilijionya kuwa kama nikiendel,ea na huruma ile nitajikuta siifanyi kazi yangu.

“Nadia mama….” Nilimuita, akageuka kunitazama.
Ebana eeee!!! Jicho jekunduuu!! Msichana alikuwa Amelia sana, kuwa jekundu pekee hakukutosha. Lilikuwa limevimba haswa.
“Abee!” aliitika, nikawahi kukwepesha macho maana nilihisi muda wowote naweza kutokwa machozi pia.
“Nenda ukaoge dadangu….nenda ukaoge….”
Alinitazama kiasi kwamba nikahisia ameijiwa na kumbukumbu nyingine, jambo ambalo sikuwa tayari kuliona likitokea. 
“Kuna maji ya moto…” aliniuliza kwa sauti ya chini ambayo ilikuwa inakwaruza.

Upesi nikairukia simu nikapiga mapokezi na kuomba huduma hiyo. 
Acha hoteli za kitalii ziitwe hivyo hivyo. Hazikupita dakika nyingi simu ikaita, nikapewa maelekezo kuwa tayari mambo yamesetiwa kitaalamu ni mimi tgu kama nataka kuoga.
Laiti kama ningekuwa na mahusiano na Nadia, siku hiyo ningemsaidia kumwogesha. Hakika alikuwa amechoka sana, alikuwa amechoka Nadia. Alistahili kusaidiwa lakini mimi nilibakia kuwa mwandishi tu. Alipoingia bafuni name nikaenda chumbani kwangu. Nikajimwagia maji.
Baada ya muda tulikuwa tunatelemsha ngazi kuelekea katika mgahawa mpana wa hoteli ya G & G. tukatafuta mahali tulivu tukajiweka hapo.
Mara muhudumu akafika tukiwa tunapitia karatasi ya orodha ya vyakula.
“Tutakuita” nilimweleza akajiondokea huku akiwa anaendelea kutabasamu kama ilivyo kawaida ya wahudumu.
“Hivi hawa Capuccino (soma: kapuchino) yao itakuwa murua.” Nilimuuliza Nadia ambaye alikuwa mwenyeji wa jiji la Mwanza.
Cappuccino ni kinywaji mchanganyiko wa kahawa na maziwa na madikodiko mengine, mara nyingi kinapatikana katika hoteli za wazito.

Kwa mara nyingine Nadia akatabasamu, kisha kwa mara ya kwanza kabisa Nadia akacheka, Nadia alicheka vyema na kwa mara ya kwanza nikafanikiwa kutambua kuwa kabla ya matatizo Nadia alikuwa mrembo haswaa. Kubwa zaidi alikuwa na mwanya katikati ya meno yake ya mbele.
Ebwanaa eee! Kilichofuata hapo ni kingine. Alianza kwa furaha….
“Ina maana unanicheka Nadia au haitamkwi hivyo jamani, hivi ni kapuchino ama kapusino…mi sijuagi hata” nilimweleza huku nikiwa katika kufurahia tabasamu lake.
“Hamna inaitwa hivyo hivyo ila umenikumbusha dada yake Desmund, mwenzangu!! mara yake ya kwanza kuiona hiyo Kapuchino sasa, kwanza alikuwa haijui, hata Desmund mwenyewe alikuwa haijui lakini eti siku hiyo akajifanya anaijua sana akamwambia dada yake aitamke, he! Akasema kafufinyo wacha tucheke hadi nikapaliwa, maskini wifi yangu akawa amekodoa macho tu. Sie tunacheka na Desmund wangu.

Mambo yanabadilika kweli jamani, wifi yangu Janeth yaani alikuja huku mjini miguu imepasuka wewe sijui nd’o wanaita magwambala, imepasuka haswaa, yaani dah! Mimi hata sikujali, alikuwa hajui kutamka maneno mengine ya Kiswahili lakini yote mi nasema Mungu atanilipia, kweli Janeth mimi nilimpatia nguo zangu, sikuona aibu kumfunza mambo mengi ya mjini hatimaye nikamtafutia kazi akaanza kujitegemea kwa mshahara wake mkubwa tu. Mshahara ambao kwa darasa lake la pili aliloishia angelipwa kwa mwaka mzima ama miwili. 

Janeth hakuyakumbuka haya, Janeth akasimama kidete kabisa anamweleza kaka yake eti mimi ni mchawi nimemwendea kwa mganga nimemwekea dawa, Janeth jamani yaani nilipokosa kanga ya kujifunika huko kijijini kwao nikachukua kanga yake akanikwapua na kudai nitaiwekea chawa kanga yake. Janeth ambaye alikuja mjini akiwa ananuka mbuzi na ng’ombe nikampulizia marashi nikamkumbatia bila kujali harufu yake, na yeye akasimama kunipinga, Janeth kweli nikaugua Malaria akashangilia eti madawa ya mganga yamenirudia, mwandishi yaani mimi sijui lolote kuhusu waganga , sijawahi kwenda Mungu aliye hai ananiona, sasa nilimkosea nini mimi Janeth., na Desmund akanyanyua kinywa chake akadai dada yake huwa hasemi uongo hata kidogo. Amakweli mfadhili mbuzi akikukera umle nyama si mwanadamu, si mwanadamu nasema.

Mwandishi yaani kumbe kumtunza kote huko huyo Janeth wala hakuwa dada yake na Desmund, eti kumbe ndiye yule mke ambaye alichaguliwa na mama yake, kwa hiyo Desmund kumbe hakunipenda tangu zamani yule. Alinitumia tu, sitaki kukumbuka pesa zangu alizotumia lakini kwa nini ameivuruga akili yangu kwa kiasi kile. Desmund na Janeth ni wanadamu wa aina gani sasa hawa, eeh!! Wanadamu gani msiojali kuwa Nadia hana ndugu mwingine katika dunia hii mnaitwaa Roho yake mnaitwangatwanga. Si mngechukua pesa zangu zote, si mnenidhulumu hata viungo vyangu iwapo vinafaa mkaniachia moyo na roho yenye amani, mbona mkanitenda vile.
Yaani Desmund kweli ukamwachia huyo mwanamke wako duka langu kubwa la nguo kisha ukanipeleka mimi huko kwenu mimi nikawe mvuvi wa samaki, Desmund ukanikabidhi katika kundi la wanaume eti nijifunze uvuvi. Desmund saa nane usiku mtoto wa kike ukaniacha ziwa Viktoria, desmund si heri ungenipiga risasi mimi Nadia nife mara moja kuliko kuniua taratibu. Nikayavumilia hayo yote hukujali, ukanikomaza mikono Desmund kwa kushika nyavu na kuwavua samaki. Wewe na hawara yako mnatesa na mali zangu unaniambia ni dada yako, shenzi kabisa Desmund, shenzi nasema. Na laiti ningejua mapema Desmund wallah ningekufanyia kitu kibaya ujue, Desmund nilikustahi sana we mwanaume. Ujue sitakiwi kulaumiwa mimi sitakiwi kabisa kulaumiwa basi tu lakini yaani basi….
Unanikabidhi kwa wavuvi kisha wananitaka kimapenzi ukaniita mimi Malaya eti ni mimi nawataka. Hivi Desmund nani alikudanganya kuwa wewe na hao ndugu zako kuwa mlikuwa na mvuto wa kupagawisha msichana?? Basi tu nilikupenda mimi Nadia, haukuwa na hadhi walau ya kunisimamisha na kuanza kunitongoza hakika. 

Lakini nafasi niliyokupa ukaamua uitumie vyema, eti huyo unayemuita dada yako, na mama yako ambaye sipendi kutukana lakini ni mama mjinga kupita wote duniani mnaniweka kikao na kunishutumu kuwa ninafanya umala katika mtumbwi. Hivi mlikuwa na akili ninyi viumbe mlikuwa na akili Desmund.
Nakuomba nirejee kuuza dukani kwa sababu upepo wa bahari unaniumiza kifua unanieleza kuwq mahesabu yatanichanganya hapo dukani labda Janeth akipata muda anielekeze, Desmund ulikuwa umelewa siku hiyo ama? Yaani Janeth aliyekuja na miguu imepasuika mjini wewe na yeye kwa pamoja hamjui kapuchino wakati huo mnatumia pesa yangu, leo hii unaniambia eti sijui mahesabu yatanichanganya. Hakika ulipitiwa na dharau ya hali ya juu. Na kama hiyo haitoshi ndugu mwandishi Desmund, mama yake na huyo Janeth siku moja wa…….” 
Kabla hajamaliza muhudumu alikuwa amefika, tukamuagizia kapuchino mbili. Moja ya kwangu na nyingine ya Nadia.
Nadia akasitisha mazungumzo yake, akainama kwa muda. Mimi nikjapiga funda moja la kapuchino kisha nikamsihi Nadia naye apate kapuchino kabla haijapoa.
Akainua uso wake nikampatia kitambaa akajifuta machozi kabla hayajatiririka.

Kisha akapiga funda moja kubwa.
“Si nilikwambia yaani hawa jamaa kapuchino yao wanatumia maziwa freshi kabisha sijui wanayatolea kwa akina Desmund maana wana mang’ombe mengi hao duh halafu yana afya kama nini…..” hapa alisema huku akitabasamu.
Nilimtazama kidogo nikamjibu kwa tabasamu pia kisha nikainama.
Nikajiwekea maswali na majibu mapya.

MOJA; Yaani Desmund na Janeth kumbe ni wapenzi wakahudumiwa na NADIA jijini Mwanza….UNYAMA NA USHAMBA MKUBWA….

MBILI: NADIA binti wa kiarabu akapelekwa kuvua samaki…HATARI hii lazima kulikuwa na kitu hapa.

TATU: NADIA alipogundua Janeth ni mke mwenza nini kilitokea???

NNE: Mbona NADIA anadai hatakiwi kulaumiwa???

TANO: DESMUND, MAMA YAKE NA JANETH wapo wapi??

Nikapiga funda jingine kubwa la kinywaji kile cha moto huku nikikiri kuwa hakika kapuchino yao ilikuwa maridadi kuliko baadhi ya maeneo jijini Dar es salaam.
Nikamtazama Nadia naye alikuwa amejikita katika kukifurahia kinywaji kile.
Kimya kikatanda…. USIKOSE NINI KITAENDELEA



Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Maskini Nadia...mmh pole

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom