Jumatano, Julai 16, 2014

WATOTO WOTE WANA HAKI SAWA, UKATILI HUU HADI LINI? "Mtoto mlemavu afungiwa ndani"


Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wenye ulemavu wilayani Karagwe, vimezidi kukithiri huku wadau wanaotetea haki za watoto wakiendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kukabiliana na tatizo hilo.
Hayo yalibainika juzi baada wadau wanaotetea haki za watoto kumtembelea Apewe Mathayo (12), ambaye ni mtoto mwenye ulemavu wa viungo aliyefungiwa ndani kwa miaka 11.
Mtoto huyo aliokolewa na mkazi wa Kijiji cha Kamagambo, Kata ya Kiruruma, wilayani Karagwe, baada ya kutelekezwa na wazazi wake.
Shirika la kuhudumia walemavu la Karagwe Community Based Rehabilitation Programme (KCBRP) kwa kushirikiana na wadau wanaotetea haki za mtoto ambao ni Dawati la Jinsia la Polisi Karagwe, Ofisa Ustawi wa Jamii na viongozi ngazi ya kijiji walikwenda nyumbani kwa Mathayo Rwakibala kufuatilia maendeleo ya mtoto huyo.
Apewe anadaiwa kutelekezwa na wazazi wake kwa miaka 11 kwa kufungiwa ndani hadi Septemba mwaka jana alipogunduliwa na Biashara Severian, ambaye alitoa taarifa kwa Shirika la KCBRP ambalo lilianza kumhudumia.
Katibu Mtendaji wa KCBRP, Aggrey Mashanda alisema tangu kutambuliwa kwa mtoto huyo wamepeleka msaada wa vitu mbalimbali vikiwamo mavazi, vyakula vya lishe, kukarabati chumba anacholala, kununua godoro na kitanda.
Misaada mingine ni kumnunulia ng’ombe wa maziwa, lakini jitihada zote hazijazaa matunda kutokana na familia hiyo kutomjali.
Mashanda alisema wameshirikisha wazazi wake kuchangia kiwango kidogo ili waanzishiwe mradi wa kuingiza kipato, lakini familia hiyo haijaonyesha ushirikiano na imeshindwa kumpeleka Hospitali ya Kagondo kufanya mazoezi.
Baba ya mzazi wa mtoto huyo, Rwakibala aliahidi kutimiza ushauri wote aliopewa na wadau hao, huku akikiri kuwa yupo tayari kutoa huduma zinazostahili kwa mtoto huyo na kuacha kumnyanyasa mke wake.
Naye Ofisa Ustawi Jamii Wilaya ya Karagwe, Owokusima Kaihura aliagiza familia hiyo kuhakikisha inampa mtoto huyo matunzo na huduma stahili na kwamba, bila kufanya hivyo sheria itachukua mkondo wake.CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom