Alhamisi, Agosti 21, 2014

HUU NI UKATILI SANA KWA WATOTO " Mzazi Awachoma moto mikononi kwa tambi za jiko Kisa Walichelewa nyumbani kutoka kuangalia tv"



Watoto wanaodaiwa kufanyiwa ukatili wakionyesha vidonda kwenye mikono yao ambavyo vinatokana na kuchomwa moto na baba ya mzazi nyumbani kwao Mbagala Kibondemaji jijini Dar es Salaam jana. 
Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na baadhi ya wazazi, vimezidi kukithiri nchini baada ya watoto wawili kudaiwa kuchomwa moto mikono na baba yao kwa kutumia tambi za jiko jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, anayetuhumiwa kufanya unyama huo ni Salum Juma, fundi gereji wilayani Temeke, mkazi wa Mbagala Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam.


Watoto hao mmoja mwenye umri miaka saba na mwingine miaka mitano (majina yao yamehifadhiwa), akiwamo wa  kumzaa na wa kufikia walikutwa na mkasa huo baada ya kwenda kuangalia runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa 5:00 usiku Alhamisi wiki iliyopita. 



Akizungumza na NIPASHE, jirani yao, Omar Fusi, alidai watoto hao walieleza kuwa walichomwa na baba yao na kufichwa ndani, lakini baadaye majirani waliwaona watoto hao wakiwa na majeraha.



Fusi alisema baada ya kuwaona wakiwa na majeraha, waliwahoji ambapo walieleza kuwa walichomwa na baba yao baada ya kuchelewa kurudi kutoka kuangalia televisheni.



Kwa mujibu wa Fusi, kitendo hicho kilifanyika huku mama yao akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.



Fusi alisema baada ya kubaini tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibonde Maji ‘B’, Teofile Balae, ambaye alitoa taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kata ya Mbagala, Eliameresa Kaaya na kuripoti polisi na kufanikisha baba huyo kukamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Maturubai ambako anaendelea kushikiliwa.



Balae alisema baada ya kushirikiana na Ofisa Ustawi wa Jamii na baba huyo kukamatwa, waliwachukua watoto hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbagala Kuu kwa ajili ya kupata fomu ya PF3 na kuwapeleka katika hospitali ya Mbagala Rangi Tatu kupatiwa matibabu.



Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Erasto Kibara, alisema walibaini watoto hao kufanyiwa ukatili huo baada ya kumkuta mmoja wao adukani alikotumwa akiwa na majeraha na kumuuliza kilichompata kisha alitoa taarifa hizo kwa mwenyekiti wa mtaa huo.



Ofisa Ustawi wa Jamii, Kaaya, akizungumza na NIPASHE katika Kituo cha Polisi Maturubai wakati watoto hao wakichukuliwa maelezo na polisi,  alisema kitendo walichofanyiwa watoto hao ni cha kikatili na kuwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapogundua ukatili katika mitaa yao ili kutokomeza vitendo hivyo vilivyoshika kasi nchini.



NIPASHE iliwashuhudia watoto hao katika Kituo cha Polisi Maturubai huku wakiwa na majeraha mkononi wakati wakichukuliwa maelezo na maofisa wa polisi wa kituo hicho.



Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk. Julius Nyakazilibe, alithibitisha watoto hao kupokelewa hospitalini hapo na kupatiwa huduma ya matibabu kutokana na majeraha yaliyosababishwa na moto.



“Ni kweli watoto hao tuliwapokea hapa hospitalini wakiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii na walipatiwa matibabu,” alisema Dk. Nyakazilibe. Mama mzazi wa watoto hao, Christina Menasi, akiwa katika kituo cha polisi na mtoto wake mchanga huku akimnywesha uji, alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa katika biashara yake ya kuchoma mihogo na aliporudi nyumbani na kukuta hali hiyo, aliingiwa na hofu ya kuripoti tukio hilo kwa kumhofia mumewe.



Mama huyo alilaani kitendo hicho cha kikatili lakini alisema akifungwa yeye ndiye atakuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo.



“Inatakiwa tuache vitendo hivi vya kikatili, lakini ikiwa mume wangu atafungwa, mimi ndiye nitakayebeba mzigo wa kulea hii familia,” alisema Christina.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Maturubai na kwamba upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO: NIPASHE

Maoni 1 :

Yasinta Ngonyani alisema ...

jamani ukatili huu yaani mpaka kuchoma moto kisa kuchelewa kurudi inasikitisha sana

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom