Ijumaa, Septemba 05, 2014

SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 31


ILIPOISHIA
Kesho yake asubuhi na mapema alikuja mwalimu aliyekuwa anafundisha katika shule wanayosoma wadogo zangu, wakati huo wadogo zangu pamoja na Charito walikuwa wamekwi sha ondoka. Mwalimu huyu alikuja kunipa taarifa ya msiba uliotokea shuleni  “Dada ujio wangu huu ni kuhusu taarifa za msiba, jana kuna mtoto alifariki baada ya kun’gatwa na mbwa, wakati akiwa anacheza na watoto wenzake, pia alikuwepo na mdogo wako Tumaini, nimekuja kukujuza kwasababu kwa niaba ya wanafunzi waliokuwa pamoja wanasema kuwa walimuona Tumaini akiwa ameongozana na mbwa huyo, sasa sijui huyo mbwa yupo hapa nyumbani” ? JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 31.

INAPOENDELEA
Nilikuwa namsikiliza yule mwalimu kwa makini, na kisha nilinyamaza kimya kidogo huku nikiwa natafakari moyoni mwangu "Mh haya ni maajabu kwakweli, Inamaana Tumaini atakuwa alitoka wapi na huyo Mbwa jamani mbona hapa nyumbani sisi hatufugi mbwa" Nilikuwa nawaza moyoni huku yule mwalimu akiwa ananitizama na kusema, "Kandida nazungumza na wewe naona umekuwa kimya ghafla".

Nilimtizama kwakumkazia macho kisha nikasema "Inanishangaza  kweli, kwani hapa nyumbani sisi hatufugi Mbwa kwahiyo ukiniambia kuwa Tumaini ameonekana na mbwa aliyesababisha kifo cha mwanafunzi wako, ni jambo la kushangaza sana inawezekana huyo mbwa ni wa maeneo ya huko huko shuleni kwenu, hapa nyumbani kwangu hatufugi mbwa" Niliongea kwa msisitizo.


Mwalimu alinisikiliza kwa makini baadaye aliniaga na kuondoka, Tumaini aliporudi kutoka shule, ilinibidi nimuulize kuhusu mbwa aliyeongozana naye shule. lakini baada ya kumuuliza Tumaini alikataa na kusema kuwa hakuongozana na mbwa huyo kwani hata yeye alishangaa kumuona mbwa mazingira yale ya shule. Maisha yaliendelea taratibu za msiba zilifanyika na hatimaye mwanafunzi yule alipumzishwa katika makazi yake ya milele. 

Baada ya wiki moja kupita sikumoja yapata majira ya saa sita za usiku wote tukiwa tumekwisha pumzika, mimi niliamka kwa ajili ya kwenda kujisaidia haja ndogo, nikiwa natoka nje kwa mbali nilisikia kama kuna kitu kinatembea na kwa wakati huo mimi nilikuwa chumbani na Charito alikuwa kitandani amelala fofofo, mwanzoni nilifikiri labda nimesikia vibaya ikanibidi nitulie nakusikiliza kwa makini ndipo niliposikia kama mtu anatembea kwa kishindo kikubwa sana, niliwaza na kufikiri labda atakuwa ni mdogo wangu anakwenda kujisaidia.
 ikanibidi nifungue mlango taratibu na ili kuhakikisha ni nani alikuwa anatembea.

Baada ya kufungua mlango nakutoka nje nikiwa naelekea sebuleni, taratibu huku nikiwa mwenye hofu nyingi ghafla alipita mbwa mweupe na alielekea moja kwa moja katika mlango wa sebuleni, kwa wakati huo nilikuwa sijawasha taa, nilishtuka sana huku nikiwa natetemeka nilisogea ukutani nakuwasha taa ili nimuangalie kwa makini yule mbwa, baada ya kuwasha taa yule mbwa alitoweka na sikumuona tena, nilibaki nikiwa nimepigwa butwaa na mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi sana moyoni mwangu niliwaza "Mungu wangu huyu mbwa atakuwa ametokea wapi, mbona mimi sijawahi kumuona humu ndani na pia atakuwa ameingiaje, au yawezekana ni yule mbwa ambaye amesababisha kifo cha yule mwanafunzi, haya ni maajabu jamani".

 Niliendelea kuwaza huku nikiwa nimesimama bila ya kufanya chochote, Charito alifungua mlango na kuniona nikiwa nimesimama huku nikionekana kuwa na hofu nyingi, alinitizama na kusema "Unafanya nini usiku huu wa manane huku sebuleni, na tena unaonekana kuwa na hofu sana" Nilimsogelea na kumsimulia kile nilichokiona, alicheka na kusema "Wewe utakuwa ulikuwa unaota, sasa mbwa atokee wapi huku ndani, achana na hayo mawazo embu  twende tukapumzike" Huku akiwa amenishika mkono  na kutaka turudi chumbani, kwa wakati huo hata kwenda kujisaidia nilisahau kabisa kutokana na hofu niliyokuwa nayo.

Kesho yake asubuhi na mapema kama kawaida Charito aliwahi kuondoka mapema kuelekea kazini, na mimi niliamka  nakumuandaa  Tumaini ili aweze kuwahi kwenda shule, na kwa wakati huo Renata alikuwa bado amelala,  kitu ambacho kilikuwa siyo kawaida ilinibidi nimfuate chumbani kwani muda wa kwenda shule ulikuwa umewadia nilipoingia chumbani nilimkuta akiwa amejikunyata kwenye shuka kana kwamba ni mtu ambaye alikuwa akisikia baridi kali sana. Nilimsogelea na kumshika "Renata, Rena, wewe Rena...... embu amka unachelewa kwenda shule".

 Aliamka taratibu huku kwa sauti ya unyonge akisema "Dada Kandida, mimi leo nimechoka sijisikii kwenda shule, mwili wangu unauma sana" Aliongea huku akiwa ananitazama kwa upole, nilimtizama na kusema "Unasema hujisikii kwenda shule, inamaana unaumwa au ni kitu gani tena Mungu wangu, mbona umelegea hivyo mdogo wangu, itabidi tuende hospitali haraka". Hali ya Renata haikuwa nzuri kwani alikuwa anaumwa na hata nilipomshika  katika mwili wake alikuwa na joto kali sana. Ilinibidi nimsindikize haraka Tumaini kuelekea shule ili nikirudi nimchukue Renata kumpeleka hospitalini.

Baada ya kumfikisha Tumaini shule haraka nilirudi nyumbani nilipofika nilimkuta Renata akiwa ameketi sebuleni akinisubiri huku akiwa anatetemeka mithili ya mtu aliyemwagiwa maji ya baridi, nilimsogelea na kumshika paji lauso wake "Usijali mdogo wangu utapona, ngoja nikupeleke hospitali  ili ukapatiwe matibabu" Renata alinishika mkono na kusema "Dada Kandida, nimemuona mbwa mweupe chumbani kwangu, nimeogopa sana sijui ametokea wapi?" Nilishutuka sana Renata aliposema amemuona mbwa chumbani kwake nilimgeukia na kusema "Unasema, umeona nini? Mbwa , wapi na saa ngapi?" Renata alinitizama tena kwa macho ya upole na kusema "Nimemuona jana usiku na leo muda si mrefu wakati ulipoenda kumpeleka Tumaini shule, Dada yule mbwa siyo mzuri anaweza kunizuru dada mimi naogopa".

 Nilibaki nikiwa nimenyamaza kimya kama dakika mbili huku nikitafakari moyoni "Inamaana yule mbwa niliyemuona jana usiku na Renata amemuona huyohuyo, Mungu wangu hii nyumba ina maajabu gani, inaniogopesha sana hali hii, sasa sijui nianzie wapi kumtafuta huyo mbwa na hata nikimueleza mume wangu Charito hawezi kuniamini kile ninachokisema, sijui nini kinaendelea katika hii nyumba" Nikiwa naendelea kuwaza Renata alinivuta mkono na kusema "Dada inabidi uwe makini sana kwani shemeji siyo mtu mzuri, na hata Tumaini, siyo yule Tumaini ulieyekuwa unamfahamu, shemeji anamtumia Tumaini katika.....".

 Akiwa anataka kuendela kuongea nilimkatisha na kusema "Hapana Renata, twende kwanza hospitali kwani hali yako siyo nzuri " Nimshika mkono na kuongozana naye kwenye gari lakini Renata aliendelea kusema "Dada nakuomba unisikilize maneno yangu, na pia ufanye uchunguzi kwa yale yote niliyokueleza" Aliongea Renata huku moyoni mwangu nikiwa nawaza "Yawezekana Renata akawa sahihi sasa itanibidi nikamlete mchungaji aje kutuombea familia nzima ili kuondokana na haya majaribu ya shetani, kwasababu nashindwa kuelewa kabisa nini hatima ya haya mambo yote kila kukicha kumekuwa na mauzauza ya hapa na pale sina budi kumshirikisha mwenyezi Mungu kwa nguvu zote ili aweze kutusaidia." JE NINI KITAENDELEA USIKOSE.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Dada Adela hadith nzuri ila unachelewa sana kuitoa kwani umepanga uweunairusha humu siku gani kwa wiki?

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom