Jumanne, Septemba 09, 2014

SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 32


ILIPOISHIA
"Yawezekana Renata akawa sahihi sasa itanibidi nikamlete mchungaji aje kutuombea familia nzima ili kuondokana na haya majaribu ya shetani, kwasababu nashindwa kuelewa kabisa nini hatima ya haya mambo yote kila kukicha kumekuwa na mauzauza ya hapa na pale sina budi kumshirikisha mwenyezi Mungu kwa nguvu zote ili aweze kutusaidia." JE NINI KITAENDELEA USIKOSE.

INAPOENDELEA
Nilikuwa nawaza sana wakati tukiwa tunaelekea hospitali, nilimtizama Renata, huku moyoni mwangu nikitafakari "Ni mara nyingi Renata amekuwa akinieleza kuwa Charito siyo mtu mzuri, sasa mbona mimi nashindwa kuona chochote kibaya kinachomuhusisha Charito, na pia ukizingatia Charito ameokoka na anamjua Mungu, haiwezekani akawa na mambo ya kishirikina, lakini yawezekana nisilolijua ni sawasawa na usiku wa kiza kinene, na kila nikifikiria haya mauzauza yanayotokea nyumbani, nashindwa kuelewa inabidi niwe makini sana" Nilikuwa nawaza nakujiuliza maswali mengi sana bila yakupata majibu.

Tulipofika Hospitali, haraka nilimpeleka Renata kupata vipimo. Baada ya kuchomwa sindano ya kupima damu tuliketi pembeni kusubiria majibu. Nikiwa nimeketi huku nimemshika mkono Renata, alipita mchungaji akiwa ameshilikia kitabu cha dini (Biblia) na alitusalimia, Renata alionekana kutabasamu huku akimtizama mchungaji kwa umakini sana, mchungaji naye alimtizama  na kusema "Pole sana mtoto mzuri, Mungu atakusaidia utapona".



 Renata alinyanyuka na kumshika mkono mchungaji, bila kutarajia nilishangaa Renata anaanza kusema "Mchungaji, naomba tuende nyumbani kwetu ukatuombee, tafadhali mchungaji naomba uongozane nasi" Mchungaji alinitazama na kusema "Dada sijui unaitwa nani, naona ni vyema tukafahamiana  mimi naitwa Mchungaji James, nimefurahi sana kuona mdogo wako akihitaji maombi, anaonekana ni mtoto mzuri sana anayejua kuwa Mungu ni mwema katika maisha yetu ya kila siku" Nilinyamaza kimya kidogo  na kisha nikasema "Mimi naitwa Kandida, na huyu ni mdogo wangu anaitwa Renata".

Mchungaji alisogea na kisha kuketi huku akisema "Nimefurahi kukutana na wewe Kandida, mdogo wako anaumwa nini?" Aliuza mchungaji "Bado sijajua nini kinachomsumbua kwani ndiyo tunasubiri majibu baada ya kuchukua vipimo" Niliongea huku nikimtizama yule mchungaji, ambapo  tuliendelea kuzungumza na baadaye alitukaribisha kwenda kusali katika kanisa lake, lakini mimi nilimueleza kuwa huwa tunakwenda kusali katika kanisa la mchungaji Mkombozi. Mchungaji yule aliposikia kuwa nimetaja jina la mchungaji Mkombozi alionekana kunyamaza kimya kwa muda na kisha akasema "Umesema unasali, kwa mchungaji Mkombozi? Kanisa lake lipo wapi? " Aliuliza mchungaji "Kanisa, lipo maeneo ya Mwenge, karibu ujumuike pamoja nasi ukitaka kuja unaweza kunipigia simu nikakuelekeza ni mchungaji mzuri na anafundisha mambo mazuri sana".

 Renata alikuwa amenyamaza kimya kwa muda mrefu lakini aliposikia kuwa namzungumzia mchungaji Mkombozi alinyanyuka na kusema "Hapana Dada Kandida, mchungaji Mkombozi siyo mtu mzuri, mimi siendi tena kanisani kwake, yule siyo mtu wa Mungu" Nilijisikia vibaya sana baada ya Renata kutamka maneno yale, nilianza kumkataza lakini mchungaji James akasema "Hapana Kandida, muache mtoto azungumze, tambua kuwa watoto ni malaika, na wanaona mambo mengi sana, kwahiyo ni vyema ukamsikiliza na wakati mwingine unakaa na kutafakari kile alichokueleza na baada ya hapo unafanya uchunguzi, kwani huwezi kujua kama anachokisema ni kweli ama ni uongo bila ya kusikiliza na kufanya uchunguzi" Aliongea mchungaji huku akimshika mkono Renata. 

Nilinyamaza kimya bila ya kujibu chochote. Baada ya muda kidogo Niliitwa na Daktari, ili kupewa majibu ya vipimo vya Renata. Nilinyanyuka na kumshika mkono Renata huku tukielekea chumba cha Daktari,  mchungaji alisema anatusubiri kwani angependa kutufahamu zaidi. Renata aliendelea kumsisitiza mchungaji aongozane na sisi kwenda kufanya maombi nyumbani. Vipimo vilionyesha Renata alikuwa anaumwa homa tu ya kawaida, ilinibidi nishangae kwani kwa hali aliyokuwa nayo Renata asubuhi wakati anaamka nilijua atakuwa na malaria kali sana, lakini ilikuwa ni tofauti na hivyo Daktari alitupa dawa za homa na kisha tuliondoka.

 Kwa wakati huo mchungaji alikuwa ameketi nje ya Hospitali akitusubiri, Renata alipomuona mchungaji alifurahi sana na kusema "Dada Kandida nakuomba tuongozane na mchungaji hadi nyumbani" Moyoni mwangu nilikuwa nikiwaza "Mmh huyu mtoto kwanini, anashindwa kumuamini mchungaji Mkombozi, na anawezaje kumuamini huyu mchungaji ambaye tumekutana naye tu hapa Hospitalini, lakini nikifikiria ile nyumba ilivyo na mauzauza kila kukicha naona ni vyema nikaongozana na huyu mchungaji tukafanye maombi, naimani Mungu atatusimamia katika haya majaribu tunayopitia"

Baada ya kutafakari niliamua kukubali ombi la Renata, na sasa tuliongozana na mchungaji hadi nyumbani, hatimaye tulifika na kwa wakati huo Tumaini alikuwa yupo shule, na n mume wangu Charito alikuwa amekwenda kazini. Nilimkaribisha mchungaji James alipoingia tu pale sebuleni alisimama mlangoni na kusema "Mungu wangu, naomba uniongoze niweze kumtokomeza mtu huyu" Nilishtuka na kumtizama mchungaji ambaye alinisogelea na kunishika mkono mimi pamoja na Renata na kuanza kufanya maombi, alisali sana, baadaye nilihisi kama naishiwa nguvu wakati mchungaji akiwa anaomba hatimaye nilianguka chini, baadaye nilikuja kushtuka nikiwa nimeketi kwenye kochi na mchungaji James alikuwa amesimama na Renata wakiwa wananitizama. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 33.




Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

R

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom