Jumatano, Septemba 10, 2014

SIMULIZI YA MAISHA USILIE NADIA SEHEMU YA 12

Nadia alilala hatimaye, nikamsaidia kuviondoa viatu vyake miguuni nikamfunika shuka kisha nikaishusha na neti ili asisumbuliwe na wadudu warukao iwapo watatokea. Nilimtazama binti yule aliyekuwa amefumba macho, uso wake ukiwa mwekundu na machozi yaliyomtoka muda mfupi uliopita yakiacha michirizi.Nilitikisa kichwa huku mengi yakipita katika kichwa changu!! Ni kipi kilimfanya hadi kila hatua anayopita akutane na mikasa mizito kiasi hiki.

Japo mimi nilikuwa sijwahi kutokewa na msala kama huu lakini nilikiri kuwa kama ningevaa viatu vya Nadia na kuwa yeye. Kwa haya magumu aliyopitia bila shaka ningekuwa nilishajikatia tamaa kitambo kirefu na labda hata ningekuwa nilishajifia huko kwa kujiua.
Lakini Nadia alikuwa anaishi na alikuwa akiusimulia mkasa huo ambao ulimweka katika nafasi ambayo alikuwa sasa. Nafasi ya mjutaji!!
Hakika alikuwa mwanamke wa aina yake binti huyu!!
Nilitafakari sana na usingizi ulinipitia baadaye sana usiku!!



Majira ya saa tatu na nusu asubuhi nilikuwa katika chumba cha Nadia tena, siku hii nilimkuta akiwa amemaliza kujiandaa, tulikuwa na safari ya kwenda katika hifadhi ndogo ya ‘SAA NANE’ iliyopo jijini Mwanza.
Tulitaka tuwahi kwenda ili tuwahi kurudi.
“Leo umejitahidi kuwahi!” alinambia.
“Aah! Leo nimeota ndoto mbaya nilikuwa nakimbizwa, sasa nikajikwaa, ile nainuka nikimbie tena nd’o nainuka kitandani.” Nilimtania tu lakini akastajabu…
“Eheee…umenikumbusha umenikumbusha…” alisema huku akijilazimisha kukumbuka jambo fulani…hapo nikatambua kuna maelezo marefu yanataka kutoka katika kinywa chake, nikabofya kifaa changu cha kurekodia kilichokuwa mfukoni.
“Nini tena Nadia au na wewe umeota unakimbizwa…” nilidadisi.

“Hapana kaka huenda kweli ni Desmund alimuua jamani!! Desmund atakuwa alimuua..”
“Nani tena Nadia….” Nilimuuliza swali kimakosa, sikutakiwa kumuuliza, lakini haikuleta madhara yoyote kwani huenda hata hakunisikia.
“Ujue jana nimegundua kitu ambacho nilijiuliza siku nyingi sana, huenda yeye Desmund aligoma kabisa kukiri lakini nilibaki na imani hiyo kuwa ni yeye alimuua Danny yule askari mpelelezi. Maskini Danny, sawa alikuwa na mabaya yake lakini kwa nini Desmund alimuua kwa kuniibia siri kidogo tu isiyokuwa na mantiki?

Jana nilikwambia nilivyokuwa nimewekwa rumande bila kutolewa kwa ajili ya mahojiano, nilikwambia jina kama Danny hivi. Yah! Danny!! Bila yeye nadhani ningeweza kuishia kuhamishwa rumande na kiha kutupwa gerezani bila kosa lolote, Danny alinitoa rumande na kuamua kunihoji, alinihoji kama mtu anayejua kitu fulani, alinihoji maswali mengi sana, nami kwa kuwa sikuwa na njia nyingine bali kusema ukweli nikamweleza juu ya hila ninayofanyiwa na Desmund na familia yake kwa ujumla. Danny alinisikiliza huku kila baada ya dakika kadhaa akiandika nukuu anazozijua yeye.
Baada ya mahojiano aliniambia kauli nzito. “Binti, kwanini usijiweke mbali na Desmund. Jiweke mbali naye yule atakusumbua sana, kila mtu mweupe anayejaribu kumgusa kwa sasa anaishia pabaya. Desmund hapendi wahindi, hapendi waarabu na anayo haki ya kuwachukia. Wewe jiweke mbali naye tu!!
“Lakini alikuwa mume wangu!!” niliingilia kati.
“Kuwa mume wako ama bwana yako kwa sasa haina maana, tuachie sisi tunaomjua Desmund na historia yake, cha muhimu kwa sasa jiweke mbali naye. Kulingana na maelezo yako, umenijeruhi sana kama ni mateso yametosha na hautakiwi kutumikia kifungo kisichokuwa na jina wala hukumu. Mimi nitakusaidia, lakini ukitoka hapa potea mbali kabisa. Maana Desmund hakupendi hata kidogo na nina kuhakikishia kuwa ukifa hataumia hata kidogo. Hawapendi waarabu kwa sababu zake za miaka mingi ambazo yeye anaziita sababu za msingi!! Tumejaribu kumshauri lakini hataki kubadili msimamo.” Maelezo ya askari yule yalinichanganya sana, nikabaki kuduwaa. Desmund na umasikini wote ule niliomkuta nao ana kisa gani na wahindi na waarabu. Kumbe tangu siku ya kwanza alikuwa ananichukia!! Nilibaki kuduwaa.

Nikataka kuuliza swali lakini afande Danny akanikata kidomodomo kuwa ule haukuwa wakati wa maswali!
Akanirudisha rumande bila kunieleza jambop jingine la ziada. Baada ya dakika kadhaa nikaletewa chai nzito ya maziwa, nikawagawia rafiki zangu wa wakati ule ndani ya selo. Mimi sikuweza kunywa chochote.
Usiku ambao sikufahamu ni saa ngapi mlango wa mahabusu ukafunguliwa, nikaitwa jina nikaitika. Nikatolewa nje ya ile mahabusu!! Safari hii hakuwa Danny bali askari mwingine tu ambaye sikuwahi kumjua jina lake.

Aliponifikisha nje nikiwa pekupeku vilevile nilikutana na gari ndogo ikinisubiri. Mlango ukafunguliwa nikaingia mle ndani. Gari ikaondolewa!! Taa ya ndani ilipowashwa nikagundua kuwa dereva ni Danny.
Moja kwa moja tukafika mtaa uitwao ‘Kariakoo’ hukohuko Musoma. Hapa ndipo Danny aliongea mara ya kwanza akiniambia chanzo cha mtaa ule kuitwa Kariakoo.
Baada ya dakika chache nyingine tukafika nyumbani kwa Danny.
Vilikuwa ni vyumba viwili vilivyoungana, choo na bafu vilikuwa nje.

Kitu cha kwanza baada ya kufika kwa askari huyu nilitakiwa kuoga, lakini bado sikutakiwa kwenda nje. Aliniletea maji katika ndoo na beseni kubwa akaniambia niogee ndani ya beseni, japo nilikuwa naona aibu nilioga.
“Safisha masikio hayo vizuri binti!!” Danny alinisisitiza kutokea chumba cha pili. Baada ya chakula, nikamsihi Danny anieleze chanzo kidogo tu kwanini Desmund alikuwa akiwachukia watu weupe. Nilitamani sana kujua ili niamini kuwa Desmund yu sahihi ama la!!

“Umechoka sana binti! Kesho siingii kazini, nitakusimulia asubuhi sawa!!” alinijibu huku akipiga mwayo!! Sikuwa na kipingamizi, nikamkubalia. Akanipa gogoro tukapangua viti nikalitandaza chini. Akaniletea mashuka.
“Unajua bila kumshirikisha mama yangu walaah nisingeweza kukutoa kule, mama yangu amelizwa na historia yako Ameumizwa na machungu yote uliyopitia na mwisho amenipa kibali cha kukusaidia, mama yangu ni kila kitu kwangu na mimi ni kila kitu kwake. Mimi mtoto wa ngama.” Alinambia huku akitabasamu.
“Mtoto wa ngama nd’o nini?”
“Mimi ni mtoto pekee na yeye nd’o mama pekee.” Alinijibu tena.
Moyo wangu ulikuwa wa baridi sana katika namna ya utulivu, nilitamani sana kumuona mama huyo awezaye kuumizwa na maisha ya mtu ambaye hajawahi kumuona kamwe. Hakika ilishangaza hali hiyo. Danny akaniambia tutaongea mengi asubuhi. Lakini alipoona sijaridhika akachukua simu yake, akabonyeza namba kadhaa, alivyozungumza kwa kudeka nikajua anaongea na mama yake. Akanipa nami nikamsalimia, sauti ya mama yule ilikuwa ya ukarimu sana. Nikatamani kumuona siku moja.
Sasa niliridhika na nikatabasamu!!!
Nikajitupa katika godoro na baada ya muda kidogo nikasinzia!!

Baadaye nikahisi kama ndoto, kuna kitu kilikuwa kinanipapasa matakoni. Nikawa nahisi ni ndoto nami napuuzia, nikazidi kupapaswa, safari hii nikaunyanyua mkono na kupeleka mahali nilipohisi ule mpapaso!!
Nikakutana na mkono ukinipapasa. Nikataka kupiga kelele nikakutana mara nikazibwa mdomo wangu, nilijua kuwa Danny anataka kunibaka, Danny alikuwa naye anataka kunitendea unyama ambao kama ni kweli basi mama yake mzazi alikuwa anaulaani. Nikajaribu kufurukuta lakini haikuwezekana.
Hakika alikuwa Danny, mara akanisogelea masikioni.
Wanaume!! Wanaume na tamaa!! nililalamika kimya kimya huku nikimtazama.
Kumbe nd’o maana alikuwa anasisitiza nioshe masikio vizuri…shenzi kabisa!!
Ajabu!! Mawazo yangu yalikuwa batili. Danny hakuingiza ulimi wake masikioni mwangu. Badala yake aliongea kwa sauti ya kunong’ona.
“Kuna watu nje…….simama njoo huku.” Sauti yake ilimaanisha. Sasa nikawa kimya, nikajiziba mdomo mwenyewe.
Danny akanipakata hadi katika chumba alichokuwa amelala. Akaniamuru kwa vitendo niingie uvunguni!!
Nikatii!!!
Nikiwa uvunguni nikasikia mlango unagongwa!! Danny akaondoka kuelekea kule mlango ulipogongwa.
“Msichana yupo wapi kijana!!” sauti nzito iliuliza.
“Mi sijui msichana gani kwani?” sauti ya Danny ikajibu.
Hapo halikuulizwa swali kwa muda nikasikia kukurukakara, na mara Danny akasikika analia. Bila shaka alikuwa anatembezewa kipigo kikali.
Walimpiga huku wakianza tena kumuuliza kuhusu msichana ambaye bila shaka ni mimi, lakini ajabu Danny hakuwaambia. Nilikuwa natetemeka, mikojo ikizidi kulowanisha chupi yangu nikiwa chini ya kitanda uvunguni. Nilijua kuwa lazima Danny akizidiwa atanitaja na safari hii nadhani nd’o nilikuwa naenda kufa.
“Nasema nasema….” Nilimsikia Danny akisema huku sauti ikimkwamakwama.
“Yupo wapi msichana sema upesi.”
“Nimemsafirisha kwenda kwao…” alidanganya. Nami uvunguni hali ikiwa tete!!
“Unataka mama yako aKute kichwa chako mlangoni kwake” sauti ilimuuliza.
“Haki ya Mungu nawaambia….nimemsafirisha kwenda Mwanza.” Alisisitiza Danny.
“Kijana yaani umemtoa usiku huu halafu unasema umempeleka Mwanza….unatutania sivyo. Ayubu hebu na wewe mtanie.”
Hapo nikasikia kilio kikuu kutoka kwa Danny kisha kimya kikatanda baada ya kishindo.
“Mpumbavu huyu atakuwa amemuhifadhi kwa mama yake. Watoto wengine kujitafutia vifo maksudi tu!!” kauli hiyo ikanipagawisha. Ina maana Danny amekufa kwa sababu yangu!! Danny amekufa akinitetea, kwanini hakusema tu waniue…Danny alikuwa anategemewa na taifa na mbaya zaidi hakuwa hata na mtoto..niliumia sana. Mara nikawa kimya tena baada ya watu wale kuingia mle chumbani, sijui walichukua nini lakini niliwasikia wakivuruga vitu huku na kule. Kisha wakatoweka!!
Niliendelea kudumu uvunguni kwa nusu saa nyingine kisha nikatoka nikiwa natetemeka sana. Niliamini kuwa nimemuua Danny iwapo nitamkuta akiwa mfu!!!
Haswaa!! Haikuhitaji elimu ya utabibu kutambua kuwa Danny ni mfu, inanilazimu kukueleza mwandishi ili upate picha alivyokuwa lakini vinginevyo sitaki kukumbuka picha ile. Danny alikuwa amepasuliwa kichwa chake bila shaka kwa panga nililolikuta pale chini, nondo ilipenya katika tumbo lake na utumbo ulikuwa nje. Mwandishi niliumia kumtazama Danny niliumia sana, yaani wakamkata na mikono yote miwili…..aaaah!! Danny!! Kwanini sasa ulinisaidia mimi nisiyekuwa na umuhimu!! Na ni akina nani sasa waliokuja kukuua Danny!!....sasa kama laana mama alinipa mimi mbona wapate majanga na hawa wengine eeh!! Mama niambie hivi ulinilaani mimi ama uliwalaani hata wanaohitaji kunisaidia, mama ongea nami sasa eeh!! Sema nami…nife sasa kama ni hivyo…niue nije huko unieleze!!” Hapa Nadia akaanza kuomboleza kwa sauti ya juu. Nikamkabili nikauzungusha mkono wangu begani mwake na kuanza kumbembeleza
“Nadia haya mambo hutokea, binadamu hatufanani licha tu ya kutokamilika ambayo ni kwetu sote lakini kumbuka kila mtu ana roho yake, USILIE NADIA hayo yametokea tayari na yamepita, USILIE NADIA..tena kuhusu mama acha kukufuru, mwache apumzike….” niliendelea kumsihi.
Sasa akatulia kidogo kisha akiwa anabubujikwa machozi bado akaweza kumalizia maelezo yake.
“Kabla ya kulala Danny aliweka simu yake katika chaji kisha akaitia katika mfuko wa suruali yake. Akaitundika palepale sebuleni nilipokuwa nimelala.
Akili yangu ikafanya kazi upesi, nikaamini kuwa wauaji walikuwa wakimtambua Danny vizuri na hata mama yake walikuwa wanamtambua. Sasa kama walikuwa wanamtambua mama yake pia. Bila shaka walikuwa wameenda kumuuliza pia na yeye kama hana jibu wanamua vilevile.
Nilichukua simu ya Danny,nikabofya kitufe cha kupigia.
“La Mujer De Mi Vida” nikajikuta natabasamu mwenyewe, kwa sababu nilikuwa mtazamaji mzuri sana wa tamthilia hivyo nikaelewa maana kuwa alimaanisha ‘Mwanamke wa maisha yangu!’….nikapiga namba hiyo.
Iliita kwa muda mrefu sana kisha ikapokelewa.
“We Danny nawe…nini sasa..” alilalamika mama.
“Mama ni mimi Nadia, kuna tatizo mama jihadhari huko usiwe peke yako kuna watu wabaya mama wanakuja huko..” nilimweleza.
“Unasema?” aliuliza sasa akiwa makini.
Nikataka kumweleza tena simu ikaishiwa salio.
Nikasubiri anipigie!! Hakupiga!!

Nikatazama saa ya ukutani ilikuwa saa nane na nusu usiku!! Nikayacha maiti ya Danny ndani, nikapekua pesa nikazipata kiasi kidogo. Nikaondoka na simu yake.
Majira ya saa tisa usiku nilikuwa nazagaa huku na kule ndani ya mji wa Musoma bila kuelewa ni kitu gani natakiwa kufanya…
Hapa nikakiri kuwa hakika Nadia mimi nilikuwa nimelaaniwa

Mji ukazidi kuwa mchungu!!!........nilifanikiwa kupata salio baadaye kabisa lakini mama hakuwa akipatikana tena…chozi la uchungu likanitoka, nayapigania maisha yangu, naipigania haki yangu, mali zangu za halali, mali nilizozivuna na Desmund kwa sababu tu ya mapenzi yangu kwake!! Leo hii nachukiwa kila pande, nimetengwa na sasa nasababisha vifo, Danny amekufa akinitetea, sijui kuhusu mama mwenye upendo uliopitiliza mama aliyenipenda hata bila kuniona!!...Desmund, Desmund mapenzi yangu yooote niliyokupa umenitenda hivi Desmund….kweli umeamua kunifanya niwe mkimbizi kiasi hiki Desmund ambaye sijawahi hata kukutukana sijawahi kukulaumu Desmund, Des niliyekunyenyekea licha ya kuwa nakuzidi kwa kila kitu…leo unaniita Chokoraa na nisiyefaa katyika jamii, unawatuma watu waniue mimi Desmund!!” kikafuata kilio kikuu huenda kupita vyote, Nadia alilia sana, alilia akiomboleza juu ya kifo cha Danny na kuhusu mama asiyejua kama alikufa ama la!! Lakini Nadia aliamini kuwa walimuua. Nadia alilia kinyakyusa!! Alilia huku akilaani katika namna ya kuimba!!
“Nadia, mimi nipo upende wako na sitakusaliti, ni mimi na wewe tunajua wapi tulipokutana amini kuwa …”


“Shhhhhhh!!!! Wote ninyi ni wale wale..” alinikaripia. Nikatambua kuwa hii ni hasira iliyopitiliza. Nikaamua kumuacha Nadia alie akimaliza apumzike na huenda anaweza kusema nami tena, maana kwa hali aliyokuwanayo angeweza kunipiga hata makofi!!

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom