Jumatano, Machi 11, 2015

Ujumbe wa Mama Maria Nyerere "Sikustushwa kuzushiwa nimefariki dunia."

 
Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, amesema baada ya kupokea taarifa za kuzushiwa amefariki dunia juzi, hakushtushwa na uvumi huo badala yake alifanya sala.
 
Kadhalika, amesema uvumi huo wa kifo chake inawezekana unatokana na vuguvugu la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, pamoja na utandawazi uliopo wa sayansi na teknolojia wa karne ya 21 unaotawaliwa na matumizi ya mitandao ya kijamii.
 
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuwathibitishia Watanzania kuwa bado yu hai na mwenye nguvu.
 
Alisema alipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka kumjulia hali akiwamo Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri, na kwamba alipata usumbufu na kuamua kutokupokea simu za watu wengine.
 
“Wala sikushtushwa na taarifa za uvumi wa kuwa nimefariki, ila nilipokea simu nyingi sana, wengine walikuwa wananisalimia, wengine waliposikia sauti yangu wanakata simu,” alisema Mama Maria.
 
Alisema kuwapo kwa utandawazi umechangia mambo hayo yote na kueleza kuwa unaliongezea taifa hofu na mashaka.
 
“Au kwa kuwa imenitokea mimi ndo mnaona kitu cha ajabu, mi kwangu naona ni kitu cha kawaida kuzushiwa kifo,” alisema.
 
Alisema kupokea taarifa za kuzushiwa kifo si mara ya kwanza kwake kwani hata miaka ya nyuma akiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakitokea Indonesia, walipokea taarifa nyingi za uvumi wa kifo.
 
Juzi mitandao kadhaa ya kijamii iliandika taarifa za uzushi, ikidai kuwa Mama Maria Nyerere amefariki dunia.
 

CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom