Alhamisi, Mei 28, 2015

Ujumbe wa leo kutoka kwa Dk Mengi "Sera ya kuwawezesha Watanzania haitekelezwi"


Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema Tanzania ina sera nzuri ya kuwawezesha Watanzania, wakiwamo vijana kujikwamua katika hali duni za maisha, lakini haitekelezwi.
 
Alisema hayo katika uzinduzi wa programu ya Airtel Fursa, jana jijini Dar es Salaam.
 
Dk. Mengi alisema sera ya kuwezesha wananchi ya mwaka 2004 nchini ni nzuri, lakini inaishia katika maneno majukwaani, vinginevyo ingeweza kuwafikisha mbali Watanzania katika kuboresha maisha yao.
 
“Sera ya kuwawezesha wananchi ipo. Ni nzuri sana. Ingeshughulikiwa kivitendo, wangekuwa mbali. Lakini leo sera ya kuwawezesha wananchi inaishia katika maneno majukwaani,” alisema Dk. Mengi. 
 
 
Aliwataka vijana kufanya kazi kwa bidii na kuwa na ndoto kubwa siyo kwa kutaka kufanana na matajiri walioanza, bali kuwa na malengo zaidi yao.
 
Alisema ili vijana wafanikiwe katika hilo, wanapaswa kuwa na macho yanayoona fursa, kujiamini, kutojiona wadogo, kwani katika umri walionao wanaweza kuwa matajiri. 
 
 Dk. Mengi alisema hakuna aliyezaliwa kuwa wa pili, lakini baadhi ya viongozi wanaona hivyo kwani fursa zinapotokea zinaenda kwa watu wa nje mbali na kuwapo kwa sera hiyo.
 
“Vijana wengi wanashindwa kuanzia wapi. Kinachotakiwa ni kuwa na macho yanayoona fursa. Mahali pa kuanzia ni kuwa na ndoto kubwa...ndoto kubwa huanza na kidogo na kujua unakotaka kwenda,” alisema Dk. Mengi.
 
Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Sunil Colaso, alisema Tanzania ni moja ya nchi inayokua kwa kasi kiuchumi, huku asilimia kubwa ikiwa ni vijana, ambao wanahitaji kuwezeshwa kufikia malengo yao na kuwaandaa kuwa wafanyabiashara wakubwa wa baadaye.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel, Balozi Juma Mwapachu, alimpongeza Dk. Mengi, akisema ni Mtanzania pekee, ambaye yupo mstari wa mbele kutetea maslahi ya wazalendo na kutiwa moyo na vijana, ambao wapo tayari kujiwezesha na kuwezeshwa kufanikisha malengo yao.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom