Jumanne, Julai 28, 2015

ISOME HII KWA UMAKINI "Uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ungeliweza kusubiri"


Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alifanya uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya kumteua aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi kama ilivyo kwa majaji uko chini ya mamlaka ya rais kisheria na kikatiba. Rais hataomba ruhusa kwa mtu yeyote katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba. Ni haki na mamlaka yake kumteua yeyote kwenye nafasi zilizotamkwa hivyo kisheria. Tunajua, tunaheshimu na kutambua kuwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi alioufanya mwishoni mwa wiki na kumuapisha siku hiyo hiyo, ni kwa mujibu wa mamlaka yake.
Pamoja na kutambua mamlaka hayo ya kisheria ya rais, pia pamoja na kutambua kuwa hakuna mwenye uwezo wa kuhoji, lipo jambo ambalo limetusumbua kidogo na kwa kweli limesumbua wadau wengi wa uchaguzi nchini.
Tangu kufanyika kwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi mwishoni mwa wiki, wapo wadau wa aina mbalimbali waliojitokeza kuhoji ulazima wa mabadiliko hayo katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye joto kubwa la maandalizi ya uchaguzi mkuu. Ikumbukwe hoja hapa siyo uwezo wa aliyeteuliwa, ila ni muda.
NEC ilianza kazi ya kuandilisha wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa utambuzi wa alama za mwili (Biometric Voters Registration BVR) Februari mwaka huu. Hadi sasa kazi inaelezwa kukamilika kwa asilimia kubwa katika mikoa yote kasoro Dar es Salaam ambako uandikishaji unaendelea. Mipango ya upatikanaji wa BVR, ratiba ya kuandikisha na hata zabuni mbalimbali zilikwisha kutangazwa na kutolewa kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi mkuu. Yote hayo yamefanyika chini ya Mkurugenzi aliyeondolewa. 

Kwa maneno mengine maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa zaidi ya asilimia 70 yamefanywa chini ya uongozi wa Mkurugenzi anayeondoka. Tunajua, uchgaguzi ni mchakato. Mkurugenzi ambaye ameteuliwa kuwa jaji ameshiriki katika uandikishaji wa wapigakura kwa zaidi ya asilimia 90; ameshiriki kupanga ununuzi wa vifaa na vitendea kazi vingine kwa zaidi ya asilimia 90; atakuwa ndiye mtu wa katikati kabisa wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa maana ya kusimamia wataalam wote wa uchaguzi. Kwa kifupi ndiye mtendaji mkuu wa mambo yote yanayohusu uchaguzi.
Katika mazingira ya namna hiyo, uamuzi wa kufanya mabadiliko ikiwa imebakia takribani miezi mitatu tu wananchi wapige kura ya kuwachagua madiwani, wabunge na rais, kwa kweli inaibua shaka kubwa. Shaka hii ni kwa nini mabadiliko dakika hizi za majeruhi? Je, uteuzi huu usingeliweza kusubiri walau aliyekwisha kuanza kufanya kazi hii muhimu na nyeti kwa taifa aikamilishe?
Tunajua Mkurugenzi aliyeondolewa siyo kwa sababu ya kushindwa kumudu majukumu yake. Ingelikuwa ndivyo, hasingepandishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa maoni yetu utendaji wake ulitosheleza aliyotakiwa kutimiza, kwa maana hiyo kuondolewa kwake kungeliweza tu kusubiri akamilishe kazi ambayo alikuwa amekwisha kuianza, yaani mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Ni dhahiri kumekuwa na madai na malalamiko mengi juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kumekuwa na maswali mengi juu ya mfumo wa BVR, kumekuwa na na hoja juu ya NEC kutokupatiwa rasilimali fedha kwa wakati na ndiyo maana leo hii miezi mitatu kabla ya wananchi kupiga kura bado dafrati la wapigakura halijakamilika. Wananchi na wadau wa uchaguzi wamekuwa wakijiuliza hivi hali hii ni makusudi au kuna njama ndani yake. Hakuna majibu juu ya hoja hizi.
Wananchi wamekuwa wakijiuliza ilikuwaje kwa mfano mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 daftari la wapigakura lilikuwa limekwisha kukamilika, lakini mwaka huu mambo yamekuwa ni kinyume kabisa? Swali hili limekuwa likisumbua wengi siyo kwa sababu nyingine yoyote, ila ni kutokana na kutokufurahiswa na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi kwa ujumla wake. 
Tunafikiri pamoja na ukweli kwamba uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete kwa kumuondoa Mkurugenzi wa Uchaguzi na kumweka mwingine ni halali kisheria, katika mazingira ya sasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu maswali mengi zaidi yanaibuka juu ya uamuzi huo wa lalasalama. Ni kwa maana hiyo, sheria pekee haitoshi katika kufanya maamuzi, kwani mazingira, nyakati na hata hisia za wananchi ni muhimu pia kuzingatiwa ili kuendeleza hali ya amani, kuaminiana na kuheshimiana iliyodumu katika taifa hili tangu uhuru wake ili pia kuujengea uchaguzi mkuu uhalali pasi na shaka yoyote. 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom