Ijumaa, Julai 10, 2015

Ujumbe wa leo Kikwete asema "Baadhi ya viongozi CCM ni wezi"


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho siyo waaminifu na wamejinufaisha na mali za chama hicho hali ambayo imekigeuza kuwa ombamba kwa wafanyabiashara.
“Msitembee tu kwa matajiri kwenda kuombaomba, wanawadhalilisha bure. Inashangaza kuona chama hiki biashara yake kubwa ni kulaza magari ya watu na sijui mapato yake yanakwenda wapi…Tunazo rasilimali, tunayo mitaji, lakini hatuzitumii rasilimali hizo kupata mapato,”alisema Rais Kikwete.

Akifungua jengo jipya la mikutano la kimataifa la chama hicho, Dodoma Convention Centre, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa kwake na ubadhirifu unaofanywa na viongozi hao, ambao wameanza kugawana viwanja, kujenga majumba, wengine kujimilikisha rasilimali za chama hicho na wengine kuweka mapato ya rasilimali zake mfukoni.
Kufuatia hali hiyo, Rais Kikwete amemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana, kuunda kitengo maalum cha ukaguzi wa mali za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kumteua Mkaguzi Mkuu atakayezunguka nchi nzima kufanya uhakiki wa mali zake na kutoa taarifa kwa uongozi wa juu.
Alisema CCM imekuwa ikitumia sera ya ujamaa na kujitegemea, lakini hivi sasa wameipotezea kwa kutegemea wafadhili na wakati mwingine chama hicho kimejikuta kikienda kuchukua fedha za moto (rushwa), ambazo zinakilazimisha kutumia muda mwingi kujisafisha.
“Kama ni mtaji ni mtaji mfu, lazima tuitoe ile ‘dead capital’ iwe hai; sijui tumekutwa na nini au viongozi wetu wana maarifa mafupi. Kazi ya kujipanga foleni, kila siku ya kukimbilia kwa matajiri itaisha lini, wanawadhalilisha tu, mnapata aibu, sijui mtaondokana nao lini?” alihoji.
Alidai kwamba Jiji la Dar es Salaam peke yake, CCM ina viwanja zaidi ya 420, lakini haviendelezwi na matokeo yake vimegeuka karakana ya biashara ya kulaza magari.
“Watu wote pale wanaangusha magorofa na wanapata mapato. Viwanja vile biashara kubwa ni ya kulaza magari, mapato yenyewe ya kulaza magari sijui hata anachukua nani, lini tutazinduka kwenye usingizi huu…Tambueni kwamba ardhi ile ni mtaji,”alisisitiza Rais Kikwete.
Imeandikwa Godfrey Mushi,Augusta Njoji, Editha Majura na Salome Kitomari
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom