Alhamisi, Februari 25, 2016

Ujambazi ulioibuka upya Dar unatisha, udhibitiwe sasa.





Matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yameibuka kwa kasi jijini Dar es Dar es Salaam na kutishia usalama wa raia na mali zao.Kuna matukio kadhaa yaliyotokea jijini humo ya uporaji wa kutumia silaha sambamba na kujeruhi watu.

Liko tukio ambalo watu wanaodaiwa kuwa majambazi walivamia maduka matano katika mtaa wa Kimara Temboni, wilayani Kinondoni na kupora fedha na mali mbalimbali pamoja na kujehuri watu wawili kwa risasi.
Kadhalika, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limemkamata mwanamke anayedaiwa kuwa kinara wa kusuka mipango ya  kufanikisha wizi wa fedha za wateja katika benki mbalimbali.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na watuhumiwa wengine wanne ambao walikuwa wakishirikiana kufanikisha wizi huo.
Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakifanya unyang’anyi wa kutumia silaha, walikamatwa Alhamis iliyopita eneo la Buguruni na kuwa
mwanamke huyo amekuwa akienda benki na kukaa humo kama mteja kisha kuangalia mteja anayetoa kiasi kikubwa cha fedha na kuwasiliana na watuhumiwa wenzake ili kufanikisha uporaji.
Jeshi hilo pia lilisema mwishoni mwa wiki iliyopita, lilikamata silaha mbili aina ya SMG iliyokatwa mtutu ikiwa na risasi 24 kwenye magazine pamoja na bastola aina ya Browning. 
SMG ilipatikana baada ya kukamatwa watu wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi, waliokuwa wakikimbia baada ya kufanya uporaji wa Sh. milioni 12.

Matukio hayo na mengine ambayo hatukuyataja hapa yanathibitisha kuwa ujambazi unaibuka upya na kwa kasi ya kutisha na kutoa salamu kwa vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi kwamba linawajibika kujitathmini na kujipanga upya kikabiliano navyo kwa kuwa ulinzi wa usalama na mali zao ndilo jukumu lake la msingi.

Katika miaka ya karibuni, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa limetulia kutokana na kutokuwapo na matukio mengi ya ujambazi tena mkubwa wa kutumia silaha tofauti na hali ilivyokuwa mwaka 2006 ambacho kilikuwa kupindi cha mpito kutoka uongozi wa awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa na wa awamu ya nne ya Jakaya Kikwete.
Matukio kadhaa ya ujambazi yanayotokea sasa mbali na tuliyoyataja, yanatisha. Kila uchao watu wanaporwa fedha katika maeneo mbalimbali na wengine kujeruhiwa au kuuawa, wengi wao ni wale wanaotoka kuzichukua katika benki na kwenye ATM za benki.
Kwa kuwa matukio ya ujambazi yameshamiri kipindi hiki ambacho Wizara ya Mambo ya Ndani imesainiana makubaliano na Jeshi la Polisi na Jeshi hilo kusainiana na makamanda wa mikoa kuhusu kudhibiti uhalifu, ni matumaini yetu kuwa mpango huo utatekelezwa kwa tija na ufanisi kwa kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, alisainiana mkatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu, naye akasainiana na makamanda wa polisi wa mikoa wakati wa kupokea ripoti yenye maoni ya wadau kuhusiana na namna ya kudhibiti uhalifu kwa lengo la kulinda usalama wa raia na mali zao.
Mpango huo ambao ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), utakapozinduliwa na utekelezaji wake kuanzia Mkoa wa kipolisi  Kinondoni na baadaye mikoa yote, bila shaka utadhibiti na kupunguza uhalifu. Ni matarajio yatu kwamba utaivusha nchi isirudi katika hali ya mwaka 2006, bali wananchi wote waishi maisha ya usalama na mali zao.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom