Pages

Jumatatu, Novemba 19, 2012

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SURA YA ......4.......



MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
ILIPOISHIA “Mmh jamani huna hela ndogo kaka au kuna kitu kingine unataka kununua dukani nikakuchukulie, asubuhi hii chenchi zinasumbua kweli.” Alisema Julieth kwa kulalamika. “Usijali Julieth nipe hizo chapati na fedha inayobaki ni zawadi yako.” Alijibu John. “Mh we kaka, hela yote hii nibaki nayo kuna usalama kweli? Hapana kaka ngoja nikutafutie tu chenchi.” Alisema Julieth huku akinyanyuka kwenda dukani. USIKOSE SURA YA .....4.....

INAPOENDELEA
“Julieth usiogope mimi sina nia mbaya na wewe chukua tu hiyo hela itakusaidia usijali.” Alitamka John huku akimzuia kuondoka. Julieth aliamua kukaa chini na kumsikiliza John hatimaye wakafahamiana. John alikuwa ni mkazi wa Mwanza na alikuwa ni mfanyabiashara wa samaki. Julieth alimweleza hali halisi ya maisha yao. Baada ya kufahamiana kwa siku kadhaa walianza kuwa marafiki na baadaye John alimtaka Julieth awe mpenzi wake. Mwanzoni Julieth alikataa sana kuhusu urafiki wa kimapenzi na John. 

Lakini baadaye alikubali wakawa marafiki. siku moja Julieth akiwa amekaa nje ya nyumba yao John alipita pale na kufanya maongezi na Julieth. “Julieth tumekuwa marafiki kwa muda wa wiki tatu sasa naona nikwambie ukweli. Kutoka siku ya kwanza nilipokuona nilitamani sana uwe mpenzi wangu. Naomba unipe nafasi ndani ya moyo wako. Nakupenda Julieth zaidi ya urafiki tulionao.” John alimwambia Julieth.

“Haiwezekani John! Mimi ni masikini sana unaiona familia yetu inanitegemea sana mimi, halafu nianze tena mapenzi! Hapana! Tena sitaki! Wewe tafuta tu mwanamke atakayekufaa anayeendana na wewe.” Alikataa Julieth kwa msisitizo mkubwa. “Sikiliza nikwambie Julieth, mimi na wewe tukiwa pamoja hata familia
yako itakuwa yangu pia, tutasaidiana sana katika maisha. Mama yako atakuwa hana matatizo tena. 


Wewe nipe nafasi amini hutajuta maishani kwa kunikubali mimi.” John aliendelea kubembeleza. Julieth alinyamaza kimya kwa muda huku akichimba chini na kidole gumba cha mguu wa kushoto. “Huyu kaka tumefahamiana kwa muda mfupi sana lakini ni mtu mwenye heshima na amekuwa karibu na mimi kwa wakati wote. Lakini zaidi ya yote hata mimi pia nimempenda. Nikimkubali naamni hata mama atampenda pia. Lakini je, mama atakubali niolewe katika umri huu?”Aliwaza Julieth huku John akimwangalia kwa macho na uso wa kumtamani.

“Nimekubali ombi lako.” Julieth hatimaye alikubali huku akiendelea kuchimba chini na kuangalia pembeni akijaribu kuyakwepa macho ya John. “Nimefurahi sana Julieth nakupenda sana tutakwenda kuishi wote Mwanza.” Aliongea John huku akimkumbatia, kumbusu na kumnyanyua Julieth juu kama mtoto mdogo.
“Wewe! Mimi niende Mwanza nimwache mama na nani? Hapana kwanza inabidi nikupeleke ukamwone mama umwambie lakini hilo la kwenda Mwanza sahau.” Julieth Alimaka na Kuhamaki.

Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa wote na bila kupoteza muda wote wawili walianza safari ya kwenda nyumbani kwa kina Julieth ili kuonana na mama. Walipofika walimkuta mama Julieth akiwa amekaa sebuleni. Julieth aliongoza kuingia ndani huku akifuatiwa na John. Julieth alimweleza mama yake juu ya uhusiano wao na John.

Mama Julieth alichukia sana kusikia eti Julieth kapata rafiki wa kumwoa. Kimsingi mama yake hakuwa tayari kumruhusu Julieth kuolewa katika umri mdogo. Vilevile, mama yake Julieth alikuwa bado ana ndoto ya kwamba Julieth atasoma hadi chuo kikuu. “Julieth usijidanganye kabisa umri wako bado ni mdogo kuhimili mikikimikiki ya ndoa. Lakini pia mimi bado napenda ukasome ili ndoto yako ya kuwa daktari itimie.”Alitahadharisha mama Julieth juu ya urafiki alionao na John.

“Hapana mama kama ni kusoma atasoma tu, na kuhusu kwamba Julieth ana umri mdogo si tatizo kwani kuna wengine wanaolewa wakiwa na umri chini ya umri wa Julieth, lakini wanahimili vishindo vya maisha ya ndoa.” Alifafanua zaidi John. “Na wewe mwenyewe muolewaji unasemaji mbona umenyamaza kimya?” Aliuliza mama Julieth. “Mimi mama nipo tayari kuolewa naye kwani kwa kipindi cha wiki tatu tangu nimfahamu ameonyesha moyo wa kutusaidia.” Alijibu Julieth huku akimwangalia John kwa macho ya kusisitiza.

“Sawa! Kwa sababu yeye ameridhia hata nikimkatalia ni kazi bure. Ila nawaomba mfuate taratibu zote za kimila na kufunga ndoa rasmi ili mpate baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa wazazi pia.” Alishauri mama Julieth. USIKOSE SURA YA ......5........

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Unakaribishwa kutoa maoni yako.