ILIPOISHIA“Mimi mama nipo tayari kuolewa naye kwani kwa kipindi cha wiki tatu tangu nimfahamu ameonyesha moyo wa kutusaidia.” Alijibu Julieth huku akimwangalia John kwa macho ya kusisitiza.
“Sawa! Kwa sababu yeye ameridhia hata nikimkatalia ni kazi bure. Ila nawaomba mfuate taratibu zote za kimila na kufunga ndoa rasmi ili mpate baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa wazazi pia.” Alishauri mama Julieth. USIKOSE SURA YA ......5........
INAPOENDELEA
“Huo ni
ushauri mzuri mama, lakini namwomba niende naye Mwanza nikamtambulishe
kwa wazazi wangu halafu atarudi ili tufanye taratibu hizo kama
ulivyoshauri.” Aliomba John. “Kumbe
kwenu ni Mwanza?” Aliuliza Mama Julieth. “Ndiyo
mama.” Alijibu John. “Na je
maisha yenu yatakuwa wapi?” Aliuliza mama Julieth. “Baada ya
taratibu zote za kufunga ndoa kukamilika tutakwenda kuisha Mwanza.”
Alijibu John. “Sasa baba
kama mtaishi mbali na mimi nani atanihudumia, maana Julieth ndiyo
alikuwa akinisaidia.
Mimi mwenyewe hali yangu si nzuri sana naumwa
mara kwa mara na Julieth anajua.” Alihoji mama Julieth. “Hapana
mama usijali mimi na mwenzangu tumekwisha jipanga namna ya
kukusaidia. Kwanza nataka uondoke hapa uhamie kwenye nyumba nzuri
nitakayokupangishia. Pia nitakuachia pesa ili uweke msichana wa kazi
ambaye atakusaidia kazi mbalimbali. Kuhusu pesa isiwe tatizo kabisa mambo yote
yatakaa sawa.” John aliongea na kuahidi kwa kujiamini huku akimwangalia
Julieth ambaye alikuwa akitabasamu muda wote wa maongezi.
“Sawa mimi
nashukuru kama mmejipanga hivyo. Mungu akubariki sana mimi sina
kipingamizi tena alimradi mmependana na kufuata taratibu za kufunga
ndoa ili mpate baraka za Mungu. Pia ninaomba mkishaanza maisha
muwe mnakuja huku kutusalimia mara kwa mara.” Mama Julieth alishauri
huku akimkazia macho Julieth na baadaye John. “Hilo
halina tatizo kabisa mama hapa ni nyumbani tutakuja bila shaka kwani
nyumbani ni nyumbani, hata hivyo kwa sasa akishawaona wazazi wangu tu
atarudi ili kukamilisha mambo ya ndoa kama ulivyoshauri.” Alijibu
John.
********************************************************************
Mikakati
ya kuondoka ikaanza, mama Julieth akahamishwa kutoka nyumba
waliyokuwa wanakaa na kuhamia katika nyumba kubwa ambayo ilikuwa na
kila kitu ndani. Kisha alitafutwa msichana kwa ajili ya kazi za ndani.
Halafu nje ya nyumba alimfungulia duka dogo ambalo mama Julieth
alikuwa akiuza bidhaa ndogondogo kama sabuni, sukari, unga na vinginevyo.
Mwisho John alimnunulia mama Julieth simu kwa ajili ya mawasiliano
ili kukitokea tatizo lolote atoe taarifa mapema. Mama Julieth alifurahi
sana.
Siku ya
kuondoka ilikaribia Julieth alionekana mwenye huzuni kwa ajili ya kumwacha mama
yake. Mama Julieth yeye alikuwa katika hali ya kawaida akisisitiza
kuwa Julieth akumbuke yote aliyomwambia. Safari ya
kwenda Mwanza ilianza hatimaye walifika salama na kwenda moja kwa
moja nyumbani kwa John, maeneo ya Igoma. Julieth alishangaa sana kuona
nyumba aliyokuwa akiishi John ilivyokuwa kubwa, nzuri na ya kifahari
iliyojaa vitu vya thamani.
“Mpenzi
nyumba yako ni nzuri sana, yaani nyumba yote hii unakaa mwenyewe?”
Aliuliza Julieth. “Hapa ni
kwako mama, nilikuwa nakaa mwenyewe na vijana wa kazi lakini sasa nina
mke aitwaye Julieth naamini nyumba hii itakuwa nzuri zaidi hasa ikiwa na
watoto na mke mzuri kama wewe.” John alijibu kwa kiburi na majivuno. Julieth
alitabasamu huku akizunguka huku na kule akishangaa uzuri wa nyumba ile
ya kifahari. John alipeleka mizigo chumbani na kumwelekeza kila kitu
kilichomo na matumizi yake.
John na
Julieth waliishi maisha ya raha na furaha. John alimtembeza Julieth sehemu
mbalimbali ili kumwonyesha utofauti wa mazingira ya Mwanza na Arusha.
Katika kuishi kwake Arusha Julieth alikuwa hajawahi kufika Mwanza,
aliupenda sana mji wa Mwanza hususan samaki aina ya sato na sangara
wanaopatikana katika mji huo ambao huvuliwa katika Ziwa la Viktoria.
Kwa ujumla Julieth alifurahia sana maisha yake mapya. Baada ya
wiki moja kupita Julieth alitaka kuwafahamu wazazi wa John, lengo kuu
la safari yao ilikuwa kwanza kwenda kuwafahamu wakwe zake.
“Vipi
mpenzi lini tutakwenda nikawafahamu wakwe?” Aliuliza Julieth. “Usijali
mpenzi wangu tutakwenda tu kwani una wasiwasi gani, si upo na mimi kuna
kazi tu zimenibana kwa sasa ila tutapanga mapema wiki ijayo.” Alimjibu
John.
“Sawa John
hakuna tatizo nilikuwa nataka kujua ili nimjulishe mama Arusha.”
Alijibu Julieth. Mazungumzo
yaliendelea baadaye walichoka na kwenda kupumzika.
*****Baada
ya mwezi mmoja****
Wazazi wa
John walikuwa wakiishi Bukoba na siyo Mwanza kama John alivyosema
akiwa Arusha. Kila mara Julieth alipomwambia suala la kwenda kuwafahamu
wazazi wa John aliambiwa kuwa watakwenda asiwe na wasiwasi.
Baadaye kutokana na raha alizokuwa anazipata Julieth, alijisahau kabisa
kama hajafunga ndoa na John. Mama yake Julieth alipokuwa akimpigia
simu na kumuuliza vipi kuhusu ndoa alimjibu hakuna tatizo mipango
inaendelea vizuri. Kumbe ilikuwa ni uongo wao walikuwa wakijirusha
na kusahau mambo ya ndoa na taratibu nyingine za kimila.
********Baada
ya miezi mitano**************
Baada ya
mapenzi na raha kushamiri, Julieth alipata ujauzito ambao hakugundua
kama ana mimba. Aligundua baada ya kwenda hospitali kupima
afya yake kutokana na kutojisikia vizuri ikiwa ni pamoja na kusikia kichefuchefu.
Suala la mimba lilimfurahisha sana Julieth. “Huu ndio
wakati mwafaka wa kufunga ndoa, najua John atafurahi sana nikimzalia
mtoto. Akija leo nitamwambia tufanye haraka tufunge ndoa.” Aliwaza
Julieth. USIKOSE SURA YA ......7.........
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.