ILIPOISHIA
Baada ya siku kadhaa kupita hakukuwa na mabadiliko yoyote ila matatizo yalizidi kila siku ilikuwa ni ugomvi. Miezi kadhaa ilipita bila Julieth kuwa na mawasiliano na wazazi wake kwani alikuwa hana simu, hivyo ilikuwa vigumu kujua hata wazazi wake walikuwa wanaendeleaje. Kwa kweli maisha yalikuwa magumu sana. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wamiezi saba lakini John alikuwa hajali.
INAPOENDELEA
Siku moja
John alimwambia Julieth kwamba siku zake za kuondoka zinahesabika.
Ilikuwa ni yapata kama saa mbili usiku wakati Julieth akiandaa
chakula cha jioni. John alifika na kumwita Julieth. “We mwehu
si ulikuwa unataka uende nyumbani kwenu sasa muda wako umefika
unaweza ukaondoka muda wowote nakupa wiki mbili tu.” Aliongea
John kwa maneno ya kutukana. “Lakini si
ulisema tutakwenda wote? Hebu niangalie na hali hii kweli ndiyo niende
nyumbani mwenyewe. Afadhali nisubiri hadi nijifungue ndiyo niende
nyumbani.
“Wewe una kichaa nini hivi hapa ni kwako? Tena sikiliza
kwa makini nataka uondoke uende popote unapopajua hata ukifa shauri
yako. Kwanza hata hiyo mimba si yangu. Kwa hadhi yangu siwezi kuwa na
mke kama wewe. Kwa taarifa yako mimi nina mke na mtoto na siku si
nyingi anarudi sitaki aje akutane na kinyago kama wewe humu ndani.”
John alitukana na kuongea kwa kebehi na dharau. Akiwa
amejiinamia Julieth alisikiliza yale maneno na kuhisi kama ni ndoto.
Kabla
hajazungumza lolote John aliondoka na kumwacha akiwa na mawazo
sana na kushindwa kuelewa mwenziwe ana matatizo gani. Baada ya
wiki moja kupita tokea John alalame na kutukana wakati Julieth akiwa
amekaa sebuleni mara John aliingia na kupita pale sebuleni kama hajamwona
kisha aliingia ndani na kurudi na mabegi ya nguo na kumtupia huku
akimfukuza Julieth aondoke na kwenda kwao.
“Kuanzia
muda huu ninavyoongea sitaki kukuona katika nyumba yangu tena. Kama
kuna kitu nimesahau kukitoa ukakitoe sasa hivi sitaki kukuona hapa mke
wangu karibu atarudi.” Aliongea John kama mtu aliyepagawa. “Jamani
mimi nitakwenda wapi na hii mimba? John uliniambia unanipenda
kweli leo unanifanyia hivi? Nakuomba kama nimekukosea unisamehe
unajua hali halisi ya maisha yangu nitafanyaje mimi kama unanifukuza?
Je, maisha yangu yatakuwaje? Aliuliza Julieth kwa uchungu huku
machozi yakimtoka kama mtoto mdogo.
“Mbona
siku uliponitoa kwetu ulionyesha kunipenda sana, halafu ukamwambia
na mama….” Kabla Julieth hajamaliza kuongea machozi yalimtiririka
mashavuni kama vile kamwagiwa maji kichwani. “Mimi
nikupende wewe! Mjinga sana, nimekwambia ondoka kabla sijakuua.John
”Alimfukuza Julieth na kutupa mabegi yake nje. Ilikuwa jioni
yapata saa
kumi na moja, Julieth alilia sana huku akiwa hajui atakwenda wapi.
Aliondoka na kwenda nyumba ya jirani kidogo ambapo alikuwa anakaa
rafiki yake aliyeitwa mama Janeth na kumsimulia mkasa mzima.
“Pole sana
rafiki yangu wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo, mimi nitakusaidia
ulale leo, halafu kesho uende tu nyumbani kwenu Arusha. Nitakupa
hela kidogo.” Mama Janeth alimwonea huruma na kumfariji. “Asante
sana mama Janeth kwani hapa nilipo sijui ningefanyaje.” Alishukuru
sana Julieth na kwenda kulala baada ya kuonyeshwa sehemu ya
kupumzika. Usiku
akiwa amelala mara akaanza kuumwa uchungu wa kujifungua, wakati huo
mimba ilikuwa na umri wa miezi saba. Mama Janeth alimkimbiza
Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ambako alipelekwa moja kwa moja
chumba cha kujifungulia.
Muuguzi wa zamu alimwambia mama Janeth
aende nyumbani na awahi kuleta chai asubuhi. Julieth
alijifungua salama watoto mapacha mmoja wa kike na mwingine wa kiume.
Mama Janethi alipokuja asubuhi alifurahi sana kuona mgonjwa wake
amepata watoto mapacha bila matatizo, aliwashukuru sana wauguzi na kuwapa
shilingi elfu ishirini kama shukurani na kwa furaha aliyokuwa nayo.
Julieth alijifungua kabla ya miezi tisa kutokana na misukosuko aliyokumbana
nayo. Hata hivyo Julieth ilibidi aendelee kukaa pale hospitalini
kwa muda wa miezi miwili huku akipewa huduma zote na mama
Janeth.
Baada ya
miezi miwili Julieth aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alikaa kwa mama
Janeth kwa muda wa mwezi mmoja akiwa anamuhudumia ili apone vizuri.
Hali ya Julieth pamoja na watoto iliendelea kuwa nzuri. Siku moja
wakiwa wamekaa sebuleni baada ya kula chakula cha jioni mama
Janeth na Julieth walikuwa na maongezi kuhusu John. “Hivi
Julieth, kwa nini usirudi kwa John labda akikuona na watoto atakupokea.”
Alishauri mama Janeth. “Mama
Janeth John amebadilika sana si yule wa siku zile, amekuwa mkali
kama mbogo
aliyejeruhiwa. Ninaogopa sana asijeniumiza na pengine hata kuua
wanangu.” Julieth alijibu.
“Hapana
jaribu kwenda na watoto kwani anajua kuwa umeshajifungua ingawa
anaona aibu ataanza vipi kuja kuwaona.” Mama Janeth aliendelea kutoa
ushauri. “Sawa!
Hebu nijaribu kwenda na watoto kwani kama unavyosema akiwaona
watoto pengine atapunguza hasira.” Alijibu Julieth. Huku akiwa
amewabeba watoto wake aliondoka kuelekea kwa John.
Alipofika
alikuwa na wasiwasi mkubwa akifikiria jinsi atakavyokabiliana na uso wa
John baada ya kuachana kwa takribani miezi mitatu. Alisogea jirani,
akagonga taratibu na kusubiri afunguliwe. Mara mlango ulifungulwa na
mwanamke mwenye uso wa kujiamini kisha akaanza kumsemesha Julieth: “Habari za
leo dada! Alisalimia. “Salama
dada yangu! Habari za hapa?” Alijibu na kuuliza Julieth. “Karibu
dada nikusaidie nini?” Aliuliza bila hata kujibu swali aliloulizwa.Julieth
alishtuka sana na kuingiwa na hofu kubwa kumwona yule mwanamke
aliyefungua mlango. USIKOSE SURA YA 9...........
hi adela, hadithi imekuwa tamu kweli hadi sikutamani iishe jamani naisubiri kwa hamu ili nijue mwisho wa Julieth, asante sana usitukatesha jamani
JibuFuta