ILIPOISHIA “Wewe!
Wewe! John! Muogope Mungu ulinichukua kwetu Arusha na kunidanganya
kuwa unanipenda leo hii unaniona sifai. Eti kichaa! Baada ya
kunidanganya na kuniharibia maisha yangu leo unaniona kichaa. Ungeniambia
ukweli haya yote yasingetokea, kumbe ulikuwa una mke na mtoto.
Sawa! mimi nitaondoka ila Mungu ndiye atakayenisaidia nakutakia maisha
mema.” Alifoka Julieth kwa mfululizo bila hata kumpa John fursa ya kujibu
huku akibubujika machozi.USIKOSE SURA YA ...10......
INAPOENDELEA
Wakati akizungumza maneno hayo mama Philipo alibaki
kimya akitafakari kisha akaungana na John kumshambulia Julieth; “Hebu tuondolee kilio hapa ufanye uhuni wako upate
mimba halafu uje hapa na vitoto vyako nani akupokee, kamtafute baba wa watoto
wako. Unataka kunigombanisha na mume wangu toka mjinga wewe.” Alitamka mama
Philipo huku akimsukumiza Julieth na watoto wake nje. Julieth alitoka akiwa
analia sana.
Julieth alirudi kwa mama Janeth na kumwelezea yote
aliyokutana nayo. Mama Janeth alisikitika sana na hakuwa na namna nyingine ya
kumsaidia zaidi ya kumpa nauli na pesa kidogo za matumizi ili arudi kwao
Arusha; “Julieth wewe nenda tu nyumbani ukamweleze mama yako
hali halisi kwani ukiendelea kuishi hapa utateseka sana na ipo siku huyo John
atakutafuta. Nakutakia kila la heri Mungu atakusaidia utawalea watoto wako
vizuri.” Mama Janeth alishauri.
“Nashukuru
sana mama Janeth kwa msaada wako, tangu siku nilipoumwa uchungu hadi sasa. Umekuwa
msaada mkubwa sana kwangu. Mimi nitakwenda nyumbani na hata huko nyumbani sijui
wanaendeleaje kwani sijawasiliana nao kwa muda mrefu. Kuna siku nilimpigia mama
simu ikawa haipatikani sijui wana hali gani.” Mama Janeth akampa simu ajaribu
kumpigia tena mama yake lakini haikupatikana. Julieth aliwaza
moyoni mwake; “Jamani mama atakuwa ana matatizo gain? Labda simu
itakuwa imepotea au imeharibika.”
“Julieth
unaondoka watoto hatujawapa majina, mimi ningependa huyu wa kiume aitwe
Dominiki na huyu wa kike aitwe Domina au unasemaje.” “Sawa hakuna shaka ni majina mazuri najisikia fahari
nakufarijika sana kwa wewe kuwapa majina watoto wangu kwani bila wewe pengine
wasingekuwepo.” Alijibu Julieth huku akiwa na mawazo mengi. Waliendelea na mazungumzo wakala chakula cha usiku na
muda wa kulala ulipofika wote walikwenda kupumzika ili kesho yake asubuhi na
mapema Julieth aanze safari ya kwenda Arusha.
Kesho yake asubuhi na mapema saa kumi na moja Julieth
alijiandaa na kusindikizwa na mama Janeth hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi.
Basi liitwalo Jordan liliwasili, waliagana harakaharaka na safari ilianza
kuelekea Arusha.
Akiwa kwenye
basi alikuwa amekaa karibu na mama mmoja ambaye alimsaidia kumshika mtoto
mmoja. Safari ilianza huku Julieth akiwa na mawazo mengi moyoni mwake;
“Nikifika sijui nitaanzaje kumweleza mama. Kwa
matatizo yake ya moyo (shinikizo la damu) sijui atalipokeaje swala hili.”
Aliendelea kuwaza huku gari likichanja mbuga.
Safari iliendelea hatimaye walifika Arusha saa kumi
na mbili za jioni. Julieth alipoteremka tu alianza kuangalia huku na kule
akishangaa mabadiliko ya mji ule kama mgeni. Alichukua teksi na kwenda moja kwa
moja nyumbani kwao mtaa wa Kaloleni katika nyumba aliyomwacha mama yake. Wakati
anamlipa dereva teksi, mara dada mmoja aliyetokea nyuma yake akamwita kwa
mshangao;
“He! Julieth! Julieth! Umerudi Julieth!” Akamkumbatia
yeye na watoto wake pamoja.
“Jamani za siku nyingi.” Aliendelea kumsemesha
Julieth. Mwanzo Julieth hakumtambua lakini alivyozidi kumwangalia akamkumbuka.
“Oh! Kumbe Zubeda! Mambo vipi rafiki yangu?
Nimefurahi sana kukuona habari za hapa?” Zubeda alikuwa ni rafiki yake Julieth,
kwani walikuwa wakiuza chapati pamoja wakati Julieth akiwa Arusha. Domina alianza kulia, haraka Zubeda alimchukua
Dominiki ili Julieth amnyonyeshe Domina. USIKOSE SURA YA 11
Mmh! Story zako zinanoga Adela . Mungu akujaalie afya njema na akupe maisha marefu inshallah.
JibuFutaJamani I wish ningepata Kbs kitabu vile hadithi ilivyo nzr! Bless u swt hrt.xxx
JibuFutaASANTENI KWA KUENDELEA KUWA NAMI
JibuFutaASANTENI KWA KUENDELEA KUWA NAMI
JibuFuta