Pages

Jumatatu, Agosti 12, 2013

SIMULIZI FUPI "AKUFUKUZAYE AKUAMBII TOKA"


SIMULIZI FUPI_ AKUFUKUZAYE AKUAMBII TOKA
MTUNZI_ADELA DALLY KAVISHE


"Mbona umepauka sana, au haujapaka mafuta, mmmh halafu unanenepa sana siku hizi" Nilimtizama Ashura na kusema "Mbona mimi najiona nipo kawaida na pia nimepaka mafuta." Huku akicheka kwa dharau Ashura aliingia ndani na kuniacha nikiwa nimesimama kibarazani. Nilijiuliza maswali mengi kwanini Ashura ananicheka nilijitizama huku nikihisi labda nina kasoro yoyote katika mwili wangu lakini sikuiona. Basi nilimpuuza na kuendelea na safari yangu.


Mimi ni mzaliwa wa Morogoro katika familia ya watoto watatu, Baada ya kumaliza kidato cha sita nilipata nafasi ya kuendelea na elimu ya chuo kikuu Dar es salaam, Kutokana na hali halisi ya maisha ya nyumbani nilipotokea wazazi wangu walikuwa hawana uwezo, hivyo ilinibidi nimuombe rafiki yangu Ashura anisaidie hifadhi katika chumba alichokuwa amepanga karibu na maeneo ya chuo. Ashura alinikubalia na hivyo nilipata sehemu ya kuishi bila ya kutumia gharama yoyote.


Maisha yetu yalikuwa mazuri kwani tulipendana sana mimi na rafiki yangu Ashura, kiasi kwamba pale shuleni watu walikuwa wakituita mapacha, kwani mara nyingi tulikuwa tukiongozana kama kumbikumbi.Kwa kiasi kikubwa Ashura alikuwa akinisaidia sana, kwani ni msichana aliyetokea katika familia ya kitajiri. Binafsi nilikuwa naishi maisha ya kujinyima sana kutokana na hali halisi ya maisha yangu.


Baada ya mwaka mmoja kupita tukiwa tunaendelea kuishi pamoja, Ashura alipata mchumba ambaye alikuwa akija kumtembelea mara kwa mara, siku moja nikiwa nimeketi kitandani nikijisomea Ashura alikuja na kusema "Batuli, leo mchumba wangu atakuja kulala hapa, sasa sijui itakuwaje." Nilimtizama Ashura kwa dakika chache bila ya kuzungumza chochote halafu nikamwambia.
 "Mh, lakini ni bora ungeniambia mapema sasa hivi ni saa tatu za usiku, nitaenda  kulala wapi" Alikuwa amesimama mlangoni huku akiguna na kusema "Sasa sijui itakuwaje, lakini mimi namwambia aje, tutajua la kufanya" Moyoni mwangu nilikuwa nawaza "Hivi Ashura anawezaje kumwambia mpenzi wake aje kulala wakati chumba ni kimoja na kitanda ni kimoja sasa akija mimi nitaenda wapi". Nilikosa amani kabisa lakini sikuwa na namna. Haukupita muda mrefu  yule mchumba wake alikuja na walikubaliana kuwa watalala kitandani na mimi nitalala kwenye kochi. 


Siku hiyo nililala kwa tabu sana, lakini ilinibidi nivumilie na kufikiri kuwa ilikuwa ni siku hiyo moja tu, lakini hali ile iliendelea mara kwa mara, na mimi nilikuwa nikilala kwenye kochi. Siku moja nilirudi nikiwa nimechelewa nakukuta mlango umefungwa. nilibisha hodi bila ya mafanikio. Ilinibidi niondoke na kwenda kuomba kulala kwa jirani. Kesho yake nilipomuuliza Ashura kwanini hakunifungulia mlango akasema kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi.


Mambo yaliendelea kuwa magumu, kwani Ashura aliendelea kunifanyia visa vya hapa na pale wakati mwingine alikuwa akinizungumzia vibaya kwa watu, kuwa mimi namtaka mpenzi wake halafu mimi ni masikini na sina uwezo kila kitu namtegemea yeye. Nilikuwa navumilia sana. Siku nyingine alikuwa akija anaimbia nyimbo za mafumbo "kodi nimelipa mie, kulala ulale wewe, chakula nimenunua mie kula unakula wewe" majanga mbona majanga" huku akicheka na kuondoka. Kutokana na hali halisi ya maisha yalivyokuwa yakiendelea niliamua kumuomba rafiki yangu mwingine anisaidie hifadhi kwa muda huku nikiwa naendelea kutafuta pesa ya kupangisha  chumba pale chuoni. 


Siku hiyo nilipokuwa nakusanya vitu vyangu Ashura alikuja na kuniuliza "Hee Batuli, mbona unondoka jamani, mmh ghafla ghafla hivi" Nilimtizama na kusema "Akufukuzaye hakuambii toka hata siku moja vitendo tu utaviona kuwa huyu mtu hapendi uendelee kuishi naye, mimi nimeamua kuondoka.  samahani sana kama kuna jambo lolote nilikukosea, na pia asante sana kwa kunisaidia kwa kipindi chote tulipokuwa pamoja".


Baada ya miezi sita kupita Ashura alikuwa ametengana na mpenzi wake, na kwa kipindi chote hicho alikuwa haongei na mimi, siku moja aliamua kunifuata na kuniomba msamaha kwa yote aliyonikosea. "Naomba unisamehe Batuli mimi ni binadamu sijakamilika, nisamehe rafiki yangu najua nilikukosea sana" Kwasababu mimi nilikuwa sina kinyongo tena bila hiana nilimsamehe Ashura na tuliendelea kuwa marafiki kama kawaida.

Maoni 1 :

  1. Hadithi nzuri.
    Mamii vipi ile simulizi ya. Bado mimi?

    JibuFuta

Unakaribishwa kutoa maoni yako.