James alikuwa ni kijana mtanashati, mwenye mvuto na pia alikuwa ni mfanyabiashara wa vifaa vya magari. Maisha yake alikuwa akipenda sana wanawake warembo, na kutokana na muonekano mzuri na pesa alizokuwa nazo aliwavutia warembo wengi, Mara nyingi marafiki zake walijaribu kumshauri aachane na tabia ya kujihusisha kimapenzi na wanawake wengi, lakini kama waswahili wasemavyo, "Asiyesikia la mguu uvunjika guu na asiyefunzwa na mama yake hufunzwa na ulimwengu".
Alikuwa hasikii lolote,na wakati mwingine alikuwa akijitapa na kuwakejeli wenzake "Mimi nina pesa nyingi sana, na pia sina kasoro yoyote, ni rahisi kwangu kuwa na mwanamke ninayemtaka, sasa hawa marafiki zangu wananionea wivu kwasababu napendwa na warembo" Alikuwa akiongea kwa Kujigamba James. Pia alikuwa siyo mtu wa kudumu katika mahusiano, wanawake wengi walikuwa wakilia kutokana na kuumizwa kimapenzi na James, na alikuwa tayari kufanya lolote ili aweze kumpata msichana anayemtaka, kuna kipindi alidiriki hadi kutoa mahari kwa dada mmoja ambaye alimfuatilia kwa kipindi kirefu bila mafanikio, kwani dada huyu alionyesha kuwa na msimamo zaidi.
Lakini kwa James aligonga mwamba, kwani James alikuwa ni mtu ambaye yupo tayari kutumia gharama yoyote ile ili aweze kukubaliwa ombi lake, alichokifanya ni kumuhakikishia yule dada kuwa atafunga naye ndoa, hivyo alikwenda kutoa mahari pamoja na kumvisha pete ya uchumba. Dada huyu baada ya kuona hivyo, alimuamini sana James na sasa alikuwa huru na kumpa kila alichokuwa anakitaka. Baada ya James kuridhika na penzi la huyu dada, alibadilika ghafla, na hata huyu dada alipokuwa akiuliza kuhusu ndoa James alikuwa akitoa sababu za uongo na baadaye alimuacha kabisa. Alikuwa hajali kama kufanya hivyo anatenda kosa la kumuumiza yule ambaye alimuonyesha mapenzi ya kweli.
Baada ya mwezi mmoja tokea aachane na dada huyo.James katika matembezi yake ya hapa na pale akiwa katika ukumbi wa disko, ambapo kulikuwa na warembo wengi wakicheza muziki, huku James akiwatizama kwa macho ya matamanio ndipo alipokutana masichana mrembo aitwaye Lina. Moja kwa moja James alimfuata na kuanza kucheza naye. Lina alikuwa ni mrefu mithili ya twiga, alipendeza na gauni lake fupi liloonyesha sehemu kubwa ya mapaja yake meupe, nywele zake zilikuwa ndefu, na macho yake kama gololi yaani alikuwa mrembo sana kiasi kwamba James alikuwa amekufa kaoza kwa mrembo huyu "Lina wewe ni mzuri sana kuliko wasichana wote niliowahi kuwaona, nimekupenda sana" Lina alikuwa anatabasamu huku akisema "Asante James wewe pia ni mzuri sana nimekupenda pia".
Siku hiyo walikunywa na kufurahi pamoja, baadaye James alimuomba Lina waende kupumzika pamoja, Lina alikubali bila kipingamizi "Sawa James lakini tutaenda kupumzika nyumbani kwangu" James aliyekuwa ameshalegea huku akimtizama Lina akasema "Bila shaka mpenzi popote pale nitaenda na wewe" Basi waliongozana hadi nyumbani kwa Lina ilikuwa ni nyumba ya kifahari iliyosheheni vito vya thamani, James alikuwa akishangaa huku na kule Lina alimvuta hadi chumbani akaanza kumkumbatia kwa nguvu na kumbusu huku James akiwa amefumba macho yake. Ghafla akiwa anaendelea kupigwa mabusu motomoto, James alishtuka kusikia sauti ya paka akilia (nyau,nyau,nyau) akajivuta mikononi mwa Lina na alipomtizama Lina hakuamini alichokiona kwani sura ya Lina ilibadilika na alikuwa na sura nyingine ya mnyama ambaye ni paka na mwili wake wote ulikuwa na manyoya.
James alishtuka sana "Mungu wangu, nini hiki, Mamaaa nakufaa" Lina alicheka kwa sauti kali na kusema "Usiogope James mimi ni malaika wa moyo wako, ni mrembo kama wale wote uliokuwa nao, nahitaji penzi lako" James alitetemeka na kuanza kulia hadi haja ndogo ilimtoka,Nguvu zilimwishia na kupoteza fahamu, alipozinduka alijikuta amelala nje pembezoni mwa bahari. Na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa James kupenda warembo. Alibadilisha mwenendo wa tabia yake kabisa. "Kamwe siwezi kurudia tena kosa, nahisi nimeponea chupuchupu".
TAFAKARI SASA NA CHUKUA HATUA, KWANI SIYO KILA KING'ARICHO NI DHAHABU
Mmh! Hii kali. luv u adela keep it up mumy
JibuFuta