MTUNZI : ADELA DALLY KAVISHE |
"Nyamaza kimya tena nisikusike ukizungumza chochote nitakuuwa leo" Ilikuwa ni sauti kali ya mume wake na Tunu aliyekuwa akiongea kwa jazba huku akiwa ameshikilia kisu mkononi na kuanza kumchana Tunu mithili ya mtu anayekata nyama ya kwenda kuchoma" Tunu alikuwa analia kwa uchungu sana, na akijaribu kuomba msaada bila ya mafanikio.
Maisha ya Tunu baada ya kuolewa mwanzoni alikuwa akiishi kwa furaha. Lakini baadaye maisha yalibadilika baada ya kupata ujauzito na kufanikiwa kupata mtoto mmoja, Ambaye baada ya mwaka mmoja Mtoto alifariki kutokana na kuugua homa kali sana. Baada ya mtoto kufariki Chachunda ambaye ni mume wa Tunu, alibadilika na kuwa mwenye hasira kila wakati, na mara zote alikuwa akimlaumu mke wake kuwa yeye ndiye chanzo cha mtoto wao kufariki.Tunu alipata mateso makali sana, kiasi kwamba alitamani kuondoka na kurudi kwao lakini wazazi wake walimshauri avumilie kwani angerudi nyumbani ingekuwa ni aibu kubwa sana kwa familia yao.
Maisha yaliendelea huku Tunu akivumilia yale yote anayofanyiwa na mume wake. Baada ya miezi michache Tunu alifanikiwa kubeba ujauzito kwa mara ya pili, alifurahi sana kwani alijua kuwa akifanikiwa kupata mtoto, Furaha, amani na upendo vingerudi katika ndoa yake. Baada ya miezi minne kupita. Siku hiyo Chachunda alichelewa sana kurudi nyumbani, ilikuwa ni majira ya saa sita na nusu usiku ambapo Tunu alimsubiri kwa muda mrefu na baadaye usingizi ulimpitia na kulala fofofo. Chachunda aliporudi alikuwa amelewa, alibisha hodi muda mrefu bila ya kufunguliwa mlango.Aliendelea kugonga mlango kwa nguvu, ndipo Tunu alishtuka haraka kutoka usingizini na kwenda kufungua mlango.
Alipofungua tu huku akiwa anafikicha macho yake kutokana na usingizi akasema "Samahani mume wangu, nilikuwa, ....."Kabla hata hajamaliza kuongea alshtukia anapigwa vibao katika paji la uso "Kenge mkubwa wewe, yaani unataka mimi nilale nje, Nyumba ya Baba yako hii, mchawi mkubwa sasa leo nitakufundisha adabu" Alimshika na kumvuta Tunu huku akibamiza mlango na kuufunga kwa nguvu Tunu alikuwa anatetemeka kwa kuogopa akasema "Mume wangu, naomba unisamehe, tafadhali usinipige, tizama hali niliyonayo, nionee huruma jamani, unaniumiza, ni bahati mbaya nilipitiwa na usingizi, naomba unisamehe tafadhali" Aliongea kwa uchungu huku machozi yakibubujika katika paji la uso wake.
Lakini Chachunda hakujali alimtupa chini na kuanza kumpiga mateke huku akimtolea maneno makali "Eti nionee huruma na hali yangu, Paka mkubwa wewe, sasa nakupiga mateke ya kichwa na mgongoni ili mtoto asiumie, lazima nikufundishe adabu leo" Alimpiga sana siku hiyo baadaye alimuacha Tunu akiwa anaendelea kulia na yeye alingia chumbani kulala.
Asubuhi ilipofika hali ya Tunu ilizidi kuwa mbaya sasa alikuwa akisikia maumivu makali sana tumboni, alilia na kutembea taratibu kisha alitoka nje kuomba msaada, Kuna Mama mmoja ambaye alikuwa akiishi maeneo yale alimuona na kwenda kumsaidia. haraka alisaidiana na majirani wengine kumpeleka hospitali, ambapo wakiwa njiani damu zilianza kumtoka kwa wingi Tunu ambaye alikuwa akilia kutokana na maumivu makali. Maskini baada ya kufika hospitalini haraka alipelekwa katika chumba cha matibabu lakini tayari mimba ilikuwa imeharibika. "Tunu alilia sana "Eeeh Mungu naomba unisaidie, mume wangu ananifanyia ukatili sana, sasa nimempoteza mtoto wangu, inaniuma sana, Nimechoka na mateso nisaidie Mungu wangu".
Siku hiyo alilazwa pale Hospitali.Na kwa muda wote huo mume wake hakufika hata pale hospitalini ijapokuwa alipelekewa taarifa. Kesho yake Tunu aliruhusiwa kurudi nyumbani, Alipofika alimkuta mume wake akiwa ameketi pamoja na mzee mmoja ambaye alikuwa akijulikana kama mganga, pale kijijini kwao.Tunu alishangaa kumuona yule mganga. Akiwa anaendelea kushangaa mume wake alinyanyuka na kusema "Leo ndiyo siku yako ya mwisho, mchawi mkubwa wewe, yaani umemuuwa mwanangu wa kwanza, na kama haitoshi umeuwa hadi kiumbe kilichokuwa tumboni, sasa leo nakuuwa mimi mwenyewe".
Tunu alikuwa amebaki amepigwa butwaa na kusema "Ati mimi mchawi? Nimewaua watoto wangu?, Eee Mungu wangu.."Yule mganga alinyanyuka na kumtizama Tunu kwa dharau, kisha akamtemea mate usoni, na kuondoka zake. Wakati huo Chachunda alikuwa amechemsha maji ya moto jikoni kwa nia ya kutaka kummwagia Tunu. "Sasa leo nakuchemsha kama kuku, yaani na kuchuna kama mbuzi, mchawi mkubwa" Wakati Tunu akiangalia uwezekano wa kukimbia mara Chachunda alikuja na ndoo kubwa ya maji ya moto na kumwagia mwilini, Tunu alipiga ukunga kwa sauti kali sana, na baada ya muda alipoteza fahamu. Chachunda alikimbia akifikiri tayari Tunu amefariki.
Majirani waliosikia ile sauti walifika haraka na kumkuta tunu akiwa amevimba mwili kutokana na kumwagiwa maji ya moto. Haraka walimkimbiza hospitali na walitoa taarifa kwa wazazi wa Tunu ambao walifika na kuhuzunika sana. Mama yake Tunu alibaki akilia kwa uchungu huku akimtizama mwanaye alivyobabuka mwili kuanzia usoni, mapajani, kifuani na mikononi. "Yalaiti ningemsikiliza mwanangu yote haya yasingetokea, huyu mwanaume ni muuaji". Baadaye taarifa zilipelekwa polisi na Chachunda alikamatwa pamoja na yule mganga. Sheria ikachukua mkondo wake wote wawili walifungwa miaka 30 jela kwa kitendo cha ukatili walichokifanya.
TUUNGANE PAMOJA KUPAMBANA NA UKATILI WAKIJINSIA. ASANTE SANA SHIRIKA LA WAANDISHI WA HABARI WANANAWAKE (TAMWA) NA MASHIRIKA MENGINE AMBAYO YANAENDELEA KUTOA MCHANGO WAO KATIKA KUSAIDIA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA. UNAPOFANYIWA UKATILI NI VYEMA KUTOA TAARIFA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.