Pages

Ijumaa, Januari 03, 2014

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

 
 ILIPOISHIA
Upendo akiwa sambasamba na Eliza alielekea sehemu ile kwenye umati
wa watu ambako James alifichwa ili akamfichue. James akiwa katikati ya
umati alimwona Upendo akiwa anatoka na pembeni akiwa na Esta
alishtuka sana kumwona Esta.
“Mungu wangu yule si Esta? Anafanya nini hapa na mbona yupo karibu
na Upendo? Kuna nini kinaendelea hapa?” James aliwaza na kujiuliza
maswali mengi yaliyokosa majibu.

INAPOENDELEA


Kwa muda wa takribani dakika mbili hivi James alikuwa kama mtu
aliyechanganyikiwa. Watu waliendelea kushangilia huku James akiwa hajui
nini cha kufanya baada ya kumwona Eliza ambaye ndio Esta akiwa
anatazama huku na kule kama vile mtu anayetafuta njia ya kutokea.
James akiwa anahangaika nini cha kufanya Upendo na Eliza waliendelea
kuangalia huku na kule wakimtafuta katika umati wa watu. Ghafla Eliza
akamwona Julias na kushtuka, lakini hakujua kama ndio mume mtarajiwa
wa dada yake.

“Haa! Hivi yule si Juliasi? Amefuata nini hapa? Au ni ndugu wa huyo
James? Mmh! Nina bahati kweli sikutarajia kumwona. Sasa hii ni nafasi
nzuri ya kuzungumza naye kuhusu hatima ya uhusiano wetu na hii mimba
yake.” Eliza alijiuliza maswali mengi huku akishangaa na kufurahi kuonana
tena na Juliasi. Zoezi la kumfichua James halikufanikiwa kwani Upendo
alishindwa kabisa kumwona James alipokuwa. Hivyo waliamua kurudi na
kukaa katika sehemu maalumu iliyotayarishwa kwa ajili ya Upendo.


Sherehe ilianza rasmi, watu walijaa sana kushuhudia tukio muhimu la
kuagwa kwa Upendo. Mshereheshaji (MC) aliimudu barabara kazi yake
kwani alifanikiwa kumchangamsha na kumchekesha kila aliyehudhuria.
“Ndugu wageni waalikwa ninayo heshima kubwa sana ya kuwakaribisha
katika sherehe hii ya kumuaga binti yetu Upendo.” Alianza kuonyesha
mbwembwe zake huku akigeuka kumwangalia Upendo. Kisha akaendelea.
“Karibuni sana kuja kwenu ndo kumefanikisha sherehe hii. Kwa kuwa leo
ni siku ya furaha basi kila mtu afurahi kwa kadiri ya uwezo wake. Vyakula
ni vingi, vinywaji vimejaa, burudani kebekebe. 

Pia kutakuwa na mashindano ya kucheza twisti kwa akina baba wenye vitambi (vicheko)
ambapo washindi watano wa kwanza watapewa zawadi na akina mama:
Mshindi wa kwanza atakabidhiwa kanga yenye ujumbe ulioandikwa
‘WALIONDANI WANATAMANI KUTOKA.’
Mshindi wa pili ‘atapewa kanga iliyoandikwa ‘WALIO NJE
WANATAMANI KUINGIA.’
Mshindi wa tatu atapata kanga yenye ujumbe ‘WADOGO
WANATAMANI UKUBWA.’
Mshindi wa nne atapewa kanga yenye maneno ‘WAKUBWA
WANATAMANI KURUDIA UTOTO.’ na
Mshindi wa tano ‘NDOA NDOANA’”

Aliongea MC huku akishangiliwa na umati wa watu na wengine
wakisimama na kwenda kwa Upendo kumrushia maua ya kila rangi. Ama
kweli MC alichangamsha sherehe vilivyo.
Upendo aliinama chini huku maua yakiendela kumwagwa alipokaa.
Alitafakari sana juu ya manjonjo ya MC kwani hakuelewa maana ya
ujumbe ulio katika zile zawadi watakazo kabidhiwa washindi wa twisti.

Sherehe iliendelea kupamba moto, muda ulifika wa kupata chakula huku
vinywaji vikisambazwa kila kona kwa fujo shughuli zote hizo
zikisindikizwa na muziki mwororo ulitumbuiza kwa sauti ya chini na ya
kubembeleza. Wakati kamati ya chakula ikijiandaa kuanza kugawa chakula,
ghafla MC alisimama mbele.
“Studio! Studio! Tafadhali!” MC alichombeza kumwashiria DJ azime
muziki ambaye naye alifanya hivyo mara moja. Kisha akaendelea.
“Wageni wetu waalikwa mabibi na mabwana. Mimi binafsi sitahesabia
kama shughuli hii imefanikiwa endapo Mchumba wa Upendo
hatutamtambua. Kwa hiyo nakuomba Upendo ututambulishe mchumba
wako kwa utaratibu nitakao kupangia.” Alishangiliwa MC hata kabla
hajamaliza kusema huku wengine wa kitamka neno kweli kwa sauti za juu.
James aliposikia hivyo, moyo ulimdunda alijua sasa muda wa kuumbuka
umefika. Alijikaza kiume na kusubiri kitakachotokea.

“Upendo njoo hapa!” Alitamka MC huku akiagiza aletewe glasi yenye
mvinyo na ua jekundu lililoandaliwa kwa shughuli hiyo. Watu wote
walitulia kimya mama mmoja mwenye mtoto aliyekuwa akilia alitoka naye
nje haraka sana ili kutoharibu utulivu. Upendo alipofika, MC akaendelea.
“Upendo!” Alitamka MC huku akimwonyesha ua na ile glasi yenye
mvinyo.

“Utakwenda wewe mwenyewe bila mpambe wako hadi alipo mchumba
wako. Ukifika mpe hili ua kama ishara ya upendo wenu wa kweli. Kisha
mpe huu mvinyo kama ishara ya kumkaribisha mchumba wako katika
maakuli kisha utamshika mkono na kumwongoza hadi katika meza ya
chakula, halafu utapakuwa chakula ambacho kitawatosha wote wawili
kisha utarudi kwangu ili niwaelekeze cha kufanya.” Alipomaliza tu
kuongea shangwe na vicheko viliibuka tena huku wengine wakimsifu MC
kwa umahiri alionao katika kumudu na kuipamba sherehe.

Upendo alikwenda kumtafuta mchumba wake huku ameshika vile vitu
alivyokabidhiwa na MC, alitembea kwa madaha yote asijue wapi amekaa
James aliangalia huku na kule lakini wapi hakumuona James. Baada ya
kuhangaika sana huku watu wakiwa na shauku ya kumwona James mwisho
akamwona amekaa katikati ya wazee aliokuja nao, aliongeza mwendo na
kwenda moja kwa moja hadi alipokuwa na kupiga magoti kisha akampa
lile ua huku akishangiliwa na kila mtu. Wengine wakitamka SAFI SANA!
UMECHAGUA!. Wakati Upendo akijiandaa kumpa James mvinyo kama
alivyoelekezwa na MC ghafla Eliza alipiga kelele ambazo zilimshtua kila
mtu.
“Nooooo! Hapana! Hapana! Juliasi!, Juliasi! Haiwezekani! Nasema
haiwezekani!” Yalimtoka maneno Eliza kwa mfululizo huku akirukaruka
kuelekea alipo James. Watu walijaribu kumshika lakini Eliza aliwazidi
nguvu, alikwenda hadi alipo James huku akitweta kama mtu aliyepandisha
mapepo.
“Kumbe wewe ni shemeji yangu?” Ilikuwa ni sauti ya Eliza mdogo wake
Upendo ambaye aliwafanya watu wamshangae ana matatizo gani. Ndipo
kabla hajaendelea kuzungumza alianguka na kuzimia.
Wazazi wake walishangaa nini kimetokea na huyo Juliasi ni nani.
“Kuna nini jamani mwanangu amekuwaje leo?” Aliuliza mama Upendo
huku akionyesha mshtuko mkubwa. Basi ndugu walimchukua na
kumpeleka ndani huku akipepewa.
USIKOSE MWISHO WAKE

Maoni 2 :

  1. ohooo ishakuwa balaa...

    JibuFuta
  2. Jamani me hofu kwa pendo...duh

    JibuFuta

Unakaribishwa kutoa maoni yako.