Siku hiyo Kasebo
alionekana kukosa furaha, kutokana na kupungukiwa na pesa ya kulipa kodi
ya nyumba aliyokuwa amepanga. Akiwa amejiinamia huku akiendelea kuwaza nini cha
kufanya wazo lilimjia aende kumuomba msaada rafiki yake kipenzi anaitwa Roby. Haraka
alinyanyuka na kuelekea nyumbani kwa Roby ambapo alikaribishwa vizuri na moja
kwa moja alielezea shida yake. Roby alimsikiliza kwa umakini sana na alimuonea
huruma hivyo aliamua kumsaidia kwa kumkopesha kiasi cha shilingi laki tano.
Kasebo alifurahi
sana huku akimshukuru rafiki yake na kuahidi kuwa atarudisha pesa hiyo baada ya
wiki nne. Maisha yaliendelea, baada ya wiki nne kupita Kasebo hakumrudishia ile
pesa Roby kama alivyomuahidi, ijapokuwa kwa kipindi hicho mambo yake yalikuwa
mazuri kwani alionekana kutumia pesa nyingi katika starehe lakini Roby
alipokuwa akimkumbusha kuhusu kulipa deni alikuwa akinyamaza kimya na kuendelea
kutoa ahadi kuwa atamlipa, lakini siku zilizidi kwenda bila ya kulipa deni
hatimaye miezi mitatu ilipita.Roby alikuwa ni kijana mpole sana, baada ya kuona
Kasebo anamzungusha kumlipa deni lake aliamua kunyamaza kimya.
Katika maisha unaambiwa
shida haishi mara moja siku zote unaweza kusaidiwa leo lakini zikapita siku
mbili tatu ukaomba msaada tena. Siku moja Kasebo alipata matatizo katika
sehemu aliyokuwa anafanya kazi na hivyo alisimamishwa kazi kwa muda, kutokana
na hali hiyo maisha yake yalikuwa magumu sana, ndipo siku moja aliamua kwenda
kwa Roby kumuelezea matatizo yake. Kama kawaida Roby alimsikiliza na kumuonea
huruma sana kutokana na hali aliyokuwa nayo, aliamua kumsaidia ijapokuwa
alikuwa bado hajamlipa deni la kwanza lakini alimkopesha tena kiasi cha
shilingi laki tatu.
Kasebo alifurahi
sana na kuahidi kuwa atamrudishia pesa zote baada ya miezi miwili. Siku zilienda
hatimaye baada ya wiki tatu Kasebo alirudishwa kazini, na sasa aliwekwa katika
kitengo kizuri ambapo alikuwa akilipwa pesa nyingi zaidi. Baada ya miezi miwili
kupita Roby alienda nyumbani kwa Kasebo kumsalimia na kumkuta akiwa mwenye
furaha sana lakini alipomkumbushia tu deni lake alibadilika na kuanza
kulalamika "Yaani Roby shilingi laki nane ndiyo unanidai, kana kwamba
umenikopesha milioni mia moja, nitakulipa hivyo vihela vyako usijali"
Aliongea Kasebo huku akimuangalia Roby ambaye alibaki akimshangaa "Eti
unasema vihela? Ama kweli binadamu tunajisahau, ulikuja mpole sana wakati ukiwa
na shida sasa hivi umepata mafanikio unaonyesha dharau, sasa sikiliza mimi
ninchotaka unilipe pesa zangu tena sasa hivi vinginevyo tutaonana wabaya".
Roby alikasirika sana
siku hiyo lakini Kasebo hakujali na hakumlipa pesa yoyote siku hiyo. Baada ya
wiki moja kupita hatimaye Roby aliamua kumshtaki Kasebo ili aweze kulipwa deni
lake, ijapokuwa walikuwa ni marafiki wa siku nyingi lakini Roby aliksirika
kutokana na Kasebo kumtolea majibu ya kashfa. Baada ya Roby kumshtaki Kasebo
hatimaye alilipwa pesa zake huku Kasebo akionekana kukasirika kana kwamba
ameonewa lakini baadaye alikuja kugundua kuwa yeye ndiye mwenye makosa na
kumuomba msamaha Roby na sasa wanaishi kwa furaha kama zamani. Kumbuka dawa ya
deni ni kulipa na siyo unaenda kuopa huku mikono ikiwa nyuma lakini kulipa ina
kuwa matanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.