Pages

Jumatatu, Aprili 14, 2014

HISTORIA FUPI YA GURUMO,,BURIANI GWIJI MUASISI MITINDO YA MSONDO, SIKINDE NA NDEKULE .

Historia ya maisha Gurumo anayefahamika pia kama Kamanda na mashabiki wa muziki ilianzia mwaka 1940 alipozaliwa, katika Kijiji cha Masaki Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Anaeleza kuwa baada ya kuzaliwa alipata elimu ya msingi, wakati huo pia akisoma madrasa, chuo cha kufundisha elimu ya Dini ya Kiislamu, lakini alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari baada ya baba yake kufariki.
“Baada ya baba kufariki alinichukua mjomba wangu Selemani Sultani Mikole, wakati huo alikuwa akiishi maeneo ya Ilala Jijini Dar es Salaam,” anasimulia Gurumo.
Anaongeza: “Ukiacha mambo mengine, mjomba wangu huyo ndiye chachu ya mafanikio yangu katika kila jambo, licha ya awali kunizuia nisifanye mambo tofauti, zaidi ya kuijua dini.”
Alipotakiwa kueleza iwapo historia hiyo ya maisha yake inahusiana na wimbo wa Ukiwa alioimba akiwa na Bendi ya Orchestra Safari Sound(OSS) katika mtindo wa Ndekule, Gurumo alisema;
“Ni kweli, wimbo huo una uhusiano moja kwa moja na mjomba wangu na maisha niliyonayo sasa, hata hapa ninapoishi ni yeye alinishawishi ninunue kiwanja hiki. Kwa sasa mjomba wangu ni marehemu, lakini enzi za uhai wake alikuwa akifuatilia mambo yote kuhusu maendeleo ya maisha yangu, namshukuru.”
Gurumo alisema katika umri wa zaidi ya miaka 50, aliyotumia katika muziki hakuwa na cha kujivunia zaidi ya kujenga nyumba yenye vyumba 17 eneo la mabobo na kujenga nyumba nyingine kwenye shamba lake lililopo kijijini kwao Masaki Kisarawe, mkoani Pwani.
Kilio cha Gurumo kukosa usafiri wake kilipata jibu wakati nyota wa muziki wa Bongofleva mwenye mafanikio  Daimond Platnumz alipofanya jambo lisilotarajiwa na wengi kwa kumzawadia gwiji huyo gari dogo la kutembelea aina ya Toyota FunCargo siku mkongwe huyo alipotangaza kustaafu muziki.
Gurumo hakuficha kitu kuhusu ujana wake kwa kueleza mbali na ubitozi aliokuwanao, pia alikuwa gangwe enzi zake na pia aligeuka kuwa mtumwa wa pombe kutokana na kuwa mlevi aliyepitiliza. Alisema alikuwa anakunywa pombe isivyo kawaida jambo amabalo lilikuwa likimfanya akaorofishane na mama yake mzazi aliyetishia kumuachia laana kama angeendelea kuendekeza ulevi.
 Alisema "Kwa wanaonijua mimi sidhani kama hili ni jipya nilikuwa mlevi haswaa, kiasi mama alishindwa kunivumilia na kutishia kuniachia laana" Alisema "Baada ya kushindana na shetani kwa muda mrefu akikorofishana hara na mkewe Pili bint Said Kitwana hatimaye aliachana na ulevi mwaka 1982 miezi michache tangu Mama yake mzazi Kufariki. Gurumo ametangulia mbele ya haki, tumuombee apate makazi mema . Mungu ailaze roho yake Mahali pema Peponi. Amina.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Unakaribishwa kutoa maoni yako.