Hilo limedhihirishwa na John Waweru, raia wa Kenya ambaye amefanikiwa kufuga kucha zake kwa muda wa miaka 12 na kufikia urefu wa futi moja na inchi 3.
Anasema amefanikiwa kuzigeuza kucha hizo kuwa mojawapo ya kivutio cha utalii nchini Kenya kutokana na kuwafanya watalii kuzishangaa na hivyo kumpatia pesa kama malipo ya kivutio hicho.
Ili kuzidi kuwavutia watalii Waweru amezipaka kucha zake rangi zilizopo katika bendera ya Kenya hali inayomwongezea mvuto zaidi.
“Nimezipaka rangi ya bendera yetu kwa kuwa watalii wengi wanaokuja kupiga picha na mimi wanazipenda rangi hizo ili kuwafurahisha wateja wangu,” anasema Waweru akiongea na Kenya News
Anasema siku biashara ikiwa nzuri ana uhakika wa kurudi nyumbani na Sh5,000 (sawa na Sh94,000 za Kitanzania).
Waweru (33) anasema tangu mwaka 2002 alipoanza kufuga kucha hizo hajawahi kuzikata wala kuzipunguza kutokana na sababu yoyote ile.
“Baada ya kumaliza shule nilipata kazi lakini kucha zikawa zinakua kwa kasi kiasi cha kunifanya nishindwe kutimiza majukumu yangu nikaona bora niache kazi ili ziendelee kukua bila kikwazo chochote, nazilinda sitaki zikatike kwa namna yoyote.”
Anafafanua kuwa kikubwa anachokifanya ni kuilinda rasilimali hiyo akiamini kuwa ndiyo mtaji wake, hivyo siku zote hujaribu kujiweka mbali na ugomvi au hatari yoyote itakayosababisha kucha hizo kukatika.
“Tangu nimeanza kufuga kucha nimekuwa mtulivu mno. Najiweka mbali na ugomvi ili nisije kupoteza chanzo changu cha mapato. Nafahamu fika kuwa kupigana kunaweza kusababisha kucha zangu zikatike kitu ambacho sitaki kitokee,” anasema.
“Hata pombe nimeacha kunywa. Najaribu kufanya kila linalowezekana ili kucha zangu zisiingie kwenye hatari na huwa nazifunika kuziepusha na purukushani.”CHANZO MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.