Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Alizaliwa mwaka 1905 na kufariki tarehe 7 April 1972 kwa kupigwa risasi.Karume aliongoza mapinduzi yaliyomwangusha Sultan aliyekuwa akitawala Zanzibar hapo mwaka 1964. Baada ya miezi mitatu Zanzibar iliungana na Tanganyika iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Nyerere Baada ya muungano wa nchi hizi mbili uliozaa jina la Tanzania Karume alikuwa makamu wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Watoto ni taifa la kesho, katika kulitekeleza hilo, Hayati Karume aliona umuhimu wa watoto katika kujenga taifa madhubuti na lenye matarajio katika kufikia kilele cha maendeleo ya taifa lake. Alitamani kila kilichopo kwenye ardhi ya Zanzibar kiishi vizuri na kwa amani bila ya kunyanyaswa, kubugudhiwa wala kubaguliwa kwa hali yoyote ile ya kimaumbile wala kisaikolojia.
Marehemu Mzee Karume alikuwa mpenzi wa watu na alipenda watu pia, katika kuwajali watu wa taifa lake aliwawekea huduma zote za jamii bure na kuwa ni haki ya kila mtu kama huduma za afya, elimu, maji safi na salama, barabara pamoja na makazi bora. Katika kuwajali watoto yatima Mzee Abeid Aman Karume aliwapa huduma zote za binadamu pamoja na kuwajengea nyumba iliyo bora na salama kwaajili ya kupatiwa malezi miaka 48 iliyopita.
Kuanzishwa kwa nyumba ya watoto yatima Forodhani kuliweka bayana na kuonesha kwa vitendo mapenzi yake kwa watoto hao, kwani kuliwaepusha watoto hap uwezekano wa kunyanyaswa na kubaguliwa katika jamii zao lakini pia kuliwapunguzia mzigo jamii zikiwemo zilizokuwa zikiwalea watoto hao ilihali zikiwa kwenye mazingira magumu. Aidha, hayati Karume alijali umuhimu wa malezi bora ya watoto yatima , hivyo alijitahidi kadri alivyoweza kwa kuwapa malezi bora ili waondokane na dhana ya uyatima.
Nyumba ya watoto yatima ilianza kutumika baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, ambapo kwasasa nyumba hiyo imehamishiwa Mazizini Wilaya ya Magharibi Unguja.Katika kuyaenzi na kuyaendeleza mapenzi ya Hayati Karume kwa watoto yatima, Jumuiya ya maendeleo ya vijana, Elimu na Mazingira Zanzibar "ZAYEDESA"Iliona umuhimu wa kuimarisha makazi kwa watoto hao ndipo ilipojenga nyumba kubwa na ya kisasa huko Mazizini Unguja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.