Pages

Jumanne, Novemba 06, 2012

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SEHEMU YA ...1...

Kwa wale wadau wa simulizi nitaendelea kuwawekea simulizi , kuna simulizi nilikuwa sijaziendeleza kama ya  MAMA MDOGO, DADA YANGU ambazo zipo katika kitabu changu cha MALIPO NI HAPAHAPA  zitaendelea kwa wale ambao hamkusoma mwanzo ingia katika kipendele cha SIMULIZI ZA KUSISIMUA katika blog hii utapata kusoma sehemu zote za simulizi . katika kitabu cha MALIPO NI HAPAHAPA zipo simulizi tatu na zote utapata kuzisoma na nyingine nyingi zinakujia soon tuendelee kuwa pamoja.

MALIPO NI HAPAHAPA SEHEMU YA KWANZA

Katika Mji wa Arusha Mtaa wa Kaloleni ni eneo ambalo wakazi mbalimbali walipendelea sana kuishi kutokana na mazingira yake kuwa tulivu na yenye mandhari nzuri. Katika mtaa huo aliishi mzee mmoja aiitwaye Magesa. Mzee huyo alikuwa na mke na watoto watatu, watoto wawili wakiume ambao waliitwa Joseph na Peter na mtoto mmoja wa kike aliyeitwa Julieth.

Mzee Magesa hakuwa na uwezo mkubwa sana kifedha. Maisha ya Mzee huyo na famila yake yalitegemea sana kipato kidogo kilichotokana na biashara ya kuuza mboga sokoni ambayo alikuwa anaifanya siku zote za maisha yake hadi akapewa jina la ‘Muuza mboga’. Mke wake alikuwa ni mama wa nyumbani akijishughulisha na kupika chapati na kuuza ili kuongeza kipato kwa ajili ya mahitaji ya pale nyumbani.

Maisha yalikuwa magumu sana lakini familia ilikuwa na furaha na upendo kwani waliishi kwa kupendana na kuheshimiana. Mzee Magesa aliwapenda sana watoto wake, kwani mara nyingi alikuwa akiwafundisha mambo mbalimbali kuhusu maisha ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kusoma. Julieth alikuwa Darasa la Tano na mdogo wake Joseph alikuwa Darasa la Pili, Peter yeye alikuwa hajaanza shule.

Siku moja yapata saa mbili usiku Mzee Magesa akiwa amekaa kwenye sebule karibu na chumba chake cha kulala alimwita Julieth kwa ajili ya mazungumzo.
“Julieth!” Mzee Magesa aliita kwa nguvu. “Abee baba!” Aliitikia Julieth aliyekuwa anaosha vyombo huku akimwendea baba yake.
“Unafanya nini saa hizi?” Mzee Magesa aliuliza kwa sauti ya upole.
“Naosha vyombo baba.” Alijibu Julieth kwa adabu.
“Umemaliza?” Aliuliza tena Mzee Magesa.
“Hapana baba, bado sufuria mbili.” Alijibu Julieth.
“Acha utamalizia kesho kaa hapo nina maongezi na wewe.” Aliongea Mzee
Magesa huku akinyoosha kidole kwenye kiti cha miguu mitatu.
“Nimekuita ili kukwambia maneno machache kuhusu hali ya maisha yetu
hapa nyumbani.” Mzee Magesa alianza kueleza sababu ya wito huku
Julieth akimwangalia na kumsikiliza baba yake kwa makini.

“Kama unavyoona hali yetu ya maisha tunayoishi ni ngumu sana. Na hii
inatokana na kipato chetu kuwa kidogo. Namna pekee ya kujikwamua na
hali hii ni wewe mtoto wetu mkubwa kusoma kwa bidii ili uje utusaidie
sisi wazazi wako pamoja na wadogo zako. Na pia …” Mzee Magesa
alikatisha ghafla huku akiwa kama amekumbuka kitu fulani muhimu.
“Mama yako yuko wapi?” Aliuliza Mzee Magesa.
“Yupo chumbani.” Alijibu haraka Julieth.
“Mama Julieth!” Aliita Mzee Magesa.
“Abee!” Aliitikia mama Julieth kutokea chumbani huku akitoka.
“Mama Julieth nina maongezi kidogo na Julieth naomba na wewe
ushiriki.” Alitamka Mzee Magesa.
“Maongezi gani hayo?” Aliuliza mama Julieth.
“Wewe kaa usikilize ndio maana nimekuita”. Mzee Magesa alijibu kisha
akaendelea kuongea na Julieth huku mama yake akiwa amekaa pembeni
mwa Mzee Magesa.
“Julieth kama nilivyoanza kukwambia maisha yetu ni magumu sana
kutokana na kipato kidogo tunachopata. Tumejaribu kufanya bidii lakini
hakuna mabadiliko. Njia pekee ya kujikwamua kiuchumi katika siku zijazo
ni elimu. Hivyo wewe kama mtoto wetu mkubwa unatakiwa usome kwa
bidii sana ili uje utusaidie sisi na wadogo zako pia. Sisi wazazi wenu
tutakazana kuhangaika kutafuta fedha ili wewe usome. Angalia Mzee
Mtokambali alisomesha mtoto wake wa kwanza hadi Chuo Kikuu, leo hii
wadogo zake mmoja yupo Kidato cha Sita na mwingine Chuo Kikuu.
Maisha ya Mzee Mtokambali ni mazuri. Ninaimani hata sisi hili
linawezekana ilimradi tu kama wewe una nia ya kusoma.”
“Ni kweli angalia mke wake anavyobadilisha kanga na vitenge, ni kutokana
na kijana wao mwenye kazi nzuri. Baba Julieth, hili linawezekana mbona
binti yetu ana nia sana ya kusoma na uwezo anao.” Alidakia mama Julieth
bila hata kusubiri Mzee Magesa amalize.

“Baba na mama nimesikia sana mawazo yenu mazuri ninapenda sana
kusoma. Nitasoma!” Alisisitiza Julieth. “Julieth wewe ndiye binti yetu wa kwanza, kumbuka wadogo zako bado ni wadogo sana nakuomba mwanangu siku zote za maisha yako mtu asikudanganye ukawachukia wadogo zako. Uwapende ndugu zako na kuwaheshimu watu wote wanaokuzunguka wakubwa kwa wodogo, kwani mwanangu kuna leo na kesho leo mimi na mama yako hatutakuwepo mshikamano na upendo ndiyo silaya yenu. 

Hata ukisoma sana kama hutawapenda na kuwaheshimu wadogo zako na watu wote itakuwa ni bure.” Aliongeza Mzee Magesa. Julieth aliinamisha kichwa chini kama vile anatafakari kitu halafu akawaangalia baba na mama yake kwa uso wenye maswali. “Baba mbona mnaongea hivi? Mimi nawapenda wadogo zangu na watu wote, hata siku moja haitatokea nikawachukia wadogo zangu. Lakini mbona leo mnaongea hivi?” Aliuliza Julieth kutaka kudadisi zaidi.
“Huu ni mwendelezo tu wa maongezi ambayo mara kwa mara mimi na mama yako tumekuwa tukifanya. Ila leo tumeongea kwa msisitizo zaidi kwani maisha ni magumu kupita siku zilizopita. Lakini pia kumbuka sasa umekuwa mkubwa hivyo lazima tukwambie msimamo wetu juu ya maisha yetu, yako na ya wadogo zako, au siyo mama Julieth!” Alifafanua Mzee Magesa huku akimgeukia mama Julieth. “Ni kweli wewe ndo mkubwa lazima uyajue haya kuanzia sasa ili kukujengea uwezo wa kuishi vizuri na watu.” Aliongeza mama Julieth. “Sawa wazazi wangu nimewaelewa.” Alisema Julieth.
“Baba Julieth naona tumalize maongezi kwani kesho asubuhi na mapema
unatakiwa uwahi sokoni kufungua biashara. Na wewe Julieth kesho ni
shule, hebu tukalale.” Alishauri mama Julieth.

“Haya Julieth nenda kapumzike ila ukae nayo kichwani yote
tuliyozungumza leo.” Alisisitiza Mzee Magesa huku akisimama kuelekea
chumbani.
“Sawa baba.” Alijibu Julieth. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA PILI........


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Unakaribishwa kutoa maoni yako.