Pages

Jumamosi, Desemba 01, 2012

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SURA YA .....7.......

MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
Baada ya mapenzi na raha kushamiri, Julieth alipata ujauzito ambao hakugundua kama ana mimba. Aligundua baada ya kwenda hospitali kupima afya yake kutokana na kutojisikia vizuri ikiwa ni pamoja na kusikia kichefuchefu. Suala la mimba lilimfurahisha sana Julieth. “Huu ndio wakati mwafaka wa kufunga ndoa, najua John atafurahi sana nikimzalia mtoto. Akija leo nitamwambia tufanye haraka tufunge ndoa.” Aliwaza Julieth. USIKOSE SURA YA ......7.........


INAPOENDELEA
Ilipofika jioni aliandaa chakula cha usiku mapema huku akiwa anamsubiri mpenzi wake arudi ampe taarifa kuhusu mimba aliyonayo. John alirudi na kumkuta Julieth anafuraha sana. “Kulikoni leo mpenzi mbona unaonekana una furaha sana kuna nini?” Aliuliza John. “Mpenzi leo nimetoka hospitali kupima nina ujauzito wako na sasa nadhani utakuwa muda mwafaka tufanye haraka tufunge ndoa.” Aliongea Julieth huku akitabasamu na kujichekeshachekesha.

”Ni vizuri Julieth lakini kwanza ukisha jifungua ndio tutafunga ndoa.” Alijibu John akionyesha kutofurahishwa na taarifa ya Julieth kuhusu ujauzito. “Jamani John ni muda mrefu tumekuwa pamoja kwa nini isiwe mapema kabla sijajifungua?.” Alisisitiza Julieth huku akimsogelea na kuweka mikono yake mabegani kwa John. “Sikiliza Julieth nikwambie; ndoa ina mipango mingi sana kwa hiyo wewe nisikilize mimi.” Alisema John huku akiwa anainuka na kuelekea chumbani.

John alikuwa kama mtu ambaye hajafurahia habari alizopewa na Julieth, basi Julieth alinyamaza kimya lakini aliendelea kufikiri na kutafakari hali aliyoonyesha John baada ya kupewa taarifa ya ujauzito. “Mbona John amebadilika ghafla kuna nini? Ngoja nimwache nitamwambia kesho vizuri.” Aliwaza Julieth huku akimfuata John .Kesho yake asubuhi kama kawaida waliamka mapema sana, Julieth aliandaa chai. Walipokuwa wanakunywa Julieth alimwambia John kuwa angependa kwenda Arusha kuwaona mama na wadogo zake kwani ilikuwa ni muda mrefu.


“John naomba niende Arusha nikamsalimie mama na wadogo zangu.” Aliomba Julieth.
“Huko Arusha tutakwenda wote siku nitakayopanga mimi, tena nikipata muda.” Alijibu John akiwa amenuna. “Vipi John mbona umebadilika tangu jana naona haupo sawa tukiwa tunazungumza unaonekana una hasira kuna tatizo gani?” Julieth alihoji. “Tatizo ni wewe unaongea sana sipati hata muda wa kupumua, tena na hii chai kunywa mwenyewe.” Akaondoka na kumwacha Julieth akiwa ameduwaa. “Huyu mwanamume amekuwaje mbona hivi jamani simuelewi.” Aliwaza Julieth.

Basi Julieth akaondoa vyombo mezani na kuendelea na shughuli zake. Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele tabia ya John ilizidi kubadilika. Alianza kuchelewa kurudi nyumbani na akirudi anakuwa amelewa sana, tabia hizo zilimuumiza sana Julieth kwani raha alizokuwa anazipata zote aliziona chungu na kujikuta akiwa mtu wa mawazo na kulia siku zote, wakati mwingine alikuwa akimpiga sana na alikuwa hataki kumsikiliza kwa chochote. Ilifikia kipindi alimfukuza chumbani kwake akawa analala chumba cha wageni.

 John hakujali kama Julieth ni mjamzito alimpiga bila ya huruma, kutokana na matatizo kuwa mengi Julieth aliamua kumpigia simu rafiki yake wa kike aliyejulikana kwa jina la mama Janeth ili kuomba ushauri kutokana na matatizo aliyonayo. Akiwa anampigia simu alikuwa chumbani bila kujua kwamba John alikuwa amejificha pembezoni mwa mlango wa kuingia chumbani akisikiliza kila kitu alichokuwa anamwambia rafiki yake. Akiwa anaendelea kuongea na simu John aliingia kwa hasira sana na kumnyan’ganya simu kisha kumpiga makofi huku akizungumza maneno makali.

“We shetani ulikuwa unazungumza na nani?” Aliuliza John kwa hasira. “John leo unaniita shetani? Halafu unanipiga?” Aliuliza Julieth huku machozi yakimlengalenga. “Ndio nani ulikuwa unamwambia mimi nakunyanyasa? We masikini nakuuliza mwendawazimu mkubwa na nitakuua leo na simu naichukua, hutakiwi kuwa na simu umekalia umbea tu. Nisikusikie unamwambia mtu yeyote mimi nakutesa mwehu wewe hata ukiwaambia watanifanya nini?”

Wakati John akiwa anasema maneno yote hayo Julieth alikuwa akilia kwa uchungu wa maumivu. “Unanionea John nimekukosea nini mimi.” Alilalamika Julieth huku akishikashika na kupapasa tumbo lake. “Nyamaza sitaki kusikia sauti yako nasikia kichefuhefu kabisa toka hapa.” Alisema John huku Julieth akiondoka akiwa analia. Ama kweli usilolijua ni sawa na usiku wa kiza. Julieth hakujua kwa nini John amebadilika vile ghafla na kwamba nini kifanyike ili kumrudisha katika hali yake ya kawaida ilikuwa ni kitu kisichowezekana ilibidi awe mvumilivu na kujipa matumaini.

Baada ya siku kadhaa kupita hakukuwa na mabadiliko yoyote ila matatizo yalizidi kila siku ilikuwa ni ugomvi. Miezi kadhaa ilipita bila Julieth kuwa na mawasiliano na wazazi wake kwani alikuwa hana simu, hivyo ilikuwa vigumu kujua hata wazazi wake walikuwa wanaendeleaje. Kwa kweli maisha yalikuwa magumu sana. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wamiezi saba lakini John alikuwa hajali. 

Maoni 1 :

  1. Simulizi, kabambe, bora uwe na kitabu ili ufaidi vyema, au sio mpendwa?

    JibuFuta

Unakaribishwa kutoa maoni yako.