Bosco Baada ya kufanikiwa kupata kazi, Alifurahi sana kwani ni muda mrefu alisota mtaani huku akitafuta kazi. Maisha yalibadilika na sasa aliweza kujikimu katika mambo mbalimbali. Katika safari yake ya maisha kabla ya kufanikiwa kupata kazi alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na msichana mmoja anayeitwa Jeni na walibahatika kupata mtoto mmoja.
Baada ya mwaka mmoja tokea Bosco aanze kufanya kazi Maisha yake yalikuwa mazuri zaidi na sasa alifanikiwa kununua gari na kuishi katika nyumba nzuri. Ilifikia kipindi wazazi wa Bosco waliamu kumshauri kijana wao aowe. Na mama yake Bosco siku zote alikuwa akimshauri afunge pingu za maisha na jeni ambaye ni mama wa mtoto wake. Jeni yeye alikuwa akifanya kazi ya dukani, kwani hakufanikiwa kuendelea na masomo baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha tano.
Bosco alikuwa hana wazo la kumuoa Jeni kwani siku zote alikuwa akiwaambia wazazi wake "Kuzaa mtoto na mwanamke siyo lazima kuwa nitamuoa yeye, mimi sina mpango huo nitamlea mtoto wangu lakini suala la kumuoa Mama yake halipo kabisa katika kichwa changu" Alisema Bosco huku Mama yake akiwa anamsikiliza kwa umakini akasema "Lakini mwanangu hapo ulipo umefikia umri wa kuoa na tena, Mungu amekujalia una kazi nzuri sasa sijui kwanini hutaki kuoa, na tena Jeni ni mwanamke mrembo, mpole na mwenye heshima, halafu wewe ndiyo ulimuharibia maisha yake baada ya kumpa mimba akiwa anasoma, leo hii humtaki?"
Bosco alimtizama Mama yake na kusema "Mama, mimi siwezi kumuoa Jeni, Kwanza nina mchumba wangu ambaye nina mpango wa kufunga naye ndoa" Mama yake alinyamaza kimya na hata Baba yake alipojaribu kumshawishi alikataa na kuondoka.
Baada ya miezi miwili kupita Bosco aliamua kumleta mchumba wake na kumtambulisha kwa wazazi wake, mwanamke huyu alikuwa anaitwa Tina ambaye alikuwa amemaliza elimu yake chuo kikuu cha Dar es salaam na sasa alikuwa katika harakati za kutafuta kazi. Wazazi wake walikubali kwa shingo upande kwani walikuwa hajaridhika na maamuzi ya mtoto wao. Na kwa upande wa Jeni alisikitika sana kwani siku zote alikuwa akiamini ipo siku atakuja kuolewa na Bosco.
Maisha yaliendelea wakiwa jijini Dar es salaam baada ya kufunga ndoa, Bosco alihamishwa kikazi, na kuhamia jijini Mwanza. Wakiwa huko mke wake aliendelea kuhangaika kutafuta kazi bila mafanikio. Bosco aliamua kumshauri Tina afanye biashara, wazo ambalo Tina alilikubali na Bosco alimpa mtaji mkubwa wa kuanza biashara. Alifungua Duka la vipodozi na sasa ilimpelekea kuanza kusafiri kwaajili ya kuja kununua mizigo ya dukani jijini Dar es salaam na wakati mwingine alikuwa akienda China. Siku zilivyozidi kwenda Biashara ilikuwa na hatimaye Tina alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa duka la vipodozi jijini Mwanza.
Maisha yalikuwa mazuri, Baada ya miezi michache Bosco alipata matatizo katika sehemu aliyokuwa anafanya kazi na kupelekea kusimamishwa kazi. Hivyo alikuwa nyumbani huku akihangaika kutafuta kazi sehemu nyingine. Kama unavyojua kutafuta kazi si lele Mama unaweza ukasota sana. Siku moja Bosco aliamua kuzungumza na mke wake ili waweze kushirikiana katika biashara. Mke wake alimsikiliza kwa umakini na kusema "Unajua unanishangaza sana Bosco, yaani mimi na wewe tufanye biashara pamoja, haiwezekani wewe endelea kutafuta kazi mimi nibaki na biashara zangu, kwani hazikuhusu hata kidogo yaani ni za kwangu peke yangu".
Bosco alibaki ameduwaa huku akifikiri labda mke wake alikuwa anatania "Embu acha utani mke wangu, mimi na wewe ni kitu kimoja, changu chako, na chako changu, na isitoshe mimi ndiye niliyekupa mtaji hadi biashara imesimama vizuri" Kwa dharau Tina alicheka na kusema "Hahahaha hivi huoni hata aibu, eti nilikupa mtaji, sikiliza nikuambia hapa ndani usipotafuta kazi hauna chako, na kuhusu biashara yangu usiingilie hata kidogo".
Alinyanyuka na kuondoka huku akimuacha mume wake akiwa ameduwaa, Maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wa Bosco kwani mke wake alikuwa hamsaidii kwa chochote ilifikia kipindi alikuwa anasafiri bila hata ya kumjulisha kuwa anakwenda wapi. Baadaye Tina alijigundua kuwa ni mjamzito, Bosco alifurahi sana kwani ijapokuwa na kero zote alizokuwa akizipata kutoka kwa mke wake lakini siku zote alikuwa akimpenda sana, miezi ilisogea na hatimaye alijifungua salama mtoto wa kiume.
Maisha yaliendelea huku Bosco akiwa anaishi kwa kumtegemea mke wake. Na kwa kipindi chote alikuwa akivumilia vituko vyote alivyokuwa anafanyiwa na mke wake. Siku moja Tina alikuwa ametoka na kwenda kazini huku akimuacha Bosco akiwa na mtoto nyumbani. Kwa bahati mbaya alisahau simu yake ya mkononi, Bosco aliiona na kuichukua, akiwa anataka kuiweka kwenye droo ghafla ujumbe ulitumwa, jina la aliyetuma lilikuwa limeandikwa (my darling) mpenzi wangu, alishangaa kuona jina hili na kuamua kuusoma ule ujumbe ambao ulikuwa umeandikwa "Mpenzi nimekukumbuka sana, sasa leo naomba uje na mtoto, halafu nachukia sana kuona mtoto wangu analelewa na mwanaume mwingine, fanya mpango umfukuze huyo mjinga wako hapo vinginevyo nitakuja kumchukua mtoto wangu".
Bosco alibaki akiwa anashangaa asiamini macho yake kile alichokuwa anakisoma, hasira zilimjaa na kuketi huku akiwaza "Inamaana huyu mtoto siyo wangu? Hivi Tina anaweza kunifanyia mimi hivi, inaniuma sana, na leo akirudi, ama zake ama zangu" Baadaye Tina alirudi haraka baada ya kugundua kuwa amesahau simu alipofika alimkuta Bosco ameishikilia simu na kusema "Nani kakuambia unifichie simu yangu, nipe simu yangu, sijui likoje" Bosco alikuwa amekasirika sana bila kuzungumza chochote alimnasa kibao Tina na kusema "Leo utanieleza huyu mwanaume aliyekutumia ujumbe ni nani, na huyu mtoto ni wa kwangu au laa" Tina alimtizama Bosco kwa dharau na kusema "Yaani wewe unanipiga mimi, sasa sikiliza huyu mtoto siyo wako na huyo aliyetuma ujumbe ndiyo Baba yake, na imekuwa vizuri umelifahamu hilo naomba uondoke hapa kwangu kwanza mimi ndiyo ninayetoa matumizi na kulipa kodi ya nyumba, kwahiyo fungasha virago vyako urudi kwenu".
Bosco aliishiwa nguvu na kujikuta machozi yakimbubujika katika paji la uso wake alitamani kumrukia Tina na kumpiga lakini alijizuia kwa kutuliza hasira zake. Siku hiyo hiyo alikusanya kila kitu chake na kuondoka huku akisikitika sana "Yalaiti ningewasikiliza wazazi wangu leo hii yasingenikuta, ni bora nirudi nyumbani nikaombe msamaha" Kesho yake alirudi Dar es salaam kwa wazazi wake ambao walisikitika sana kutokana na hali aliyokuwa anayo, walimsamehe, na Baba yake alimpa mtaji wa kufungua biashara huku akimtaka asahau yote yaliyotokea. Baada ya muda walionana na Jeni na Bosco alimuomba msamaha na hatimaye baadaye maisha yaliendelea kuwa mazuri na sasa Bosco aliamua kumuoa Jeni na waliishi maisha ya furaha pamoja na mtoto wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Unakaribishwa kutoa maoni yako.