Jumanne, Novemba 10, 2015

Madudu hospitali za serikali haya hapa.



Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akifanya ziara ya ghafla kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jana, imebainika kuwa tatizo la huduma za afya kwenye hospitali za umma ni miongoni mwa maeneo ambayo serikali yake italazimika kufanya kazi ya ziada ili kulimaliza kwani kumekuwa na madudu mengi yanayowasababishia kero wananchi.
 
Katika mikutano yake mingi ya kampeni, Dk. Magufuli alisema wazi kuwa miongoni mwa maeneo ambayo serikali yake itayavalia njuga ni kuboresha huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu yake, kuhakikisha dawa zinakuwapo, vifaa tiba na pia kuinuliwa kwa maslahi ya watumishi wa kada ya afya na watumishi wengine wa serikali.

 “Nitakayemteua kuwa Waziri wa Afya halafu hospitali zikose dawa (nchini) sitamchekea. Ataondoka siku hiyo hiyo,” alisema Dk. Magufuli katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
 
Uchunguzi wa Nipashe katika baadhi ya hospitali za umma jijini Dar es Salaam umebaini kuwa eneo mojawapo linalohitaji kufanyiwa kazi kubwa katika utoaji wa huduma za afya ni kwa wajawazito.
 
Inaelezwa kuwa kina mama wanaotarajia kuwa wazazi hukumbana na changamoto nyingi wakati wa kujifungua na kwamba, yeyote asiyekuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya huduma hiyo hupata wakati mgumu na pia kuwa katika hatari ya kupoteza maisha yeye, mtoto wake au wote wawili.
 
Katika uchunguzi huo uliohusisha pia rejea za ripoti mbalimbali, imebainika kuwa zipo changamoto nyingi wanazokumbana nazo wajawazito kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na pia muda mfupi baada ya kujifungua.
 
Baadhi ya kina mama waliozungumza na mwandishi wa gazeti hili wamedai kuwa baadhi ya kero kubwa wanazokumbana nazo katika hospitali za umma jijini Dar es Salaam ni pamoja na kuwapo kwa ulazima wa kujinunulia vifaa karibu vyote vya kujifungulia.
 
Kadhalika, lipo pia tatizo la mrundikano wa wajawazito kulinganisha na ukubwa wa wodi za kujifungulia na idadi ya vitanda; kuwapo kwa wauguzi (manesi) wanaonyanyasa wajawazito katika namna inayoashiria kutengeneza mazingira ya rushwa na pia kuwapo kwa idadi ndogo ya wauguzi isiyolingana na kina mama wanaofika hospitali kila uchao kupata huduma za uzazi.
 
“Hali ni ngumu kwakweli… gharama ziko juu kwa sababu kila mmoja hutakiwa kujinunulia vifaa vya kujifungulia na pia mara nyingi huwa kuna msongamano mkubwa kiasi cha kuzidi idadi ya vitanda vilivyopo wodini,” alisema mmoja wa kina mama aliyejifungua hivi karibuni katika Hospitali ya Mwananyamala iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 
Mmoja wa kina mama aliyejifungua hivi karibuni katika Hospitali ya Mwananyamala alitaja baadhi ya vifaa alivyoagizwa kuvinunua katika mduka ya dawa na kufika navyo wakati wa kujifungua kuwa ni kibanio cha kitovu cha mtoto, wembe wa kukata kitovu, mabomba zaidi ya matatu ya sindano, dawa ya kuzuia damu kutoka, gloves jozi 3 au zaidi, dripu moja ya vichocheo vya uchungu na mrija wa kutundikia dripu.
 
Aidha, imeelezwa kuwa mahitaji mengine anayopaswa kuwa nayo mama anayetaka kujifungua ni pamoja na kulipia mpira wa kulalia, gharama za kitanda na pia kiasi cha fedha, walau Sh. 60,000 kwa ajili ya kuwapa manesi ili kujihakikishia unafuu wa huduma kutoka kwao ikiwamo kupata huduma ya maji ya moto baada ya kujifungua na pia kuogeshewa mtoto.
 
Mahitaji kama hayo yanatajwa kuwapo pia katika vituo vya afya na hospitali nyingine za umma jijini Dar es Salaam zikiwamo za Amana, Mnazi Mmoja, Temeke, Mbagala, Magomeni na Sinza Palestina. Inaelezwa kuwa hali iko hivyo pia katika hospitali nyingine nyingi za umma nchini. 
 
GHARAMA KUBWA
Uchunguzi wa Nipashe katika kujua wastani wa gharama anazobeba kila mjamzito wakati wa kujifungua katika hospitali za umma jijini Dar es Salaam ikiwamo ya Mwananyamala umebaini kuwa ni takriban Sh. 115,700; kiwango ambacho huwashinda kina mama wengi wa hali ya chini. 
 
Imebainika kuwa kiwango hiki kinajumuisha gharama za aina mbili, ambazo ni vifaa vya kujifungulia vinavyogharimu takriban Sh. 55,700 na pia kiasi cha fedha walau Sh. 60,000 anachopaswa kuwa nacho mjamzito ili kuwapatia manesi wanaokuwa zamu na hivyo kujihakikishia unafuu katika huduma.
 
 “Siku hizi ukitaka ujifungue kwa amani kwenye hizi hospitali zetu kama Mwananyamala ni lazima uwe na walau Sh. 120,000… chini ya hapo utakuwa unajihatarisha wewe na mtoto kwa sababu unaweza usipate baadhi ya huduma muhimu,” anasema mmoja wa kina mama waliojifungua hivi karibuni katika hospitali ya Mwananyamala.
 
Katika baadhi ya maduka ya dawa na vifaa tiba, imebainika kuwa vifaa vinavyotakiwa kwa ajili kujifungulia huuzwa katika kitita kimoja kwa Sh. 41,000 na kwamba, vifaa vingine visivyokuwamo kwenye kitita hufanya jumla ya gharama zote kuwa walau Sh. 55,700.
 
Mchanganuo wa bei za vifaa hivyo vikiwamo vilivyomo kwenye kitita ni kibanio kitovu cha mtoto Sh. 500, wembe kukata kitovu cha mtoto Sh. 600, mabomba ya sindano Sh. 600, string injection Sh. 4,500, gloves jozi tano Sh. 17,500, dawa kuzuia damu kutoka Sh. 7,000, dripu moja ya  vichocheo vya uchungu Sh. 5,000, mpira wa kulalia, Sh. 10,000 na pamba kubwa Sh.10,000.
 
Kadhalika, ni muhimu kwa kila mzazi mtarajiwa kuwa na kiasi cha Sh.60,000 kwa ajili ya kuwapa manesi kwani watumishi hao hujikuta wakiwa na wagonjwa wengi kuliko idadi yao hospitalini na hivyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa mjamzito anapata uangalizi wa karibu ikiwamo kupata maji ya moto ni kuwa na fedha za ziada kwa ajili yao. 
 
Aidha, inaelezwa kuwa gharama za dripu za vichocheo vya uchungu hazitabiriki kwani zaweza kuongezeka kutegemeana na hali ya mjamzito kabla ya kujifungua.
 
Uchunguzi wa Nipashe umebaini vilevile kuwa bei ya vifaa vya kujifungulia hutofautiana pia kutokana na mahala duka lilipo na pia vifaa vilivyojumuishwa katika kitita kimoja chenye kuwekwa pamoja vifaa hivyo. 
 
“Maeneo mengi hizi dripu za uchungu, mrija wa kuitundika dripu hiyo pamoja na dawa ya kuzuia damu, hununuliwa katika hospitali husika au maduka yaliyo jirani na hospitali,” mmoja wa wazazi waliojifungua hivi karibuni katika hospitali mojawapo ya umma jijini Dar es Salaam aliiambia Nipashe.
 
Kadhalika, gharama hubadilika pia inapotokea mjamzito kutakiwa ajifungue kwa njia ya upasuaji.
 
Mama mmoja ambaye alijifungua kwa upasuaji hivi karibuni katika Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja, aliiambia Nipashe kuwa alinunua kitita chake cha vifaa vya kujifungulia kama alivyoelekezwa lakini alipofika hospitali na kubainika kwamba anahitajika kufanyiwa upasuaji, aliambiwa alipe Sh. 100,000 ya vifaa na huduma.
 
“Kwa hiyo kwenye kitita changu cha vifaa nilitumia pamba tu… baada ya kutoa Sh. 100,000 nilipata kila kitu,” alisema.
 
MALIPO YASIYO RASMI KWA MANESI
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa malipo haya yasiyo rasmi hutolewa kwa manesi ili mjamzito ajihakikishie kupata nafuu ya huduma. Inaelezwa kuwa mama akishajifungua salama, ndipo hupata huduma muhimu kama kuogeshwa na pia mtoto kupata huduma za awali kama kusafishwa. 
 
“Bila kutoa ‘mshiko’ kwa manesi, mtoto aweza kuachwa bila kusafishwa au kutosafishwa vizuri na pia mama kukosa huduma ya kuogeshwa maji ya moto,” kinasema chanzo kimoja.
 
Kadhalika, mtoto anapozaliwa akiwa na tatizo kama kuzaliwa akiwa na ugonjwa wa manjano, au labda akizaliwa bila kulia, fedha za malipo yasiyo rasmi kwa manesi husaidia zaidi. Kwamba, kama mjamzito hakujiandaa kuwa na fedha katika eneo hili, atajikuta akikosa huduma muhimu na mwishowe mtoto wake kuathirika zaidi au hata kupoteza maisha.
 
WAZIRI, WAGANGA MWANANYAMALA NA TEMEKE WANENA
Mmoja wa madaktari wanawake katika Hospitali ya Mwananyamala ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia Nipashe kuwa hospitali hiyo imezidiwa na idadi kubwa ya wajawazito na ndiyo maana hulazimika kuwataka wazazi watarajiwa kujiandaa kwa kujinunulia dawa na vifaa kwa ajili ya dharura.
 
“Mjamzito anapaswa kununua vifaa vyote muhimu kama pamba, kibanio cha kitovu cha mtoto na vingine kwa sababu mahitaji ni makubwa kuliko uwezo tulio nao,” alisema daktari huyo.
 
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani, alisema hospitali yao, kama zilivyo hospitali nyingine za umma, hutoa huduma ya kujifungua kwa kina mama bure kulingana na sera ya afya inavyoeleza, lakini changamoto kubwa waliyo nayo ni kuzidiwa na idadi ya kina mama wanaofika kwao kila uchao.
 
“Tunatoa huduma bure kwa watu wa makundi matano kama sera inavyoeleza, wakiwamo kinamama wajawazito. Lakini tunatoa huduma hizo kulingana na uwezo wa hospitali yetu. Mjamzito anayelazwa hapa tunampa kitanda, dawa na vifaa vingine ambavyo hutolewa bure, lakini kwakweli tumezidiwa uwezo,” alisema.
 
Aliongeza kuwa: “Mfano wa wazi, ni wodi ya kujifungulia (labor ward)… hii ina uwezo wa kuhudumia kina mama 15 wanaojifungua kwa wakati mmoja, na ambao kwa wastani hukaa wodini kwa saa nane hadi 12. Lakini kwa siku wanaojifungua hapa ni kina mama 100 hadi 120. Hapo utaona ni kwa nini nasema ukweli kuwa tumezidiwa, lakini tunajitahidi kutoa huduma bora kadiri ya uwezo wetu.”
 
Alisema wakati wa kliniki, wamekuwa wakitoa elimu ya afya kwa wajawazito na kuwashauri wajitayarishe kwa kununua vifaa muhimu vya kujifungulia kutokana na ukweli huo, kwamba hospitali yao imezidiwa uwezo.
 
“Tunawaambia mapema wanunue vifaa ili wakipata dharura waweze kuhudumiwa haraka popote pale panapotambuliwa, hata kama siyo hapa kwetu,” alisema.
 
Hali katika wodi ya wazazi kwenye Hospitali ya Amana inatajwa kuwa pia ni ngumu kwani imewahi kuripotiwa kuwa uwezo wao kwa siku ni kuhudumia wajawazito 21, lakini hupokea wastani wa wajawazito zaidi ya 100 kwa siku na hivyo wahudumu hupata wakati mgumu wa kukidhi matakwa ya wagonjwa wao, kwa maana ya huduma, dawa na vifaa tiba.
 
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema katika hospitali yao hakuna uhaba wa vifaa vya kujifungulia.
 
Jitihada za kumpata Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Grace Magembe ili azungumzie hali hiyo kwa hospitali za mkoa wake zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
 
Hata hivyo, akizungumzia hali hiyo, aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, aliiambia Nipashe siku moja kabla ya kuapishwa kwa Dk. Magufuli kuwa Rais wa Tanzania kuwa, uhaba wa dawa na vifaa kwa wajawazito hutokana na ufinyu wa bajeti.
 
“Hata nyumbani kwako kuna wakati bajeti haitoshi. Bajeti ya serikali ni hivyo hivyo,” alisema.
 
Aliongeza kuwa: “Kisera, huduma kwa wajawazito ni bure. Lakini sera ni jambo moja na utekelezaji ni jambo jingine… lakini niseme ukweli tu kwamba bajeti haitoshelezi.”
 
Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha kuwa kila mjamzito anakuwa na bima ya afya ili kumpunguzia mzigo wakati wa kujifungua, akieleza kuwa hivi sasa wameanza kufanya majaribio katika mikoa ya Tanga na Mbeya.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom