Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MY BOOK. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MY BOOK. Onyesha machapisho yote

Ijumaa, Januari 03, 2014

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

 
 ILIPOISHIA
Upendo akiwa sambasamba na Eliza alielekea sehemu ile kwenye umati
wa watu ambako James alifichwa ili akamfichue. James akiwa katikati ya
umati alimwona Upendo akiwa anatoka na pembeni akiwa na Esta
alishtuka sana kumwona Esta.
“Mungu wangu yule si Esta? Anafanya nini hapa na mbona yupo karibu
na Upendo? Kuna nini kinaendelea hapa?” James aliwaza na kujiuliza
maswali mengi yaliyokosa majibu.

INAPOENDELEA


Kwa muda wa takribani dakika mbili hivi James alikuwa kama mtu
aliyechanganyikiwa. Watu waliendelea kushangilia huku James akiwa hajui
nini cha kufanya baada ya kumwona Eliza ambaye ndio Esta akiwa
anatazama huku na kule kama vile mtu anayetafuta njia ya kutokea.
James akiwa anahangaika nini cha kufanya Upendo na Eliza waliendelea
kuangalia huku na kule wakimtafuta katika umati wa watu. Ghafla Eliza
akamwona Julias na kushtuka, lakini hakujua kama ndio mume mtarajiwa
wa dada yake.

“Haa! Hivi yule si Juliasi? Amefuata nini hapa? Au ni ndugu wa huyo
James? Mmh! Nina bahati kweli sikutarajia kumwona. Sasa hii ni nafasi
nzuri ya kuzungumza naye kuhusu hatima ya uhusiano wetu na hii mimba
yake.” Eliza alijiuliza maswali mengi huku akishangaa na kufurahi kuonana
tena na Juliasi. Zoezi la kumfichua James halikufanikiwa kwani Upendo
alishindwa kabisa kumwona James alipokuwa. Hivyo waliamua kurudi na
kukaa katika sehemu maalumu iliyotayarishwa kwa ajili ya Upendo.

Ijumaa, Desemba 27, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA "DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

ILIPOISHIA
 “Hivi nimefanya nini mimi huyu msichana ana mimba yangu na hataki
kuitoa na mimi nafunga ndoa hivi karibuni. Sijui itakuwaje ila ngoja
nimwache siwezi kumpoteza Upendo nampenda sana na ndio mke
wangu, sitaki mawasiliano na huyu mwanamke tena.”
Basi naye aliendelea na mambo yake huku akiwa anajiandaa na harusi
yake. Wakati huo Upendo alipanga safari ya kwenda Morogoro kwani
ilikuwa imebaki kama mwezi mmoja afanyiwe sherehe ya kuagwa na
wazazi wake

INAPOENDELEA

Baada ya wiki kadhaa kupita mawasiliano kati ya James na Esta yalikwisha
kwani kila Esta alipojaribu kupiga simu James alikuwa hapokei. Na
ikitokea amepokea alimtaka asiendelee kumpigia simu tena. Upendo
aliondoka na kwenda Morogoro kwa ajili ya kuandaa sherehe. Akiwa
Morogoro mdogo wake alikuwa bado yupo chuoni, hivyo wazazi wake
walimpigia simu na kumwambia ni lazima awepo kwenye sherehe ya dada
yake.

Zikiwa zimebaki kama wiki mbili kufanyika sherehe ya kumuaga Upendo,
Eliza alirudi Morogoro kwa wazazi wake ili kusherekea pamoja na dada
yake. Siku Eliza alipofika, wazazi wake hawakuwepo ila Upendo pekee.
Upendo alipomwona mdogo wake alifurahi sana, alimpokea begi wote
wakaingia ndani.

Jumatano, Desemba 04, 2013

ENDELEA KUPATA UHONDO, SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI-DADA YANGU
MTUNZI-ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa lakini baadaye ilipokelewa.
“He! We Eliza mbona umechelewa kupokea simu?” Aliuliza Upendo.
“Mh dada samahani nilikuwa bafuni, ehe niambie.” Alijibu Eliza.
“Ndugu yangu natamani ungekuja huku unisaidie katika mipango ya
harusi yangu vipi mnafunga lini chuo?” Aliuliza Upendo.
“Makubwa! Kweli mapenzi yamepamba moto ndio unaolewa na huyo
shemeji hata simjui jamani?” Alihamaki Eliza. ITAENDELEA

INAPOENDELEA
“Wewe nawe! Utakuja kumwona siku ikifika. Kwanza yupo huko Arusha
lakini ametingwa sana sijui kama mtaweza kuonana.” Alisema Upendo.
“Hee! Jamani kweli shemeji yangu yupo huku halafu huniambii? Vibaya
hivyo dada yangu, sasa kuhusiana na mimi kuja huko kukusaidia hiyo
mipango yako ya harusi kwa sasa itakuwa vigumu kwani najiandaa na
mitihani itakayoanza mwezi ujao.” Alijibu Eliza.

“Jamani Eliza mwenzio natamani ungekuwepo ila hakuna tatizo kwani
masomo nayo ni muhimu. Mh mdogo wangu hebu niambie sijapata
shemeji mmasai huko?” Aliuliza Upendo huku akicheka.
“Mmh! mwenzangu nimepata mchumba nampenda sana, mambo yakiwa
sawa nitakufahamisha.” Alijibu Eliza.
Basi waliendelea kuzungumza na baadaye kila mmoja aliendelea na
mambo yake.

James kipindi chote akiwa Arusha alikuwa akimsaliti Upendo na kustarehe
na Esta. Baada ya siku kadhaa kupita hatimaye siku za James kurudi Dar
es Salaam zilikaribia. Esta alimfuata James hotelini ili kuzungumza naye
kuhusiana na hatma ya uhusiano wao watakapokuwa mbali.
“Juliasi karibu utaondoka kwenda Dar hivi kweli utanikumbuka? Na jinsi
warembo walivyo wengi huko Dar?” Aliuliza Esta huku akimpapasa uso
James.

Jumatano, Novemba 27, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA


KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI- DADA YANGU

ILIPOISHIA
Nakuomba usinisaliti mpenzi, najua kuna wanaume wengi
wanakufuatafuata. Ziba masikio yako usisikie neno lolote kutoka kwa
mwanamume yeyote. Alitahadharisha James.
“Mmh we nawe kwa wivu, nakupenda sana siwezi kufanya hivyo hata
siku moja.” Alijibu Upendo. ITAENDELEA

INAPOENDELA 
Baada ya mazungumzo kila mmoja aliendelea na mambo yake.
Akiwa Arusha James alianza kufanya kazi zilizompeleka akiwa na marafiki
zake ambao ni wenyeji wa huko walizunguka sehemu mbalimbali ikiwa ni
wiki mbili tangu James aondoke Dar es Salaam. Siku hiyo ilikuwa ni siku
ya Ijumaa muda wa saa mbili usiku ambapo James na marafiki zake
walikwenda katika matembezi maeneo ya Sakina.
Walipofika huko walikunywa sana pombe huku wakiwa wanafurahi
pamoja wakati huo walikuwa Sakina Bar, waliendelea kunywa hadi ilipofika
saa tano usiku.

“Aisee washikaji kwa nini tusiende disko Triple A.” James aliyekuwa
ameshalewa aliwashauri wenzake.
“Swadakta! Hilo neno! Washikaji twendeni disko sijaenda siku nyingi sana
nadhani itakuwa safi sana.” Mmoja wao aliongea huku akionyesha ishara
ya kuondoka.

Jumatano, Novemba 13, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU -MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI -DADA YANGU

ILIPOISHIA
Baadaye James alikuja pale chumbani kwa Upendo bila taarifa, baada ya
kugonga mlango na kuruhusiwa kuingia alimkuta Grace akiwa amejilaza
kitandani akisoma gazeti.
“Habari gani dada!” Alisalimia James.
“Nzuri kaka karibu kiti.” Alijibu Grace.
“Asante dada. Aaahmm! Nimemkuta Upendo?” Aliuliza James huku
akitabasamu. “Ndiyo! Ila yupo nje amekaa chini ya mti mkubwa nyuma ya jengo hili.”
Alijibu Grace huku akiamka na kukaa vizuri kitandani.
“Haya asante hebu nimfuate.” Aliaga James na kuondoka. ITAENDELEA 

INAPOENDELEA
Upendo alikuwa amekaa kwenye kiti cha plastiki huku amegeukia uzio
unaozunguka hosteli akichezea tawi dogo la mti. Mara James alikuja
kimyakimya akitokea kwa nyuma na kumziba Upendo usoni bila ya yeye
kumwona akiwa amebeba chakula kwenye mfuko. Upendo alishtuka sana
katu asijue ni nani aliyemziba macho.

“Nani tena jamani? Mimi huwa sipendi michezo ya hivi.” Alilalamika
Upendo. “Usiogope Upendo ni mimi.” James alitoa mikono yake na kumbusu
Upendo. “Waoo! James mbona hukunipigia simu kunitaarifu kama unakuja?”
Aliuliza Upendo huku akisimama kupokea mfuko aliokuwa ameubeba
James. “Nimekuletea chakula cha mchana Upendo.” Alitamka James bila kujibu
swali aliloulizwa. “Mmh! Nilijua ni watu wameamua kunichokoza. Asante sana kwa
kuniletea chakula, umejuaje James kwani mpaka saa hizi sijala njaa inaniuma kweli. Ehee! umeniletea chakula gani?” Aliuliza Upendo. “Fungua uone.” Alijibu James.
“Ooh! Chipsi na kuku napenda sana chakula cha aina hii, vipi njoo basi
tule wote.” Aliongea Upendo kwa shauku huku akimalizia kufungua
mfuko.

Upendo alichukua maji ya chupa aliyokuwa nayo na kumwomba James
anawe mikono ili wale wote.
“Hapana mimi nimeshakula we kula tu usijali nimekuletea wewe.” Alijibu
James huku akipokea chupa ya maji ili kumnawisha Upendo.
Akiwa anaendelea kula Upendo alikuwa ana mawazo mengi sana juu ya
James.

Alhamisi, Novemba 07, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI-DADA YANGU

ILIPOISHIA
“Mimi na Upendo ni marafiki wakubwa sana na huyu binti ni msichana
ambaye anajiheshimu sana tokea nilipomfahamu, nimempenda sana
kutoka moyoni mwangu natamani awe mama wa watoto wangu. Kwa vile
sijawahi kumtamkia lolote juu ya suala la mapenzi kwa kipindi chote cha
kufahamiana kwetu, nahisi nikimdokeza tu pengine anaweza akachukia.”
Aliwaza James huku akitamani kumwambia Upendo kuhusu alilonalo
moyoni mwake.Zilipita siku kadhaa kila James akionana na Upendo akawa anataka
kumwambia lakini alikuwa anasita. Siku moja alipanga kumtoa Upendo
ili kwenda naye sehemu tulivu apate fursa nzuri na adimu ya kumwambiaUpendo juu ya mapenzi aliyonayo moyoni mwake. ITAENDELEA USIKOSE UHONDO WA SIMULIZI HII

INAPOENDELEA
Ilikuwa siku ya Ijumaa James aliyopanga kumtoa Upendo jioni yake
kwenda katika matembezi. Alipomweleza Upendo juu ya azima yake ya
kutoka naye alikubali bila pingamizi. Ilipofika jioni ya saa kumi na mbili
hivi James alikwenda Hosteli ya Mabibo na gari yake aina ya Benzi
kumchukua Upendo. Alipofika Hosteli block A chumba namba 228
alimkuta Upendo akiwa tayari amejitayarisha kwa ajili ya matembezi ya
jioni. Upendo alivalia vazi la kutokea jioni ambalo lilimkaa barabara
likionyesha vizuri jinsi Mungu alivyompendelea kimaumbile. Alipendeza
sana kiasi kwamba James alijiona ni mwanamume mwenye bahati kama
angefanikiwa kumpata kimapenzi.

James aliendesha gari kuelekea Sinza eneo liitwalo Madukani katika
Mgahawa uitwao “Fast Food and Take Away” ambao ulikuwa na utulivu na
hali ya hewa nzuri. Walichagua sehemu nzuri na kwenda kukaa pamoja.
James alimpa Upendo uhuru wa kuagiza chochote alichopenda kula na
kunywa. Waliletewa vinywaji na kuanza kunywa huku wakisubiri chakula.
Muda wote mapigo ya moyo wa James yalikwenda mbio akiwaza namna
ya kuanza kumwambia Upendo suala la mapenzi. Baada ya kama dakika
ishirini hivi za maongezi ya kawaida James aliamua kumwaga sera zake.
“Upendo umependeza sana leo hilo gauni ulilovaa limekupendeza sana.”
James alianza kwa kumsifia Upendo.

Alhamisi, Oktoba 31, 2013

SIMULIZI INAYOITWA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI- DADA YANGU
hii ni simulizi ya pili kutoka katika kitabu cha Malipo ni hapahapa baada ya simulizi ya kwanza.

Mapenzi ni kitu ambacho kina nafasi kubwa sana katika maisha
ya watu kote duniani. Mapenzi haya yanaweza kuleta furaha sana endapo
mtu atampata mtu sahihi ambaye atakuwa ni muwazi, mwenye mapenzi
ya kweli na kuheshimu uhusiano huo. Lakini mapenzi yanaweza kuleta
karaha au kukosa amani kabisa kama kutakuwa na migogoro ambayo
unakuta inasababishwa na kukosa uaminifu na kuleta ugomvi kati ya
wawili wapendanao. Mapenzi haya yanaweza yakasababisha ndugu
kugombana, marafiki kukosana na hata kuuana.
*****
Eliza na Upendo ni wasichana warembo waliozaliwa katika familia ya
kitajiri mkoani Morogoro. Wasichana hawa waliishi katika maisha ya
kifahari kutokana na Baba yao Mzee Bondi kuwa na uwezo mkubwa sana
kifedha. Mzee Bondi aliwapenda sana mabinti zake na alipenda wasome
kwa bidii ili baadaye waje kuwa na maisha bora. Eliza na Upendo walisoma
katika hali nzuri sana hadi kufikia elimu ya chuo, ambapo Upendo alikuwa
akisoma Chuo Kikuuu cha Dar es Salaam na Eliza Chuo cha Uhasibu
Arusha. Kutokana na masomo walitengana na kuonana mara chache
kipindi cha likizo.

Baadaye Eliza na Upendo walijikuta wakijiingiza katika uhusiano wa
kimapenzi wote wawili kwa kijana mmoja mtanashati aliyeitwa James bila
kujijua. Uhusiano wa kimapenzi kwa mwanamume mmoja ulileta
migogoro katika familia yao.
*********
Baada ya kumaliza Kidato cha Sita Upendo alipangiwa kwenda kuendelea
na masomo ya Chuo Mkoa wa Dar es Salaam. Baba yake alifurahi sana na
kumuahidi kuwa angempa zawadi nono kama angefanya vizuri akiwa
Chuo. Kabla ya kujiunga na chuo Upendo alifanyiwa sherehe kubwa ya
kumpongeza, ambayo ilihudhuriwa na watu wengi sana ndugu jamaa na
marafiki. Wakati huo mdogo wake Eliza alikuwa Kidato cha Sita kwani
walipishana mwaka mmoja tu na kwa jinsi walivyokuwa, walionekana
kama mapacha. Wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kwa watu ambao
walikuwa hawajawaona kujua mkubwa ni yupi na mdogo ni yupi.
Siku zilipokaribia za kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Upendo
alijiandaa barabara kwa ajili ya kuanza masomo ya Chuo. Siku moja kabla
ya kuondoka Mama na Baba yake walimwita na kuzungumza naye
mazungumzo ili kumwasa na kumpa ushauri.

Alhamisi, Oktoba 24, 2013

MWISHO WA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA. NDANI YA KITABU IKIWA NI SIMULIZI YA KWANZA KATIKA KITABU HIKI KILICHOBEBA SIMULIZI TATU TOFAUTI.

Kitabu hiki cha MALIPO NI HAPAHAPA kina simulizi tatu tofauti. baada ya simulizi hii itakujia simulizi  NYINGINE
ENDELEA KUPATA UHONDO. KWA ANAYEHITAJI KITABU TUWASILIANE KUPITIA della.media@ymail.com au 0752817444

ILIPOISHIA
 “Yuko wapi mama yangu, namtaka mama yangu.” Aliuliza Julieth huku
akilia na akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa.
Yule kaka hakumwelewa anachozungumza akabaki anamshangaa. Ghafla
Julieth alianguka chini na kuzimia. Yule kaka na Zubeda walisaidiana
kumnyanyua Julieth na kumwingiza ndani kisha wakamlaza chini huku
feni ikimpepea. Yule kaka akamuuliza Zubeda aliyekuwa amewabeba
watoto wa Julieth.
“Vipi huyu mwenzio ana matatizo gani?” Aliuliza yule kaka.  JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SIMULIZI HII HADI MWISHO WAKE

INAPOENDELEA
Zubeda akamwelezea kila kitu yule kaka ambaye ndiye mpangaji mpya
katika ile nyumba, alimwonea huruma sana Julieth. Baada ya Julieth
kuzinduka aliendelea kulia asijue nini cha kufanya kwa yote yaliyomkuta.
“Usijali Julieth nitakusaidia ulale hapa mpaka kesho. Karibu sana mimi
naitwa Baraka, Zubeda amenieleza matatizo yote uliyonayo pole sana.”
Aliongea Baraka ili kumfariji Julieth.
“Asante sana kaka Baraka.” Alishukuru Julieth.

Baraka alimtayarishia maji ya kuoga na baada ya kuoga Julieth alijisikia
vizuri sana kisha alipewa chakula. Muda wa kulala ulipofika Baraka
alimwonyesha Julieth chumba cha kulala akiwa na watoto wake Domina
na Dominiki.
Alipokuwa chumbani aliwaza mambo mengi sana huku moyoni akijilaumu
mwenyewe;

“Mimi ndio chanzo cha kila kitu, hivi kwa nini niliondoka na kumuacha
mama yangu wakati nilijua anaumwa?, Ewe mama popote ulipo naomba
unisamehe na wadogo zangu Joseph na Peter sijui wako wapi, maisha
yangu ni ya mateso siku zote kwa nini lakini? Sijui nitakwenda wapi. John
alinidanganya na kuniacha, sasa na mama nimempoteza mimi nitakuwa
mgeni wa nani?” Alilia kwa uchungu huku akiwaangalia watoto wake
waliokuwa wadogo sana wasioelewa chochote, baadaye akalala usingizi
mzito kutokana na uchovu wa mawazo na safari.

Jumatano, Oktoba 09, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA

SIMULIZI- MALIPO NI HAPAHAPA
KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
Julieth alirudi kwa mama Janeth na kumwelezea yote aliyokutana nayo.
Mama Janeth alisikitika sana na hakuwa na namna nyingine ya kumsaidia
zaidi ya kumpa nauli na pesa kidogo za matumizi ili arudi kwao Arusha;
“Julieth wewe nenda tu nyumbani ukamweleze mama yako hali halisi
kwani ukiendelea kuishi hapa utateseka sana na ipo siku huyo John
atakutafuta. Nakutakia kila la heri Mungu atakusaidia utawalea watoto
wako vizuri.” Mama Janeth alishauri.“Nashukuru sana mama Janeth kwa msaada wako, tangu siku nilipoumwa uchungu hadi sasa. Umekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Mimi nitakwenda nyumbani na hata huko nyumbani sijui wanaendeleaje kwani sijawasiliana nao kwa muda mrefu. USIKOSE MUENDELEZO WA SIMULIZI HII ITAENDELEA HADI MWISHO.

INAPOENDELEA
Kuna siku nilimpigia Mama simu ikawa haipatikani.” Mama Janeth akampa simu ajaribu kumpigia tena mama yake lakini haikupatikana. Julieth aliwaza moyoni mwake; “Jamani mama atakuwa ana matatizo gain? Labda simu itakuwa imepotea au imeharibika.”

“Julieth unaondoka watoto hatujawapa majina, mimi ningependa huyu
wa kiume aitwe Dominiki na huyu wa kike aitwe Domina au unasemaje.”
“Sawa hakuna shaka ni majina mazuri najisikia fahari nakufarijika sana
kwa wewe kuwapa majina watoto wangu kwani bila wewe pengine
wasingekuwepo.” Alijibu Julieth huku akiwa na mawazo mengi.

Waliendelea na mazungumzo wakala chakula cha usiku na muda wa kulala
ulipofika wote walikwenda kupumzika ili kesho yake asubuhi na mapema
Julieth aanze safari ya kwenda Arusha. Kesho yake asubuhi na mapema saa kumi na moja Julieth alijiandaa na kusindikizwa na mama Janeth hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi. Basi liitwalo Jordan liliwasili, waliagana harakaharaka na safari ilianza kuelekea Arusha.

Jumatano, Oktoba 02, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA.

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA
KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
“Pole sana rafiki yangu wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo, mimi
nitakusaidia ulale leo, halafu kesho uende tu nyumbani kwenu Arusha.
Nitakupa hela kidogo.” Mama Janeth alimwonea huruma na kumfariji.
“Asante sana mama Janeth kwani hapa nilipo sijui ningefanyaje.”
Alishukuru sana Julieth na kwenda kulala baada ya kuonyeshwa sehemu
ya kupumzika.. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE  MUENDELEZO WA SIMULIZI HII.

INAPOENDELEA
Usiku akiwa amelala mara akaanza kuumwa uchungu wa kujifungua,
wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba. Mama Janeth
alimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ambako alipelekwa moja kwa
moja chumba cha kujifungulia. Muuguzi wa zamu alimwambia mama
Janeth aende nyumbani na awahi kuleta chai asubuhi.

Julieth alijifungua salama watoto mapacha mmoja wa kike na mwingine
wa kiume. Mama Janethi alipokuja asubuhi alifurahi sana kuona mgonjwa
wake amepata watoto mapacha bila matatizo, aliwashukuru sana wauguzi
na kuwapa shilingi elfu ishirini kama shukurani na kwa furaha aliyokuwa
nayo. Julieth alijifungua kabla ya miezi tisa kutokana na misukosuko
aliyokumbana nayo. 

Hata hivyo Julieth ilibidi aendelee kukaa pale
hospitalini kwa muda wa miezi miwili huku akipewa huduma zote na
mama Janeth.
Baada ya miezi miwili Julieth aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alikaa kwa
mama Janeth kwa muda wa mwezi mmoja akiwa anamuhudumia ili apone
vizuri. Hali ya Julieth pamoja na watoto iliendelea kuwa nzuri.

Siku moja wakiwa wamekaa sebuleni baada ya kula chakula cha
jioni mama Janeth na Julieth walikuwa na maongezi kuhusu John.
“Hivi Julieth, kwa nini usirudi kwa John labda akikuona na watoto
atakupokea.” Alishauri mama Janeth.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom