Pages

Jumatano, Oktoba 02, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA.

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA
KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
“Pole sana rafiki yangu wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo, mimi
nitakusaidia ulale leo, halafu kesho uende tu nyumbani kwenu Arusha.
Nitakupa hela kidogo.” Mama Janeth alimwonea huruma na kumfariji.
“Asante sana mama Janeth kwani hapa nilipo sijui ningefanyaje.”
Alishukuru sana Julieth na kwenda kulala baada ya kuonyeshwa sehemu
ya kupumzika.. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE  MUENDELEZO WA SIMULIZI HII.

INAPOENDELEA
Usiku akiwa amelala mara akaanza kuumwa uchungu wa kujifungua,
wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba. Mama Janeth
alimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ambako alipelekwa moja kwa
moja chumba cha kujifungulia. Muuguzi wa zamu alimwambia mama
Janeth aende nyumbani na awahi kuleta chai asubuhi.

Julieth alijifungua salama watoto mapacha mmoja wa kike na mwingine
wa kiume. Mama Janethi alipokuja asubuhi alifurahi sana kuona mgonjwa
wake amepata watoto mapacha bila matatizo, aliwashukuru sana wauguzi
na kuwapa shilingi elfu ishirini kama shukurani na kwa furaha aliyokuwa
nayo. Julieth alijifungua kabla ya miezi tisa kutokana na misukosuko
aliyokumbana nayo. 

Hata hivyo Julieth ilibidi aendelee kukaa pale
hospitalini kwa muda wa miezi miwili huku akipewa huduma zote na
mama Janeth.
Baada ya miezi miwili Julieth aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alikaa kwa
mama Janeth kwa muda wa mwezi mmoja akiwa anamuhudumia ili apone
vizuri. Hali ya Julieth pamoja na watoto iliendelea kuwa nzuri.

Siku moja wakiwa wamekaa sebuleni baada ya kula chakula cha
jioni mama Janeth na Julieth walikuwa na maongezi kuhusu John.
“Hivi Julieth, kwa nini usirudi kwa John labda akikuona na watoto
atakupokea.” Alishauri mama Janeth.


“Mama Janeth John amebadilika sana si yule wa siku zile, amekuwa mkali
kama mbogo aliyejeruhiwa. Ninaogopa sana asijeniumiza na pengine hata
kuua wanangu.” Julieth alijibu.
“Hapana jaribu kwenda na watoto kwani anajua kuwa umeshajifungua
ingawa anaona aibu ataanza vipi kuja kuwaona.” Mama Janeth aliendelea
kutoa ushauri.


“Sawa! Hebu nijaribu kwenda na watoto kwani kama unavyosema
akiwaona watoto pengine atapunguza hasira.” Alijibu Julieth.
Huku akiwa amewabeba watoto wake aliondoka kuelekea kwa John.
Alipofika alikuwa na wasiwasi mkubwa akifikiria jinsi atakavyokabiliana
na uso wa John baada ya kuachana kwa takribani miezi mitatu. Alisogea
jirani, akagonga taratibu na kusubiri afunguliwe. Mara mlango ulifungulwa
na mwanamke mwenye uso wa kujiamini kisha akaanza kumsemesha
Julieth:

“Habari za leo dada! Alisalimia.
“Salama dada yangu! Habari za hapa?” Alijibu na kuuliza Julieth.
“Karibu dada nikusaidie nini?” Aliuliza bila hata kujibu swali aliloulizwa.
Julieth alishtuka sana na kuingiwa na hofu kubwa kumwona yule
mwanamke aliyefungua mlango;

“Samahani namuulizia John.” Yule mwanamke alimwangalia Julieth
kuanzia kichwani hadi kwenye vidole vya miguu, kisha akamkaribisha:
“Karibu ndani.” Alimkaribisha Julieth huku akitangulia ndani haraka bila
hata kuangalia nyuma. Julieth aliingia na kukaa katika sofa lililokuwa jirani
kabisa na mlango huku moyoni mwake akijiuliza: “Huyu mwanamke ni
nani?” Wakati huo yule mwanamke alikuwa amekaa katika sofa lililokuwa
karibu na mlango wa kuingia chumbani, huku mtoto wa kiume mwenye
umri kati ya miaka mitano na sita hivi akichezea kijigari kidogo.
Kwa takribani dakika tatu au nne hivi walibaki kimya huku kila mmoja
akimwangalia mwenzie kwa kuibia. Ghafla yule mwanamke alivunja
ukimya kwa kutaka kujua Julieth alikuwa na shida gani;

“Samahani dada unamtaka John wa nini?” Aliuliza yule mwanamke. Julieth
alitaka kumjibu lakini alisita. Baada ya dakika moja hivi Julieth alijipa ujasiri
mkubwa na kumweleza kilichomleta pale ndani, wakati huo John alikuwa
yupo chumbani asiyejua chochote juu ya nini kinachoendelea pale
sebuleni:

“Mimi ni mchumba wa John, nilikuwa naishi hapa na nimetoka hospitali
nimejifungua hawa watoto mapacha.” Alijieleza Julieth kwa ujasiri wa
kuigiza. Yule mwanamke alishtuka na kusimama ghafla huku ameshika
kiuno na kunyoosha shingo yake kama fisi aliyesikia harufu ya mzoga.
“Wewe dada! Unajua unachoongea? Una uhakika ni nyumba hii au
umekosea nyumba? Aliuliza na kuhoji yule mwanamke.

“Dada yangu sijakosea kabisa ni hapahapa.” Alijibu Julieth akiwa katika
hali ya kujiamini kidogo.
Yule mwanamke alimuangalia Julieth, akainama chini akitafakari jambo
kisha akaendelea kufoka;
“Hapa ni nyumbani kwangu, na huyo John unayemsema ni mume wangu.”
Huku akimnyooshea kidole yule mtoto aliyekuwa anachezea kijigari.
“Na yule pale ni mtoto wetu anaitwa Philipo. Je, huo uchumba wenu
mliufanyia mbinguni? Mbona wewe dada unanishangaza sana?” Aliendelea
kufoka.

“Kama wewe umezaa naye mtoto, mimi nimezaa naye watoto, nakuomba
niitie John niongee naye.” Alifoka Julieth huku akionyesha kujiamini zaidi
kuliko mwanzo.
Baada ya kuona Julieth anavyoongea kwa kujiamini yule mwanamke
alisimama haraka na kuingia chumbani akimwacha Julieth na watoto wake
pale sebuleni.
Julieth aliinama na kuwaza kitu; “Nakumbuka siku John aliponifukuza
alisema mke na mtoto wake wanakuja je, atakuwa ndio huyu? Nahisi kama
naota. Lakini ni kweli yamenikuta nitafanya nini mimi?” Julieth aliendelea
kuwaza na kujiuliza maswali yaliyokosa majibu.

Ni dhahiri yule mwanamke alikuwa ni mke wa John kwani alikuwa akiishi
Dar es salaam akiwa masomoni katika moja ya vyuo vikuu vilivyoko huko.
John alikuwa akisafiri mara kwa mara kumtembelea na sasa alikuwa
amerudi baada ya kumaliza masomo. Wakati huo wote John alikuwa
anaishi na Julieth huku akimdanganya kuwa alikuwa anasafiri kikazi kumbe
tayari alikuwa na mke aliyefunga naye ndoa pamoja na mtoto sasa sijui
Julieth atafanya nini.

Julieth aliendelea kukaa pale sebuleni akimsubiri John. Alitumia fursa hii
kukagua sebule yote. Alitazama ukutani na kuona picha kubwa ya harusi
iliyomwonyesha John akiwa na yule mwanamke aliyemkaribisha. Alishtuka
na kuishiwa nguvu huku machozi yakimtoka asiamini anachokiona.
Mara mlango wa chumbani ulifunguliwa ghafla huku yakisikika maneno
kama vile watu wanafokeana. John alitokeza huku yule mwanamke
akimfuata kwa nyuma na kumkuta Julieth;

“Nani kakuruhusu kuja hapa kwangu wewe mbweha mkubwa?” John
alifoka na kutukuna bila hata salamu. Kisha akamgeukia mama Philipo;
“Hivi mama Philipo umeanza kukaribisha vichaa humu ndani?” Aliendelea
kufoka John.
“Hapana mume wangu mimi huyu amekuja anakutafuta wewe kwani
unamfahamu vipi? Alihoji mama Philipo kwa upole tofauti na alivyokuwa
akiongea na Julieth.

“Huyu mwanamke ulipokuwa Dar es Salaam mke wangu, alikuwa ni
mfanyakazi wangu wa ndani hapa nyumbani. Mimi nilipokuwa nasafiri
alikuwa analeta wanaume hapa nyumbani taarifa nikawa nazipata. Baadaye
alikuja akapata mimba na kuanza kusambaza maneno mimi ni mume wake
nilimfukuza na nashangaa anataka nini tena hapa na pesa yake nilishampa
siku nyingi” Bila ya aibu na hata huruma alisema John huku akimtaka
Julieth na watoto wake waondoke na asirudi tena.

“Wewe! Wewe! John! Muogope Mungu ulinichukua kwetu Arusha na
kunidanganya kuwa unanipenda leo hii unaniona sifai. Eti kichaa! Baada
ya kunidanganya na kuniharibia maisha yangu leo unaniona kichaa.
Ungeniambia ukweli haya yote yasingetokea, kumbe ulikuwa una mke na
mtoto. Sawa! mimi nitaondoka ila Mungu ndiye atakayenisaidia nakutakia
maisha mema.” Alifoka Julieth kwa mfululizo bila hata kumpa John fursa
ya kujibu huku akibubujika machozi.
Wakati akizungumza maneno hayo mama Philipo alibaki kimya akitafakari
kisha akaungana na John kumshambulia Julieth;

“Hebu tuondolee kilio hapa ufanye uhuni wako upate mimba halafu uje
hapa na vitoto vyako nani akupokee, kamtafute baba wa watoto wako.
Unataka kunigombanisha na mume wangu toka mjinga wewe.” Alitamka
mama Philipo huku akimsukumiza Julieth na watoto wake nje. Julieth
alitoka akiwa analia sana.

Julieth alirudi kwa mama Janeth na kumwelezea yote aliyokutana nayo.
Mama Janeth alisikitika sana na hakuwa na namna nyingine ya kumsaidia
zaidi ya kumpa nauli na pesa kidogo za matumizi ili arudi kwao Arusha;
“Julieth wewe nenda tu nyumbani ukamweleze mama yako hali halisi
kwani ukiendelea kuishi hapa utateseka sana na ipo siku huyo John
atakutafuta. Nakutakia kila la heri Mungu atakusaidia utawalea watoto
wako vizuri.” Mama Janeth alishauri.

“Nashukuru sana mama Janeth kwa msaada wako, tangu siku nilipoumwa
uchungu hadi sasa. Umekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Mimi
nitakwenda nyumbani na hata huko nyumbani sijui wanaendeleaje kwani
sijawasiliana nao kwa muda mrefu. USIKOSE MUENDELEZO WA SIMULIZI HII ITAENDELEA HADI MWISHO.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

inackitisha,pole juliet

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom