Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SIMULIZI FUPI. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SIMULIZI FUPI. Onyesha machapisho yote

Jumanne, Januari 28, 2014

SIMULIZI FUPI "WIFI MTATA"


Alipomaliza chuo tu Justa aliolewa na Mfaume kijana huyu alikuwa ni mfanyabiashara,  ambaye alikuwa akimpenda sana Justa. Mfaume alikuwa akiishi na mdogo wake wa kike aliyekuwa anaitwa Leti kwa kipindi hicho Leti alikuwa bado anasoma chuo. Baada ya Justa kuolewa sasa alihamia na kuishi pamoja na mume na wifi yake, maisha yalikuwa mazuri kwani Mfaume alikuwa anampenda sana mke wake. Kwa kipindi hicho Justa alikuwa bado hajafanikiwa kupata kazi hivyo alikuwa ni Mama wa nyumbani huku akiwa anaendelea kutafuta kazi. 

Siku zote Mfaume alikuwa akiacha pesa za matumizi pale nyumbani na  alikuwa akimpa mdogo wake pesa hizo yaani hata pale mke wake alipokuwa na shida ilimbidi amweleze wifi yake kwani mume wake alikuwa akimpatia pesa zote za matumizi ya pale nyumbani mdogo wake.Hali ile ilikuwa inamuumza sana Justa na ndipo alipoamua kumwambia mume wake kuwa hapendezewi na tabia yake  lakini mwanaume huyo hakutaka kumsikiliza. Siku zilivyozidi kwenda Justa alikuwa anakosa amani kabisa katika nyumba yake kwani alikuwa hana uhuru wowote kutokana na kila kitu alikuwa akipewa wifi yake. 

Jumanne, Desemba 10, 2013

SIMULIZI FUPI "SAUTI YA TUNU" SIMULIZI HII NI MAALUMU KWA SIKU HII YA MAADHIMISHO YA KUPAMBANA UKATILI WA KIJINSIA

MTUNZI : ADELA DALLY KAVISHE

"Nyamaza kimya tena nisikusike ukizungumza chochote nitakuuwa leo" Ilikuwa ni sauti kali ya mume wake na Tunu aliyekuwa akiongea kwa jazba huku akiwa ameshikilia kisu mkononi na kuanza kumchana  Tunu mithili ya mtu anayekata nyama ya kwenda kuchoma" Tunu alikuwa analia kwa uchungu sana, na akijaribu kuomba msaada bila ya mafanikio.

Maisha ya Tunu baada ya kuolewa mwanzoni alikuwa akiishi kwa furaha. Lakini baadaye  maisha yalibadilika baada ya kupata ujauzito na kufanikiwa kupata mtoto mmoja, Ambaye baada ya mwaka mmoja Mtoto alifariki kutokana na kuugua homa kali sana. Baada ya mtoto kufariki Chachunda ambaye ni mume wa Tunu, alibadilika na kuwa mwenye hasira kila wakati, na mara zote alikuwa akimlaumu mke wake kuwa yeye ndiye chanzo cha mtoto wao kufariki.Tunu alipata mateso makali sana, kiasi kwamba alitamani kuondoka na kurudi kwao lakini wazazi wake walimshauri avumilie kwani angerudi nyumbani ingekuwa ni aibu kubwa sana kwa familia yao.

Alhamisi, Novemba 28, 2013

SIMULIZI FUPI "SIWEZI KUKUACHA"

MTUNZI - ADELA DALLY KAVISHE
"Nimechoka na kero za kila siku, sitaki kabisa yaani ni bora tu niondoke nirudi kwetu"  Stara Alikuwa anazungumza kwa sauti iliyoonyesha kuwa na uchungu sana kutokana na tabia za mume wake ambaye alikuwa anachelewa kurudi nyumbani na akirudi anakuwa amelewa sana. Hali hii ilikuwa inamuumiza sana Stara ambaye alikuwa anavumilia kwasababu alikuwa anampenda mume wake.

Maisha ya Stara na mume wake kabla ya kuingia kwenye ndoa yalikuwa ni maisha yaliyojaa furaha na upendo, lakini baada ya kuingia kwenye ndoa mambo yalibadilika, Kutokana na hali hiyo Stara alikuwa akiumia sana  ilifikia kipindi akawa anashindwa kuvumilia kutokana na tabia ya mume wake kumpiga,  na kuna wakati alikuwa akirudi amelewa usiku wa manane alikuwa akimlazimisha  Stara kuwa naye kimepenzi kwa nguvu hata kama Stara akisema anaumwa, yeye alifanya nguvu yaani alikuwa akimbaka mke wake kutokana na kumtaka kimapenzi kwa nguvu bila ya kumuandaa. Stara aliumia sana. 

Jumatatu, Novemba 18, 2013

SIMULIZI FUPI. SHEMEJI, SHEMEJI...........

Kwa wale ambao wamebahatika kuwa na wadogo wa kike. Kwanza ni furaha na inapendeza sana kuona ndugu wakipendana na kusaidiana katika mambo mbalimbali. Embu soma mkasa huu.

 Rabia alikuwa akiishi Singida lakini baadaye alihamia na kuishi Dar es salaam  ambapo aliolewa na mwanaume mmoja ambaye ni mfanyabiashara  jijini Dar es salaam, Kijana huyu alikuwa na uwezo mkubwa kifedha na hivyo alikuwa akimsaidia sana Rabia kwa kila alichokuwa anakihitaji.

 Baada ya miezi michache Rabia aliamua kumchukua mdogo wake wa kike na kuja kuishi naye jijini Dar es salaam,  Mdogo wake alikuwa amemaliza kidato cha nne kwa wakati huo. Maisha waliyokuwa wanaishi pale nyumbani Rabia alikuwa hapendi sana kutoka na kwenda katika sehemu ambazo ni za starehe lakini mume wake alikuwa akipendelea sana, hivyo Rabia alimtaka mdogo wake awe anaongozana na shemeji yake. Mdogo wake Rabia alikuwa ni binti mrembo sana, mwenye umbo na sura nzuri ya kuvutia,  na alikuwa akipendeza kwa kila aina ya vazi alilokuwa akivaa. 

Jumapili, Oktoba 06, 2013

SIMULIZI FUPI POMBE SI DAWA YA MAPENZI.

MTUNZI -ADELA DALLY KAVISHE

Jerome alikuwa na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa sana, Alikuwa ni kijana mchapa kazi na wakati wote alikuwa makini sana. Katika maisha yake alisema kamwe hawezi kuchanganya kazi na mapenzi. Kijana huyu alikuwa ni mkarimu mtanashati na mwenye mvuto wa hali ya juu, baadhi ya wanawake walikuwa wakitamani kuwa karibu naye lakini Jerome alikuwa na msimamo hakutaka kabisa kujiingiza katika suala zima la mapenzi.

Akiwa anaendelea  kazi zake ambapo kazi zote alikuwa akizifanya akiwa anaishi Mkoa wa Dodoma. Baadaye alianza kusafiri  na kwenda katika mikoa mbalimbali hususani Mkoa wa Dar es salaam ambapo alikuwa akikutana na wafanyabiashara mbalimbali.

Siku moja akiwa jijini Dar es salaam katika shughuli zake alikutana na dada mmoja ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa chuo na walifahamiana, na kisha kubadilishana namba za simu. Baadaye waliendelea na mawasiliano wakiwa kama marafiki na hatimaye baadaye Jerome aliamua kufungua ukurasa wa mapenzi katika moyo wake na sasa alimpenda sana binti huyu aliyejulikana kwa jina la Selina  makazi yake yalikuwa ni Dar es salaam, mara nyingi Jerome alikuwa akija Da es salaam na wakati mwingine huyu mchumba wake alikuwa akienda Dodoma mapenzi yalikuwa motomoto. Jerome aliamini kabisa kuwa Selina angekuja kuwa mke wake alijitolea kwa kila kitu yaani aliamua kumlipia ada ya chuo na matumizi mengine.

Jumamosi, Septemba 21, 2013

SIMULIZI FUPI MWISHO WA MATESO

MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE
Kwa muonekano anaonekana ni mtu ambaye  ni mcheshi na mwenye furaha wakati wote, lakini moyoni mwake analo jambo zito sana linalomsumbua, Joanita alikuwa ni msichana ambaye alijituma sana katika masomo yake na hatimaye alifaulu vizuri na kufanikiwa kumaliza elimu ya chuo kikuu. Baada ya kumaliza chuo alihangaika kutafuta kazi huku na kule bila ya mafanikio ilifikia kipindi alihisi kukata tamaa.

 "Eeh Mungu naomba unisaidie, nimehangaika sana bila ya mafanikio yoyote  sijui nitapata wapi kazi, embu ngoja niende nikanunue magazeti ya leo labda naweza kubahatika kupata nafasi ya kazi"Basi alitoka nje na kwenda kununua magazeti. Akiwa anasoma moja kati yale magazeti kulikuwa na tangazo la nafasi za kazi katika kampuni moja maeneo ya posta ambapo alikuwa anahitajika muhasibu. Na Joanita alikuwa amesomea kazi hiyo.

Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda hadi katika hiyo ofisi, alipofika alimkuta Mzee mmoja aliyekuwa anaitwa Mzee Njero, ambaye ndiye alikuwa anahusika na kitengo cha kuajiri. Alimwelezea shida yake na yule Mzee alimsikiliza kwa umakini. "Kupata Kazi siyo kazi ngumu mrembo, kwani kwa namna ninavyokuona wewe ni mpole na pia ni mrembo sana, sasa sioni sababu ya wewe kukosa kazi" Aliongea yule Mzee huku Joanita akimsikiliza kwa umakini. 

Ijumaa, Agosti 30, 2013

SIMULIZI FUPI: TAMAA IMENIPONZA

MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
Ritha alikuwa ni msichana mrembo sana,  kila aliyemtizama alivutiwa na urembo alionao, na hata yeye alijitambua kuwa ni mrembo. Katika maisha yake Ritha  alikuwa anapenda sana vitu vizuri na vinavyokwenda na wakati kama nguo, viatu, simu na vitu vingine kadha kwa kadha. Lakini wazazi wake walikuwa hawana uwezo wa kumnunulia vitu vyote hivyo.

 Baada ya kumaliza  kidato cha nne, kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuendelea na kidato cha sita na hivyo wazazi wake waliamua kumtafutia chuo.Akiwa  anasoma chuo alikutana na marafiki wa aina mbalimbali na marafiki zake wakubwa walikuwa ni wale ambao wametokea katika familia  ambazo wanajiweza yaani matajiri. Kutokana na wazazi wao kuwa na pesa walikuwa wakimiliki simu nzuri, na kompyuta (laptop) lakini kwa upande wa Ritha alikuwa hana hata simu ya mkononi, alitamani sana kuwa na maisha mazuri kama ya wenzake.

Siku moja akiwa anatoka chuo kuelekea nyumbani alikutana kaka mmoja aliyekuwa anaendesha gari aina ya Alteza "Mambo mrembo, unaelekea wapi mamii" Yule kaka alimwita Ritha huku akipunguza mwendo wa gari lake. Ritha alimtizama yule kaka na kusema "Hapana asante, nitapanda tu daladala" Yule kaka akaendelea kusema "Samahani lakini mrembo,nakuomba mara moja kuna jambo nilikuwa nataka nikuulize" Basi Ritha akasogea karibu "Uliza tu hakuna tatizo" Kumbe yule kaka alimwita kwa ukaribu ili ambembeleze apande kwenye gari yake. Haikupita muda Ritha alikubali kupanda kwenye lile gari na waliendelea kuzungumza na kufahamiana.

Yule Kaka alikuwa ni mfanyabiashara, anaitwa Godson.Kutokana na Ritha alikuwa hana simu ya mkononi Godson alimuahidi kumnunulia simu, na kesho yake angempelekea pale chuoni. Baada ya kumfikisha Ritha maeneo ya nyumbani, alimpatia kiasi cha shilingi elfu hamsini "Kiasi hiki kidogo cha pesa kitakusaidia, kwa nauli siku ya kesho, nimefurahi sana kukufamu Ritha, wewe ni mrembo ukinipa nafasi katika moyo wako, nakuahidi utafurahi sana" Ritha huku akiuma vidole vyake kwa aibu akapokea ile pesa na kusema "Asante sana Godson, ila naomba ukanishushe kwa pale mbele hapa Mama akiniona itakuwa balaa" Basi akasogea mbele kidogo na kumshusha.

Jumatano, Agosti 28, 2013

SIMULIZI FUPI "USIMDHARAU MTU KUTOKANA NA KIPATO CHAKE"

MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE
Kuna vijana walikuwa wamekaa kijiweni huku wakizungumza, ghafla akapita kijana mmoja anaitwa Sudi na aliwasalimia, huku akiwa anaendelea na safari yake kwa bahati mbaya aliteleza na kuanguka, lakini hakuna hata kijana mmoja aliyenyanyuka na kumsaidia wote waliangua vicheko na mmoja wao akisema "Huyu jamaa atakufa kwa mawazo, si anaishi hapo mtaa wa pili kwa ndugu zake yaani hawana chochote ni masikini sana kazi yao ni kuombaomba" Huku wakiendelea kumcheka. 

Sudi alinyanyuka na kuendelea na safari bila ya kuzungumza chochote huku machozi yakionekana kumlengalenga aliwaza moyoni mwake "Watu wengi wananidharau kutokana na hali duni ya maisha niliyonayo, eeh Mungu nisaidie" Pale kijiweni waliendelea kuzungumza "Unajua umasikini ni mbaya sana, kwani siku zote ukiwa masikini, basi ujue utapata shida sana, na ukizingatia yule aliyenacho ndiyo anazidi kuwa nacho." Mmoja kati ya wale vijana alikuwa anaitwa Frank alisimama na kusema "Hivi mbona mnadharau sana jamani, unajua usimdharau mtu usiyemjua kumbukeni kuna leo na kesho, na hakuna binadamu anayependa kuishi maisha ya shida, msikufuru jamani mshukuruni Mungu kwa kuwa nyinyi mna maisha mazuri, familia zenu ni matajiri lakini kumbukeni msitumie pesa kama fimbo ya kumchapia yule asiyenacho".

Jumapili, Agosti 25, 2013

KWAKO KIJANA SOMA STORY HII FUPI UPATE KITU.....


Siku moja punda wa mkulima alianguka
ndani ya kisima. Mnyama huyo alipiga
kelele kinyonge kwa masaa kadhaa wakati
mkulima akijaribu kufikiri nini cha kufanya.
Hatimaye, aliamua kwakuwa punda wake
alikuwa mzee, na pia kisima hicho kilihitaji
kufunikwa juu, Akaona hapakuwa na haja
ya kumtoa.
Akaita majirani zake wote waje kumsaidia.
Wao wote wakachukua makoleo na kuanza
kuchota taka kwa koleo na kuzitupia ndani
ya kisima. Mara ya kwanza, punda
aligundua nini kilikuwakinatokea akapiga
kelele kwa nguvu. Basi, ikawashanganza
wale watu punda aliponyamaza ghafla!
Baada ya kutupa taka kadhaa kwenye hicho
kisima. Huyo mkulima alishangazwa na kile
alichokiona. Kwamba kila koleo la taka
lililorushwa juu ya mgongo wa punda,
punda alikuwa akifanya kitu cha
kushangaza. Alikuwa akijitikisa ili taka
zimwagike chini huku akipiga hatua moja
kuja juu.
Kadri mkulima na majirani walivyoendelea
kutupa uchafu kwa koleo juu ya punda yule,
alizidi kutikisa mgongo wake na kupiga
hatua moja kuja juu. Muda mfupi baadae,
kila mtu alishangaa jinsi punda alivyozidi
kutokeza ndani ya kisima na kuja juu.

Ijumaa, Agosti 23, 2013

SIMULIZI FUPI "BORA KUKAA KIMYA"


MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

Mara nyingi nilikuwa nikimshauri sana Sara, kuachana na mpenzi wake kutokana na mpenzi wake huyo kuwa na tabia mbaya. Ambapo wakati mwingine alikuwa akimpiga sana. Siku hiyo nilikuwa nyumbani nimepumzika ghafla nilisikia mlangoni kuna mtu anabisaha hodi kwa nguvu. "Suzi, Suzi, naomba ufungue mlango John ananiuwa" Ilikuwa ni sauti ya Sara nilinyanyuka haraka na kufungua mlango Sara alionekana kuumia  maeneo ya usoni nilishtuka sana kumuona katika hali ile "Hee! Umepatwa na nini Sara, mbona hivyo kulikoni?" Nilimuuuliza huku nikimkaribisha ndani.

 Aliingia na kuketi lakini bado alikuwa analia kwa uchungu huku akisema "Yaani mimi kweli John ni wakunifanyia hivi,  wakati nimemfumania na mwanamke mwingine? Halafu ananipiga" Nilisogea na kuketi karibu huku niki mliwaza "Pole sana Sara, lakini kwanini anakupiga, kwa kosa lipi ulilomfanyia, huyu mwanaume ana kichaa heee! na wewe rafiki yangu mwanaume kama huyo hakufai ni bora uachane naye kabisa. Embu tizama  umemfumania halafu anakupiga,  usiwe mjinga kiasi hicho Sara wanaume wapo wengi, kama yeye anakuona wa nini, basi ajue kuna wengine wanafikiria watakupata lini. Mwanaume gani mshamba huyo usipoangalia ipo siku atakuvunja mguu".

 Niliongea maneno mengi huku nikimtizama Sara aliyekuwa anaendelea kulia akasema "Inaniuma sana, kwa jinsi ninavyompenda John, lakini sasa siwezi kuendelea kuwa naye bora tuachane kabisa". Na mimi nilikuwa namshauri asikubali kuendelea kuwa na uhusiano na John kutokana na ukatili anaomfanyia.

Tuliendelea kuzungumza huku nikimliwaza Sara, ilifika majira ya saa mbili usiku nikiwa naandaa chakula,  huku Sara akiwa ameketi sebuleni mara mlango ulifunguliwa kwa nguvu, na aliyekuwa amekuja muda huo alikuwa ni John, nilisogea na kuongea kwa sauti ya jazba "Umefuata nini hapa kwangu, naomba utoke nje, mwanaume muuaji wewe.Toka nje John sitaki kukukona hapa kwangu" Sara alikuwa ameketi huku akiwa amejiinamia bila ya kuzungumza chochote.

John alinitizama na kusema "Nimekuja kumchukua mpenzi wangu" Alisema John kwa kujiamini, nilicheka kwa dharau na kusema " Unanichekesha kweli wewe, eti nimekuja kumchukua mpenzi wangu, kama unampenda kweli kwanini unamsaliti na tena kama haitoshi unampiga" John hakunijibu chochote alimsogeleaa Sara na kumshika mkono "Darling (mpenzi) nakuomba twende nyumbani tukazungumze, nakupenda sana Sara" 

Jumatano, Agosti 14, 2013

SIMULIZI FUPI " SIJAPOTEZA FURAHA YANGU'

MTUNZI_ ADELA DALLY KAVISHE
Nilikuwa katika wakati mgumu sana, kwani hakuna aliyekuwa akinijali, lakini sikukata tamaa kwakuwa niliamini Mungu yupo pamoja nami. Kuna wakati nilijikuta nakata tamaa kutokana na watu wengi kunizungumzia maneno yasiyokuwa na ukweli wowote. Maisha yangu yalikuwa yamezungukwa na marafiki wengi ambao kwa kiasi kikubwa nilikuwa nikiwaonyesha upendo na kuwaamini kuwa ni watu wa muhimu sana katika maisha yangu, Lakini kumbe  haikuwa vile ninavyofikiria walikuwa wamejivika ngozi ya kondoo lakini mioyo yao ikiwa imejaa chuki juu yangu.
Katika Maeneo ya  Vijana Kinondoni jijini Dar es salaam  nilikuwa nikishi na  Mama yangu mkubwa, kwani sikubahatika kuishi na wazazi wangu Baba na Mama yangu walifariki nikiwa mdogo sana. Mama yangu mkubwa alinilea vizuri sana hadi nilipomaliza elimu yangu ya sekondari, na kufanikiwa kuanza  chuo cha uhasibu. Nikiwa chuoni nilikutana na marafiki mbalimbali.

 Saida alikuwa ni rafiki yangu kipenzi  pale chuoni. Siku moja nikiwa najisomea Saida alikuja na kusema "Rozi rafiki yangu, kuna jambo nataka kukuambia, lakini mwenzangu usije ukamwambia mtu yeyote kuwa mimi ndiye niliyekueleza jambo hili" Ilinibidi nishangae na kusema "Ni jambo gani hilo? Mbona unaniweka roho juu. "Maneno yameenea hapa chuoni, watu wanakusema sana vibaya, yaani sijui nianzie wapi kukueleza." Moyo wangu ulishtuka nikawa nimebaki nashangaa "He! Watu wananisema vibaya? Kwani mimi nimefanya nini? Mbona unanishangaza Saida embu kuwa muwazi uniambie ni kitu gani kinaendelea".

Jumatatu, Agosti 12, 2013

SIMULIZI FUPI "AKUFUKUZAYE AKUAMBII TOKA"


SIMULIZI FUPI_ AKUFUKUZAYE AKUAMBII TOKA
MTUNZI_ADELA DALLY KAVISHE


"Mbona umepauka sana, au haujapaka mafuta, mmmh halafu unanenepa sana siku hizi" Nilimtizama Ashura na kusema "Mbona mimi najiona nipo kawaida na pia nimepaka mafuta." Huku akicheka kwa dharau Ashura aliingia ndani na kuniacha nikiwa nimesimama kibarazani. Nilijiuliza maswali mengi kwanini Ashura ananicheka nilijitizama huku nikihisi labda nina kasoro yoyote katika mwili wangu lakini sikuiona. Basi nilimpuuza na kuendelea na safari yangu.


Mimi ni mzaliwa wa Morogoro katika familia ya watoto watatu, Baada ya kumaliza kidato cha sita nilipata nafasi ya kuendelea na elimu ya chuo kikuu Dar es salaam, Kutokana na hali halisi ya maisha ya nyumbani nilipotokea wazazi wangu walikuwa hawana uwezo, hivyo ilinibidi nimuombe rafiki yangu Ashura anisaidie hifadhi katika chumba alichokuwa amepanga karibu na maeneo ya chuo. Ashura alinikubalia na hivyo nilipata sehemu ya kuishi bila ya kutumia gharama yoyote.


Maisha yetu yalikuwa mazuri kwani tulipendana sana mimi na rafiki yangu Ashura, kiasi kwamba pale shuleni watu walikuwa wakituita mapacha, kwani mara nyingi tulikuwa tukiongozana kama kumbikumbi.Kwa kiasi kikubwa Ashura alikuwa akinisaidia sana, kwani ni msichana aliyetokea katika familia ya kitajiri. Binafsi nilikuwa naishi maisha ya kujinyima sana kutokana na hali halisi ya maisha yangu.

Jumatatu, Agosti 05, 2013

SIMULIZI FUPI 'NDUGU LAWAMA"


SIMULIZI FUPI_ NDUGU LAWAMA
MTUNZI _ADELA DALLY KAVISHE

"Asante sana shemeji Beni kwa msaada ulionipa, lakini nilikuwa naomba uniongezee kiasi cha shilingi laki tano tu, kuna jambo nataka kulifanya, nimepungukiwa kidogo, naimani utanisaidia". Alikuwa ni shemeji yangu ambaye ni kwa kipindi kirefu nimekuwa nikimsaidia kuendeleza biashara zake,  kwa wakati huo nilikuwa sina kiasi  hicho cha fedha "Ningependa kukusaidia shemeji lakini hali yangu kiuchumi kwa sasa imeyumba ila usiwe na shaka nitafanya mikakati ndani ya siku mbili tatu nitakupa hiyo pesa.lakini shemeji kuwa makini sana na utumiaji  wa pesa kwani kwa sasa pesa imekuwa ngumu kupatikana hivyo ni vyema ukawa makini sana katika biashara yako". Baada ya kumaliza mazungumzo shemeji alinielewa na kuondoka.

Kesho yake asubuhi ilikuwa ni siku ya jumamosi ambapo siku hiyo si kwenda kazini, alikuja dada yangu akiwa pamoja na mtoto wake mdogo wa kike.  "Habari za masiku dada, karibu sana" Dada alinitizama huku akisema "Kaka habari yangu si njema kwani hapa nilipo, nimekuja kwako nina shida  mtoto amerudishwa nyumbani kwasababu ya anadaiwa ada, sasa kaka naomba unisaidie shilingi laki tatu niweze kumrudisha  mjomba wako shule, yaani hapa nilipo sina mtu mwingine wa kumtegemea zaidi yako". 

Nilikuwa nimeketi  pale sebuleni huku nikiwaza na nafsi yangu "Mhhh hapa nilipo leo nimeamka nina shilingi elfu kumi na tano tu mfukoni mwangu sasa nitawezaje kumsaidia dada yangu" Nilimtizama dada na kusema "Daah, hali ni mbaya sana dada yangu, umenikuta sina pesa kabisa lakini embu subiri naweza kumkopa rafiki yangu kiasi hicho cha pesa ili mtoto aende shule." Nilimpigia simu rafiki yangu anaitwa Zuberi na kumuomba anikopeshe pesa kidogo, kwa bahati nzuri nilifanikiwa hivyo nilimpa kiasi kile cha fedha dada.

Ijumaa, Agosti 02, 2013

MDHARAU MWIBA, MGUU HUOTA TENDE





Hivi wewe kaka unahadhi gani ya kuwa na mwanamke kama mimi. Embu jiangalie vizuri kuanzia chini mpaka juu halafu unitizame na mimi yaani huendani na mimi hata kidogo. Sulea Alikuwa akiongea kwa sauti kali sana huku akibidua midomo yake na kucheka kwa dharau.Kijana Vale alinyamaza kimya huku akionekana kuona aibu sana.Kwasababu palikuwepo na mkusanyiko wa watu eneo lile.


Akaamua kuomba samahani "Nisamehe Sulea, sikujua kama mimi kukutamkia nakupenda ingeleta tatizo kiasi hiki.Ni kweli mimi na wewe hatuendani asante sana nakutakia maisha mema" Aliongea Valle na kuondoka huku Sulea akiendelea kumrushia maneno "Kwenda zako kapuku mkubwa wewe,huna jeuri ya kumtunza mwanamke kama mimi, hahahaha usione vyaelea ujue vimeundwa, nenda katafute kapuku mwenzio.


Watu waliokuwepo pale wengine walicheka na baadhi wakionekana kusikitika sana "Mmh huyu mwanamke ana dharau jamani, halafu ana kauli chafu sana".

Alhamisi, Agosti 01, 2013

SIMULIZI FUPI ...YALAITI NINGELIJUA...... NI SIMULIZI INAYOISHIA PAPO HAPO.



MTUNZI ...ADELA DALLY KAVISHE


  Nilijaribu kumuita lakini hakuniitikia na hata nilipomsogelea aliendelea kutembea bila ya kusimama. Nilijisikia vibaya sana, kwani nilijiona nimedharaulika. Hata watu waliokuwepo karibu walinitizama kwa nyuso za kuonyesha kuwa wananionea huruma. Nilibaki nikizungumza na nafsi yangu. "Hivi ni kweli Lema anaondoka na kuniacha, hapana siwezi kuamini nilimuamini kwa moyo wangu wote". 

Nilibaki nalia huku nikijisemea na moyo wangu "Ama kweli dunia hadaa, ulimwengu shujaa na asiyesikia la mkuu huvunjika mguu. Leo hii naumbuka kwa yote haya yaliyotokea katika maisha yangu, lakini mbona sijui kosa langu, inamaana ni kweli amenibadilikia kwa kiasi hiki. Lakini nakumbuka watu wengi walinikanya kuhusu tabia ya Lema lakini mimi nilikuwa nafanya mambo yangu kwa siri sana. 

Tizama sasa nabaki naumia na kuteseka peke yangu. Maisha yangu yote nilimuamini mwanaume huyu. Ndugu, jamaa na marafiki walinikanya lakini nilihisi labda wananione wivu leo hii najuta kwani siamini kama kweli Lema amenitendea yote haya. Alikuwa amejiinamia chini Salima huku akilia kwa uchungu. Maumivu makali moyoni mwangu eeh Mungu nisaidie.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom