Jumamosi, Septemba 21, 2013

SIMULIZI FUPI MWISHO WA MATESO

MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE
Kwa muonekano anaonekana ni mtu ambaye  ni mcheshi na mwenye furaha wakati wote, lakini moyoni mwake analo jambo zito sana linalomsumbua, Joanita alikuwa ni msichana ambaye alijituma sana katika masomo yake na hatimaye alifaulu vizuri na kufanikiwa kumaliza elimu ya chuo kikuu. Baada ya kumaliza chuo alihangaika kutafuta kazi huku na kule bila ya mafanikio ilifikia kipindi alihisi kukata tamaa.

 "Eeh Mungu naomba unisaidie, nimehangaika sana bila ya mafanikio yoyote  sijui nitapata wapi kazi, embu ngoja niende nikanunue magazeti ya leo labda naweza kubahatika kupata nafasi ya kazi"Basi alitoka nje na kwenda kununua magazeti. Akiwa anasoma moja kati yale magazeti kulikuwa na tangazo la nafasi za kazi katika kampuni moja maeneo ya posta ambapo alikuwa anahitajika muhasibu. Na Joanita alikuwa amesomea kazi hiyo.

Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda hadi katika hiyo ofisi, alipofika alimkuta Mzee mmoja aliyekuwa anaitwa Mzee Njero, ambaye ndiye alikuwa anahusika na kitengo cha kuajiri. Alimwelezea shida yake na yule Mzee alimsikiliza kwa umakini. "Kupata Kazi siyo kazi ngumu mrembo, kwani kwa namna ninavyokuona wewe ni mpole na pia ni mrembo sana, sasa sioni sababu ya wewe kukosa kazi" Aliongea yule Mzee huku Joanita akimsikiliza kwa umakini. 


"Nitashukuru sana kama nitafanikiwa kupata kazi kwani nimekwishahangaika sana bila ya mafanikio" Aliongea Joanita kwa sauti ya upole na Mzee Njero alicheka kidogo na kusema "Unajua ukiwa unatafuta kazi inakubidi, uwe mvumilivu na ukubaliane na changamoto zozote unazokutana nazo,na ndiyo maana wahenga wanasema mtaka cha uvunguni sharti ainame. Sasa Joanita mimi nitakusaidia utapata kazi usiwe na wasiwasi vyeti vyako nimeviangalia vizuri sana, una vigezo vyote vya kufanya kazi katika kampuni yetu. Wewe nenda nyumbani halafu nitakupigia simu, usiwe na shaka kabisa kazi umepata".

Joanita aliondoka akiwa na furaha sana, kwani moyoni alikuwa na matumaini makubwa kuwa amepata kazi. Baadaye jioni majira ya saa moja, yule Mzee alimpigia simu Joanita na kumwambia kuwa waonane maeneo ya Sinza Golden Park Hotel, huku akimsisitiza kuwa waonane kwani kuna jambo angependa kumwelekeza ili aweze kufanikiwa kupata kazi. Kutokana na Shida aliyokuwa nayo Joanita hakusita kwenda kuonana na Mzee Njero.

Moja kwa Moja Joanita alielekea maeneo ya Sinza Golden Park. Alipofika aliangaza macho huku na kule na hatimaye alimuona Mzee Njero alipokuwa ameketi. Huku akitabasamu Mzee Njero alimkaribisha Joanita. "Karibu sana, mrembo, karibu uketi, ngoja nimuite muhudumu, sijui ungependa kutumia kinywaji aina gani, bia, mvinyo au soda jisikie huru  kwa chochote utakachokipenda." Joanita alikuwa amejiinamia kama mtu anayetafakari jambo na kusema "Asante sana , maji ya kunywa tu yanatosha" Mzee Njero akasema "Hapana Joanita yaani maji tu, haiwezekani ngoja akuletee angalau na soda." Alisisitiza Mzee Njero na muhudumu alikwenda kuleta vinywaji na mazungumzo yakaendelea.

Huku akimtizama kwa shauku la kutaka kujua ni kitu gani Mzee Njero alikuwa anataka kumuelekeza Joanita akasema "Naomba unisaidie nifanikiwe kupata kazi,Baba yangu, nimeteseka sana, uliniambia kuna jambo unataka kunielekeza?" Aliuliza Joanita huku Mzee Njero akiwa ametulia tuli akimtizama Joanita kuanzia chini mpaka juu kwa macho ya matamanio. "Unajua nimesahau, kukusifia, leo umependeza sana Joanita, nashangaa unavyosema unateseka, unajua wewe ni mrembo sana" Joanita aliguna kidogo bila ya kujibu chochote Mzee Njero akaendelea kusema "Kuhusu kazi usiwe na wasiwasi mimi nitakusaidia ila nilikuwa naomba na wewe unisaidie jambo yaani tusaidiane" Joanita akasema "Mmmh mimi sina chochote Mzee wangu, nitakusaidia nini?" Mzee Njero akacheka kidogo "Inamaana haunielewi Joanita, mimi nakuhitaji kimapenzi, unipe mahaba motomoto, nijisikie raha  halafu itakuwa rahisi kwako kupata kazi".

 Joanita alimtizama Mzee Njero kwa kumkazia macho huku moyoni mwake akiwaza "Yaani huyu Mzee si analingana na Baba yangu jamani, hivi kwanini mtu anashindwa kukusaidia bila ya kutaka rushwa jamani haya mambo nakutana nayo kila kukicha, eeh Mungu mateso haya hadi lini."Akiwa anawaza kwa sauti iliyojaa jazba akasema "Hivi wewe Mzee una akili kweli, unajua nilikuwa nakuheshimu sana kwa muonekano wako lakini kumbe nia yako ni kunitaka mimi kimapenzi? Hapana mimi siwezi na tena hiyo kazi siitaki kama ni kwa njia hiyo ya rushwa ya ngono" Mzee Njero akacheka kwa dharau na kusema "Ohoo ndiyo maana haupati kazi, hivi unafikiri kupata kazi ni jambo rahisi, sasa sikiliza mimi sina msaada na wewe tena endelea na maisha yako ila ujue nilikuwa na nia ya kukusaidia kabisa." Joanita alinyanyuka kwa hasira na kuondoka.

Baada ya wiki mbili kupita aliendelea kuhangaika kutafuta kazi ndipo alipofika katika ofisi moja maeneo ya Kinondoni, na kukutana na Dada mmoja aliyeitwa Recho. katika ile ofisi Joanita alifanikiwa kupata kazi lakini kwa masharti kutoka kwa Dada Recho ambaye ndiye alikuwa katika kitengo cha kuajiri. "Joanita mimi nitakusaidia upate kazi, ila inabidi tusaidiane, mshahara wako wa kila mwisho wa mwezi tutakuwa tunagawana nusu kwa nusu kwa muda wa mwaka mmoja, baada ya hapo nitakuachia uendelee kupokea wote" Joanita hakuwa na namna zaidi ya kukubaliana na Recho. Na mshahara aliokuwa anatakiwa kupokea ilikuwa ni shilingi laki tano kwa mwezi, kwahiyo walikubaliana na Recho watagawana mshahara huo nusu kwa nusu, kila mwezi kwa muda wa mwaka mmoja Joanita atakuwa anapokea laki mbili na nusu tu.

Maisha yaliendelea huku Joanita akiwa anafanya kazi kwa bidii,  na akimsikiliza Recho kwa kile alichokuwa anakitaka. Baada ya miezi mitano Alikuja Mkurugenzi wa kampuni na kumuita Joanita "Habari yako Joan nimependa sana unavyofanya kazi kwa bidii, sasa nafikiria kukupandisha cheo" Joanita alifurahi sana na kusema "Asante sana boso kwani mshahara huu wa laki mbili na nusu haunishi kabisa katika kuendesha maisha yangu." Yule bosi akashangaa kusikia laki mbili na nusu "Hee si unapokea shilingi laki tano? Mbona unasema laki mbili na nusu." Basi Joanita hakuwa na namna ilimbidi amweleze ukweli Mkurugenzi wake makubaliano yake na Recho aliyekuwa katika kitengo cha kuajiri. Yule bosi alisikitika sana, na hatimaye Recho alisimamishwa kazi kutokana na kuomba rushwa na Joanita alipandishwa cheo kutokana na juhudi zake za kazi. "Asante sana, Mungu nimeteseka kawa muda mrefu lakini  sasa nafurahi. MWISHO WA MATESO

KATIKA MAISHA, UNAWEZA KUKUTANA NA CHANGAMOTO NYINGI SANA LAKINI UNATAKIWA KUWA MVUMILIVU NA USIKATE TAMAA, UNAAMBIWA MVUMILIVU HULA MBIVU.


Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

yani ths story ipo kama yangu tu tho mm bado kupata kazi ila naamin siku yangu itafika kwani mungu yupo na mimi na kila jambo na wakati wake!!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom