Jumatano, Agosti 14, 2013

SIMULIZI FUPI " SIJAPOTEZA FURAHA YANGU'

MTUNZI_ ADELA DALLY KAVISHE
Nilikuwa katika wakati mgumu sana, kwani hakuna aliyekuwa akinijali, lakini sikukata tamaa kwakuwa niliamini Mungu yupo pamoja nami. Kuna wakati nilijikuta nakata tamaa kutokana na watu wengi kunizungumzia maneno yasiyokuwa na ukweli wowote. Maisha yangu yalikuwa yamezungukwa na marafiki wengi ambao kwa kiasi kikubwa nilikuwa nikiwaonyesha upendo na kuwaamini kuwa ni watu wa muhimu sana katika maisha yangu, Lakini kumbe  haikuwa vile ninavyofikiria walikuwa wamejivika ngozi ya kondoo lakini mioyo yao ikiwa imejaa chuki juu yangu.
Katika Maeneo ya  Vijana Kinondoni jijini Dar es salaam  nilikuwa nikishi na  Mama yangu mkubwa, kwani sikubahatika kuishi na wazazi wangu Baba na Mama yangu walifariki nikiwa mdogo sana. Mama yangu mkubwa alinilea vizuri sana hadi nilipomaliza elimu yangu ya sekondari, na kufanikiwa kuanza  chuo cha uhasibu. Nikiwa chuoni nilikutana na marafiki mbalimbali.

 Saida alikuwa ni rafiki yangu kipenzi  pale chuoni. Siku moja nikiwa najisomea Saida alikuja na kusema "Rozi rafiki yangu, kuna jambo nataka kukuambia, lakini mwenzangu usije ukamwambia mtu yeyote kuwa mimi ndiye niliyekueleza jambo hili" Ilinibidi nishangae na kusema "Ni jambo gani hilo? Mbona unaniweka roho juu. "Maneno yameenea hapa chuoni, watu wanakusema sana vibaya, yaani sijui nianzie wapi kukueleza." Moyo wangu ulishtuka nikawa nimebaki nashangaa "He! Watu wananisema vibaya? Kwani mimi nimefanya nini? Mbona unanishangaza Saida embu kuwa muwazi uniambie ni kitu gani kinaendelea".

Saida aliguna kidogo nakusema "Rafiki yangu, hivi  ni kweli una uhusiano wa kimapenzi na mwalimu  wa hesabu. Mr Ngowi, ndiyo maana unafaulu vizuri somo lake?" Ilinibidi niweke daftari langu pembeni na kusema "Eti nini Saida, kina nani wanasema hivyo, jamani mbona watu wanapenda kuzungumza maneno ya uongo, mimi sina uhusiano wowote na mwalimu Ngowi" Saida akacheka nakusema "Basi watu wengi hapa chuo wanajua ni kweli na anayesambaza hayo maneno ni Lina, ila chonde chonde usije kunitaja" Nilijisikia vibaya sana siku hiyo kwani ukweli ni kwamba sikuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu.

Siku zilivyozidi kwenda maneno yaliendelea na Saida alikuwa akija na kunieleza maneno ambayo yanzungumzwa kuhusu mimi. Nilivumia hali hiyo bila yakumuuliza mtu yeyote kwani nilikuwa sipendi ugomvi.Siku ya jumamosi na jumapili mara nyingi nilikuwa nikienda kushinda nyumbani. Ilikuwa ni jumamosi moja ambapo nilienda nyumbani na kumkuta mama yangu mkubwa akiwa amekasirika sana. Nilimsalimia lakini hakuniitikia jambo ambalo niliona siyo la kawaida.

 Nilijaribu kumsalimia tena ndipo aliponyanyuka na kunipiga kibao katika paji la uso wangu " Wewe mwendawazimu, mimi nakulipia ada, halafu unaenda kufanya mambo ya ajabu chuoni, hivi wewe ni mtu wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu wako? Tena nimesikia  huwa haulali chuoni kila siku unakuja kuchukuliwa na wanaume tofauti, yaani unabadilisha wanaume kama nguo. Hivi hii tabia ya ukahaba umeipata wapi?" Nilibaki nimeduwaa huku nikmisema "Hapana Mama mimi sina tabia hiyo, siwezi kufanya hivyo, unanionea Mama" Nililia kwa uchungu kwani Mama aliendelea kunigombeza huku akinipiga makofi ya usoni bila ya kunisikiliza. 

Maisha yangu yalikosa furaha kwani kila kukicha yalikuwa yakiibuka mambo tofauti, lakini sikujua nani ambaye anaweza kunifanyia yote haya. Kwani moyoni mwangu nilikuwa najua sikuwahi kumkosea mtu yeyote.

 Baada ya wiki mbili huku nikiwa sina maelewano mazuri na familia yangu.Siku hiyo nilikuwa chumbani nimepumzika pale chuoni alikuja Lina huku akiwa na kikosi cha marafiki zake. "Tumechoshwa na maneno yako, Rozi wewe mwanamke ni mnafki sana, kwanini unapenda kutufuatilia maisha yetu, unanisema vibaya kwa watu kuwa mimi na uhusiano wa kimapenzi  na walimu, eti  ndiyo maana nafaulu vizuri, ukaona haitoshi ukaenda kumwambia mpenzi wangu mimi namsaliti. Kwanini unanifuatilia au unamtaka mpenzi wangu?". Aliongea Lina kwa sauti ya jazba.

 Nilinyanyuka pale kitandani na kuuliza "Mbona siwaelewi, Eti unasema mimi nakusema vibaya, hivii  unajua unanishangaza wewe Lina yaani wewe unavyonizungumzia mimi vibaya, unampelekea maneno ya uongo hadi Mama yangu mkubwa, umeona haitoshi unataka kunisingizia mimi nakusema vibaya." Baada ya mimi kusema hivyo wote walinyamaza kimya kwa muda huku wakitazamana, mmoja wao akauliza "Nani amekuambia hayo maneno, acha uongo Lina hajawahi kukusema vibaya" 

Kutokana na hasira nilizokuwa nazo kwa wakati huo niliamua kumtaja Saida, ndipo wote wakabaki wakishangaa kumbe Saida huyohuoyo ndiye aliyekuwa anawapelekea maneno kwamba mimi namzungumzia vibaya Lina. Kwa wakati huo Saida alikuwa hayupo tulimsubiri  hadi aliporudi na sasa kila mmoja alimvamia kwa maneno makali huku wakimwimbia kwa tabia yake mbaya ya kusema uongo na kuchonganisha watu. Nilijisikia vibaya sana kwani mtu niliyemuamini kama rafiki yangu ndiyo alikuwa na nia ya kunichonganisha na marafiki hadi familia yangu. Aliniomba msamaha, mwanzoni ilikuwa ni vigumu kumsamehe lakini baadaye niliamua kumsamehe na maisha yanaendelea SIJAPOTEZA FURAHA YANGU.

Kuwa makini, usiamini maneno yote unayoambiwa, na mtu yeyote yule ni vyema kuchunguza ili kuwa na uhakika wa kile ulichoambiwa vinginevyo unaweza kugombana na watu kwa jambo lisilokuwa na ukweli. wahenga wanasema KIKULACHO KI NGUONI MWAKO. 

WADAU BADO NAWEKA MAMBO SAWA ILI MUENDELEE KUSOMA SIMULIZI YA BADO MIMI NA KOSA LANGU NI LIPI NAOMBA UVUMILIVU WENU KIDOGO.

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

yaan mi bado naisubir kwa ham "bado mimi na kosa langu nilipi.

Unknown alisema ...

Nice story hata mimi yashanikuta hayo.
By de way poa kwa udhuru huo nitasubiri mana nina hamu ya kujua mwisho wa Bado Mimi!!
Kazi nzuri Adela

Bila jina alisema ...

wanasema mvumlivu hula mbivu; lakini uvumilivu ukizidi mhh................
cjui atakula nini

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom