Pages

Ijumaa, Agosti 30, 2013

SIMULIZI FUPI: TAMAA IMENIPONZA

MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
Ritha alikuwa ni msichana mrembo sana,  kila aliyemtizama alivutiwa na urembo alionao, na hata yeye alijitambua kuwa ni mrembo. Katika maisha yake Ritha  alikuwa anapenda sana vitu vizuri na vinavyokwenda na wakati kama nguo, viatu, simu na vitu vingine kadha kwa kadha. Lakini wazazi wake walikuwa hawana uwezo wa kumnunulia vitu vyote hivyo.

 Baada ya kumaliza  kidato cha nne, kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuendelea na kidato cha sita na hivyo wazazi wake waliamua kumtafutia chuo.Akiwa  anasoma chuo alikutana na marafiki wa aina mbalimbali na marafiki zake wakubwa walikuwa ni wale ambao wametokea katika familia  ambazo wanajiweza yaani matajiri. Kutokana na wazazi wao kuwa na pesa walikuwa wakimiliki simu nzuri, na kompyuta (laptop) lakini kwa upande wa Ritha alikuwa hana hata simu ya mkononi, alitamani sana kuwa na maisha mazuri kama ya wenzake.

Siku moja akiwa anatoka chuo kuelekea nyumbani alikutana kaka mmoja aliyekuwa anaendesha gari aina ya Alteza "Mambo mrembo, unaelekea wapi mamii" Yule kaka alimwita Ritha huku akipunguza mwendo wa gari lake. Ritha alimtizama yule kaka na kusema "Hapana asante, nitapanda tu daladala" Yule kaka akaendelea kusema "Samahani lakini mrembo,nakuomba mara moja kuna jambo nilikuwa nataka nikuulize" Basi Ritha akasogea karibu "Uliza tu hakuna tatizo" Kumbe yule kaka alimwita kwa ukaribu ili ambembeleze apande kwenye gari yake. Haikupita muda Ritha alikubali kupanda kwenye lile gari na waliendelea kuzungumza na kufahamiana.

Yule Kaka alikuwa ni mfanyabiashara, anaitwa Godson.Kutokana na Ritha alikuwa hana simu ya mkononi Godson alimuahidi kumnunulia simu, na kesho yake angempelekea pale chuoni. Baada ya kumfikisha Ritha maeneo ya nyumbani, alimpatia kiasi cha shilingi elfu hamsini "Kiasi hiki kidogo cha pesa kitakusaidia, kwa nauli siku ya kesho, nimefurahi sana kukufamu Ritha, wewe ni mrembo ukinipa nafasi katika moyo wako, nakuahidi utafurahi sana" Ritha huku akiuma vidole vyake kwa aibu akapokea ile pesa na kusema "Asante sana Godson, ila naomba ukanishushe kwa pale mbele hapa Mama akiniona itakuwa balaa" Basi akasogea mbele kidogo na kumshusha.


Ritha alikuwa anatabasamu  huku akizungumza na nafsi yake "Jamani, leo ni siku yangu ya bahati, huyu kaka anaonekana ni mtu mwenye pesa sana, yaani amenipa shilingi elfu hamsini ijapokuwa sijamjibu chochote kuhusu ombi lake, mmmh yaani huko chuoni watanikoma, kwanza hii pesa niifiche vizuri, nikienda Mwenge nanunua viwalo kwa kwenda mbele" Siku hiyo Ritha alikuwa  na furaha sana. Kesho yake kama kawaida alikwenda chuoni, alipotoka tu alimkuta Godson anamsubiri.

 Moja kwa moja  walisalimiana na alimpakia katika gari lake wakiwa ndani ya gari Godson alimpa Ritha simu nzuri ya mkononi aina ya samsung galaxy. Ritha kwa furaha alimkumbatia Godson huku akimbusu na kusema "Asante sana, jamani nimefurahi sana, kweli nimeamini unanipenda Godson" Huku akicheka Godson akasema "Nimekupenda sana Ritha, ukiwa na mimi kila kitu unachokitaka utakipata nipo kwaajili yako".Na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mahusiano ya kimapenzi kati ya Ritha na Godson.

Maisha ya Ritha yalibadilika, kwani alianza kuvaa nguo za gharama na alikuwa hapandi daladala tena sasa alikuwa akijakuchukuliwa na kupelekwa chuo kila siku. Na hata wazazi wake walipokuwa wakimuuliza na kumkanya alikuwa awasikilizi aliwadharau na kuona Godson pekee ndiyo wa muhimu katika maisha yake. Aliishi maisha ya starehe sana na kuwadharau watu wengine bila ya kujali chochote. Hata marafiki zake walikuwa wakimshangaa "Mmmh ama kweli watu wanabadilika, sikuhizi Ritha anaringa sana tokea ampate huyo bwana mfanyabiashara" Walikuwa wakizungumza marafiki zake.

Baada ya miezi sita Ritha alipata ujauzito na kuamua kumwambia Godson ambaye alimwambia asijali atamlea vizuri.Basi akawa na kiburi kuwa ataolewa na Godson.Baada ya siku mbili tatu Ritha akiwa hana hili wala lile,  mara alipita muuzaji wa magazeti na moja kati ya yale magazeti ukurasa wa mbele kulikuwa na picha ya Godson na habari ikisema "Mfanyabiashara jambazi asotwa rumande" Ritha hakuamini alichokiona akasogea karibu na kununua lile gazeti kisha kusoma kwa umakini. Ni kweli habari ile ilimuhusisha Godson kutokana na kosa la ujambazi.

 Akiwa anaendelea kusoma ile habari akagundua kuwa Godson alikuwa na mke na watoto watatu. "Mungu wangu, inamaana Godson ni jambazi, na tena kumbe alikuwa na mke? Mama yangu nimekwisha.Nitafanya nini mimi na nina mimba ya miezi minne sasa na nyumbani lazima nitafukuzwa najuta mimi TAMAA IMENIPONZA. Alikuwa anaongea mwenyewe kama mtu aliyechanganyikiwa.

 Baada ya mwezi  mmoja kupita hali ilizidi kuwa mbaya kwani mawasiliano na Godson hayakuwepo tena. Na sasa aliwaomba msamaha wazazi wake na bila hiana wazazi walimsamehe.Hivyo walimlea hadi alipojifungua salama mtoto wa kiume. Na maisha ya Godson haikuelewweka yaliishia wapi kwani watu wengine walikuwa wanasema kuwa baada ya kuachiwa huru alihamia nchi nyingine pamoja na familia yake. 

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Safi sana godson!. umefanya la maana, bac huko uliko nakupa 5!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom