Pages

Alhamisi, Agosti 01, 2013

SIMULIZI FUPI ...YALAITI NINGELIJUA...... NI SIMULIZI INAYOISHIA PAPO HAPO.MTUNZI ...ADELA DALLY KAVISHE


  Nilijaribu kumuita lakini hakuniitikia na hata nilipomsogelea aliendelea kutembea bila ya kusimama. Nilijisikia vibaya sana, kwani nilijiona nimedharaulika. Hata watu waliokuwepo karibu walinitizama kwa nyuso za kuonyesha kuwa wananionea huruma. Nilibaki nikizungumza na nafsi yangu. "Hivi ni kweli Lema anaondoka na kuniacha, hapana siwezi kuamini nilimuamini kwa moyo wangu wote". 

Nilibaki nalia huku nikijisemea na moyo wangu "Ama kweli dunia hadaa, ulimwengu shujaa na asiyesikia la mkuu huvunjika mguu. Leo hii naumbuka kwa yote haya yaliyotokea katika maisha yangu, lakini mbona sijui kosa langu, inamaana ni kweli amenibadilikia kwa kiasi hiki. Lakini nakumbuka watu wengi walinikanya kuhusu tabia ya Lema lakini mimi nilikuwa nafanya mambo yangu kwa siri sana. 

Tizama sasa nabaki naumia na kuteseka peke yangu. Maisha yangu yote nilimuamini mwanaume huyu. Ndugu, jamaa na marafiki walinikanya lakini nilihisi labda wananione wivu leo hii najuta kwani siamini kama kweli Lema amenitendea yote haya. Alikuwa amejiinamia chini Salima huku akilia kwa uchungu. Maumivu makali moyoni mwangu eeh Mungu nisaidie.


Sikuamini kilichotokea, lakini ndiyo hali halisi maji yamekwisha mwagika hayazoleki tena.Nikiwa naendelea kuwaza alikuja rafiki yangu kipenzi Anna na kunishika begani huku akisema "Pole sana Salima muombe sana Mungu atakusaidia" Wakati Anna akiniliwaza machozi yaliendelea kunibubujika kwa wingi katika paji la uso wangu. Baadaye nilinyanyuka na kuelekea nyumbani taratibu.Maisha yangu yamekuwa na mtihani mkubwa sana. Baada ya kukutana na Lema mwanaume ambaye nilifikiri atakuwa ndiye chaguo la maisha yangu. Lakini haikuwa hivyo nikikumbuka siku ya kwanza tulikutana nikiwa natoka kazini kuelekea nyumbani nikiwa naendesha gari langu aina ya Rav 4. 

Katika maeneo ya Posta jioni usafiri huwa ni wa shida sana.Katika kituo cha daladala kulikuwa na watu wengi wakisubiri usafiri huo.Mimi nikiwa katika foleni kaka mmoja alikuja karibu na gari yangu na kunisemesha "Samahani dada, unaweza kunisaidia lifti" Nilimtizama yule kaka na kusema "Mimi naelekea Kijitonyama, kwani wewe unaenda wapi?" Akanijibu kwa haraka "Naelekea hukohuko dada yangu naomba unisaidie" Haikuwa kawaida yangu kuwapa lifti watu barabarani hususani mtu nisiyemfahamu lakini niliamua kumsaidia huyu kaka.


Siku moja Lema aliniomba tutoke pamoja kwani kuna jambo angependa kunieleza. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kwangu kwani nilikuwa napenda sana kuwa karibu na Lema wakati wote.Tukiwa tumeketi maeneo ya Makumbusho, Lema hakusita kuniambia juu ya hisia zake "Nikikutizama Salima wewe ni mwanamke mrembo sana, wakati mwingine najiona kama sistahili kuwa karibu yako lakini siku zinavyozidi kwenda, upole na ukarimu wako unanifanya nikupende zaidi. 

Natamani ungekuwa mpenzi wangu yaani uwe furaha ya milele katika maisha yangu, nakupenda sana Salima." Huku akiwa ananitizama alisema Lema.Mimi nilikuwa nimejiinamia kwa aibu "Asante Lema, hata wewe ni kijana mzuri sana.Ila siamini kama hauna mwanamke unayempenda." Lema alitabasamu nakusema "Nulijua utaniuliza hivyo, ni kweli nishawahi kuwa mpenzi lakini tulitenganana ni muda mrefu sasa niko peke yangu. Lakini moyo wangu umekutana na mwanamke mwenye kila sifa nilizokuwa nazihitaji ni wewe Salima naomba unipe nafasi katika moyo wako" Moyoni mwangu nilikuwa nikiwaza kwa kiasi gani nilikuwa natamani Lema awe mpenzi wangu na sasa hatimaye ndoto zangu zimekamilika.

Tulizungumza na baadaye nilimwambia Lema anipe muda nitafakari juu ya ombi lake. Baada ya wiki moja hatimaye tulifungua ukurasa mpya wa mapenzi motomoto. Nilimpenda sana Lema kwa moyo wangu wote. Nikiwa katika mahusiano ya kimapenzi na Lema sikuwahi kuwaambia marafiki wala ndugu zangu. Mapenzi haya niliyafanya siri kwa imani kwamba ipo siku Lema atakuja kujitambulisha nyumbani. Baada ya miezi mitatu, siku moja nilikutana na rafiki yangu mmoja anaitwa Sindy tulisalimiana "Jamani Salima nilikuwa nakutafuta sana, vipi mbona simu yako nikikupigia sikupati hewani au umebadili namba".

 Ni kweli nilikuwa nimebadilisha namba ya simu akaendelea kuzungumza "Unajua nilikuwa nakutafuta nikupe taarifa za msiba wa Belinda, si unajua alikuwa anaumwa sana" Nilishangaa kwani Belinda nilikuwa nikimfahamu "Maskini jamani, sikuwa na taarifa daah " Sindy akasema "Ndiyo hivyo ndugu yangu, huyu Lema atawamaliza wadada wa mjini" Nilihisi labda nilikuwa sijamsikia vizuri na kusema "Eti umesema Lema! Atawamaliza wadada wa mjini?".

 Niliuliza kwa shauku lakutaka kujua ni Lema yupi "Inamaana wewe humjui Lema kijana mmoja mtanashati. Anaishi karibu na maeneo ya pale kwenu yaani yule kijana anajijua kabisa ni muathirika lakini huwa anawaambukiza wadada wa mjini kwa makusudi" Nilihisi kuishiwa nguvu lakini ilinibidi nijikaze ili Sindy asielewe chochote.

Baada ya Sindy kuondoka, nilijikuta machozi yakinitoka na kuwaza sasa nitafanyaje kumbe Lema alikuwa na tabia chafu zilizojificha. Akili ikanituma niende kupima afya yangu kwanza. Maskini sintokaa nisahau ni kweli nilikuwa nimeathirika na moja kwa moja nilimjua aliyeniambukiza virusi vya UKIMWI na sasa nilirudi nyumbani huku nikiwa nimekata tamaa kabisa. Nilipofika nikiwa nmeketi kibarazani huku natafakari ghafla alipita Lema akiwa ameongozana na mwanamke nilimwita lakini hakuniitikia na hata niliposogea karibu alijifanya kuwa hanijui kabisa. Moyoni mwangu nilibaki naumia na kujuta kumuamini Lema kijana ambaye ni tapeli wa mapenzi na sasa ameniacha na maumivu ya milele.

Usimuamini mtu kwa haraka fahamu kuwa Majuto ni Mjukuu. na pia kumbuka usiache mbachao kwa msala upitao.

SIMULIZI FUPI ZITAKUWA ZINAKUJIA HAPA NI SIMULIZI AMBAYO ITAKUWA INAISHA KWA SIKU HIYOHIYO.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Jmn basi tumalizie ya bdo Mimi,tafadhl tunaomba.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom