MTUNZI - ADELA DALLY KAVISHE
"Nimechoka na kero za kila siku, sitaki kabisa yaani ni bora tu niondoke nirudi kwetu" Stara Alikuwa anazungumza kwa sauti iliyoonyesha kuwa na uchungu sana kutokana na tabia za mume wake ambaye alikuwa anachelewa kurudi nyumbani na akirudi anakuwa amelewa sana. Hali hii ilikuwa inamuumiza sana Stara ambaye alikuwa anavumilia kwasababu alikuwa anampenda mume wake.
Maisha ya Stara na mume wake kabla ya kuingia kwenye ndoa yalikuwa ni maisha yaliyojaa furaha na upendo, lakini baada ya kuingia kwenye ndoa mambo yalibadilika, Kutokana na hali hiyo Stara alikuwa akiumia sana ilifikia kipindi akawa anashindwa kuvumilia kutokana na tabia ya mume wake kumpiga, na kuna wakati alikuwa akirudi amelewa usiku wa manane alikuwa akimlazimisha Stara kuwa naye kimepenzi kwa nguvu hata kama Stara akisema anaumwa, yeye alifanya nguvu yaani alikuwa akimbaka mke wake kutokana na kumtaka kimapenzi kwa nguvu bila ya kumuandaa. Stara aliumia sana.
Na siku moja aliamua kwenda nyumbani na kumueleza Mama yake mzazi matatizo anayokutana nayo. Mama yake alimsikiliza kwa umakini na baadaye aliondoka na Stara hadi nyumbani kwa mume wake ambapo siku hiyo mume wa Stara alikuwa nyumbani, Baada ya Mama kuanza kumuuliza maswali kwanini anamtesa Stara. Mwanaume huyo alikuwa amenyamaza kimya huku akionekana kuwa mpole kana kwamba anaonewa, "Sikiliza nikuambie kijana, chonde chonde naokuomba usiniumizie mtoto wangu, kwani sintojali kama wewe ni mkwe wangu, nitakupeleka polisi, na tena jambo hili sijamfahamisha Baba Stara, sasa mimi naondoka lakini nakuambia kama mtoto wangu umemchoka ni bora umrudishe nyumbani kuliko kumpiga kama ngoma."
Aliongea Mama Stara huku akionekana kuwa na hasira. Mume wa Stara aliomba msamaha na kuahidi kuwa hatorudia tena. Baada ya siku mbili kupita tokea Mama Stara aende kuwasuluhisha pale nyumbani.
Siku hiyo Mume wa Stara alikuja nyumbani kama kawaida akiwa amelewa sana, alianza kumtolea maneno machafu mke wake "Wewe mwendawazimu, njoo hapa, nimekuambia sogea hapa" Stara alikuwa anatetemeka huku akisema "Lakini mume wangu si ulisema umeacha pombe, na hautonipiga tena" Kabla hajamaliza kuongea alivutwa kwa nguvu na kuanza kupigwa vibao katika paji la uso wake, alilia na kulalama kwa uchungu "Mimi siwezi kabisa haya maisha, nimechoka, sitaki mimi, kila siku unanipiga, nimekukosea nini mimi, naondoka narudi kwetu, nimekuchoka sikutaki niachie unaniumiza".
Aliendelea kumpiga bila ya huruma huku akisema "Siwezi kukuacha wewe ni wa kwangu tu, na utakufa na mimi" Stara alikuwa anaogopa alijivuta kutoka kwenye mikono ya mume wake na kukimbia huku mume wake akimkimbiza. Kwa bahati nzuri alikutana na taksi akapanda haraka na kuelekea nyumbani Baba na Mama yake walipomuona walihuzunika sana na moja kwa moja walipiga simu polisi na Mume wa Stara alikamatwa na kwenda kufunguliwa mashtaka ya kumpiga mke wake.
Stara alirudi nyumbani kwao na kuamua kuishi na wazazi wake. Mume wake aliachiwa huru, baada ya kulipa faini, lakini bado anaendelea kumsumbua Stara na kumtumia ujumbe kuwa "Anampenda na kamwe hawezi kumuacha" Lakini Stara ameamua kuendelea na maisha yake. Huku akiwa makini na kutakiwa kutoa taarifa polisi endapo kama atafanyiwa jambo lolote na aliyekuwa mume wake.
NI VYEMA KUTOA TAARIFA ILI USAIDIWE INAPOTOKEA UNAFANYIWA UKATILI
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni